Thursday, 10 October 2019
Mafuriko yasababisha vifo vya watu sita Mkoani Tanga
Watu sita wamefariki dunia na kaya kadhaa Wilayani Korogwe hazina mahala pa kuishi baada ya nyumba zao kuanguka na zingine kujaa maji kutokana na mvua kubwa iliyonyesha kuanzia saa 2 usiku wa Oktoba 8 hadi majira ya saa 9 alasiri Oktoba 9.
Kwa mujibu wa kamanda wa Polisi mkoa wa Tanga SACP Edward Bukombe alisema kuwa mvua hiyo iliyonyesha katika vijiji vya Halmashauri ya Wilaya ya Korogwe katika milima ya Usambara ilisababisha barabara kuu ya Arusha -Segera -Dar eneo la Msambiazi Korogwe mjini kutopitika na kufungwa kwa muda kwa tahadhari za kiusalama.
Mkuu wa wilaya ya Korogwe Kissa Gwakisa alithibitisha kwa barabara hiyo kufungwa kwa muda na hadi kwa muda wa saa mbili na baadae kuendelea na safari zake kati ya Tanga, Dar es salam, Lushoto, Moshi, Arusha na Nairobi kupitia Namanga mkoani Arusha yaliruhisiwa.
Akizungumzia vifo vya watu sita, Kamanda Bukombe amesema kuwa watu hao ambao majina yao bado hayajulikana ni katika kijiji cha Dindira mwanamke mmoja na watoto wake wawili waliangukiwa na nyumba usiku wakati katika kijiji cha Bungu msichana mmoja anayejulikana kwa jina la Asha Yahaya Ambanyonge alikuwa kalala na wadogo zake wawili ambapo nao wameangukiwa na nyumba na kufariki papo hapo.
Wilayani Muheza katika barabara ya Amani -Muheza kata ya Mbaramo eneo la Msangazi mawasiliano ya barabara yalifungwa kwa muda kutokana na mafuriko yaliyoziba njia.
CHANZO: MPEKUZI
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment