Saturday 16 March 2019

Polisi wakiri kumbambikia kesi ya mauaji mfanyabiashara




Mfanyabiashara huyo ni yule ambaye juzi Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP), Biswalo Mganga, alimzungumzia kuwa baadhi ya askari wa Jeshi la Polisi walimbambikia kesi ya mauaji huko Tabora.

Akizungumza na waandishi wa habari jana jijini Dar es Salaam, Msemaji wa Jeshi la Polisi nchini, Ahmed Msangi, alisema awali walipokea barua ya malalamiko kutoka kwa mfanyabiashara huyo.

Alisema baada ya kupoka, Ofisi ya Upelelezi wa Makosa ya Jinai ilimtuma ofisa wake mwenye cheo cha juu kwenda Tabora kufanya uchunguzi na kwamba hadi sasa anaendelea kuukamilisha ili hatua zichukuliwe dhidi ya waliohusika.

"Mpaka sasa yuko huko, kiufupi kwa taarifa ya awali aliyotuletea ofisa wetu ni kwamba kulikuwa na ukweli kwamba mwananchi yule alikuwa ameonewa," alisema Msangi.

“Tunaamini na kuelekezwa siku zote tunapofanya kazi za polisi tuzifanye kwa weledi na kuzingatia misingi ya sheria, kama mtu amekwenda kinyume hatuwezi kukaa kimya, hatua stahiki zitachukuliwa lisijirudie tena,” alisema.

Awali, akizungumza na Nipashe, Msangi alisema baada ya Jeshi la Polisi kupokea barua ya mfanyabiashara huyo, walimtuma ofisa wao lakini wakati akiendelea na upelelezi ndipo wakaona kwenye magazeti.

Juzi, DDP aliliumbua Jeshi la Polisi baada ya kueleza baadhi ya askari wake walivyombambikiza kesi ya mauaji mfanyabiashara Sadiki baada ya kumpoka fedha.

Kutokana na kadhia hiyo, Rais John Magufuli aliagiza hatua zaidi zichukuliwe dhidi ya wote waliohusika katika tukio la kumbambika kesi ya mauaji namba 8/2018 mfanyabiashara huyo.

Akizungumza na waandishi wa habari juzi jijini Dodoma, DPP Mganga alisema Machi 6, mwaka huu, Sadiki aliandika barua ya wazi kwa Rais Magufuli kupitia moja ya magazeti ya kila siku nchini, akilalamika kubambikwa kesi hiyo mkoani Tabora.

Mganga alieleza kuwa, baada ya mfanyabiashara huyo kukamatwa na askari polisi, walimnyang’anya Sh. 788,000, simu ya mkononi na mali alizokuwa amenunua kwa ajili ya wakulima wakati anakwenda kufanya ununuzi.

"Kwa mujibu wa malalamiko yake yaliyoandikwa kwenye gazeti moja, baada ya kukamatwa aliwekwa kwenye Kituo Kikuu cha Polisi Tabora kwa kumbambikizia kesi ya kuvunja na kuiba na alikaa kituoni kwa wiki moja na alipopelekwa mahakamani, alisomewa shtaka la mauaji," Mganga alieleza.

Mkurugenzi huyo alisema kuwa baada ya Rais kusoma barua hiyo, aliagiza Ofisi ya Taifa ya Mashtaka ifuatilie malalamiko ya mwananchi huyo kwa haraka ili kujua ukweli wake.


“Baada ya maelezo hayo, Ofisi ya Taifa ya Mashtaka ilifuatilia suala hilo na kufanya mahojiano na mlalamikaji pamoja na kupitia nyaraka mbalimbali zilizopo katika Kituo cha Polisi cha Tabora Mjini zinazohusiana na suala lake," alisema.


Katika kufuatilia malalamiko hayo, Mganga alisema Ofisi ya Taifa ya Mashtaka imebaini malalamiko ya mfanyabiashara huyo ni ya kweli, kwa kuwa kitabu cha kuzuia wahalifu (detention register) kilichopo katika kituo hicho cha polisi kinaonyesha Sadick alikamatwa Juni 21, 2018, kwa kosa la kuvunja nyumba usiku na kuiba na aliingizwa mahabusu ya polisi saa tisa alasiri.

Alisema kitabu hicho pia kinaonyesha Juni 29, 2018, mlalamikaji alitolewa mahabusu saa mbili asubuhi na kupelekwa mahakamani na tarehe hiyo hiyo, alifunguliwa kesi ya mauaji namba 8/2018 ikionyesha Mei 6, 2018, akiwa Barabara ya Kazima, Tabora Mjini, alimuua Jackson Thomas.

Mganga alisema wakati wa kufuatilia malalamiko hayo, ofisi yake ilibaini kuwa Julai Mosi, 2018, alikamatwa Edward Matiku Nduli kwa kosa la kuvunja nyumba usiku na kuiba. Mnamo Julai 16, 2018, naye aliunganishwa katika shauri la mauaji namba 8/2018 akihusishwa na mauaji dhidi ya Jackson Thomas.


NIPASHE

No comments:

 

ADVERTISE WITH US

AFRICAN FASHION

PLACE YOUR ADS HERE!