BAGAMOYO ni mji wa kihistoria maarufu sana nchini na duniani kwa ujumla. Hii inatokana na ukweli kwamba ulikuwa makao makuu ya serikali ya wakoloni wa Kijerumani Afrika Mashariki, iliyojumuisha nchi za Tanganyika, Rwanda na Burundi.
Baada ya wazungu kuligawa bara la Afrika kupitia mkutano wa Berlin mwaka 1884-1885, Tanganyika, Rwanda na Burundi zikawa nchi moja zilizowekwa chini ya himaya ya Wajerumani ambayo makao yake makuu yalikuwa ni Bagamoyo kuanzia mwaka 1886 hadi 1891 kabla ya kuhamishiwa Dar es Salaam mwaka 1891 hadi 1919.
Bagamoyo ilikusanya wafanyabiashara kutoka mataifa mengi duniani wakiwemo waliotoka Uarabuni, Uajemi, India, China na Ulaya ambao walileta bidhaa mbalimbali kama vile nguo, majambia, silaha, sahani, vioo, shanga, viungo, vyakula n.k. Wafanyabiashara hao walibadilishana bidhaa na wenyeji kwa kuchukua pembe za ndovu, watumwa, madini, ngozi za wanyama, magamba ya kobe, miti ya mikoko na kadhalika.
Huku wakisaidiwa na pepo za kasi na kusi, wageni waliendesha mashua zao hadi Pwani ya Afrika Mashariki. Mnamo karne ya 13 Washirazi waliujenga mji wa Kaole ambao ni miongoni mwa miji ya kale kabisa Afrika Mashariki ambako dini ya Kiislamu ilishika mizizi.
Misheni ya kwanza Afrika Mashariki pia ilianzishwa Bagamoyo na Fr. Anthony Horner mnamo mwaka 1868 ambapo mwaka huohuo Kanisa Katoliki liliadhimisha miaka 150 ya uinjilishaji. Pamoja na kwamba Bagamoyo tayari ilikuwa inakaliwa na waislamu wengi, wamisionari pia waliamua kujenga kanisa la kwanza Afrika Mashariki mwaka 1872.
Wapelelezi/wavumbuzi wengi maarufu duniani katika harakati zao za kuchunguza rasilimali za Afrika walipitia Bagamoyo kama vile John Speke, Richard Burton, Henry Stanley, James Grant n.k lakini pia mwili wa Dk David Livingstone alipofariki kule Zambia ulipitishwa Bagamoyo kabla ya kusafirishwa kwenda kuzikwa katika eneo la makaburi ya watu maarufu Uingereza, Westminster Abbey mwaka 1873.
Mbali na Bagamoyo kuwa mlango wa dini zote mbili; Ukristu na Uislamu, ilikuwa ni njia ya misafara ya watumwa na wapelelezi mashuhuri hadi kuwa makao makuu ya kwanza ya Tanganyika na Afrika Mashariki.
Bagamoyo imehifadhi siri nyingi za mali kale ambazo watanzania wengi hawazijui. Na sasa mji huu unatarajiwa kuingizwa katika orodha ya Urithi wa Dunia na Shirika la Umoja wa Mataifa la Elimu, Sayansi na Utamaduni (UNESCO).
Mji Mkongwe
Ni mji wenye mvuto uliopo pembezoni mwa ufukwe wa bahari ya Hindi wenye majengo mengi ya kihistoria na mitaa miembamba, eneo ambalo Wajerumani waliliita “Kaiser strasse” lakini kwa sasa likijulikana kama “Indian street”.
Majengo yake mengi yalijengwa kwa mawe ya matumbawe pia walitumia chokaa (lime mortar) iliyotokana na matumbawe na kuezekwa kwa miti ya mikoko.
Ujenzi wa majengo haya una usanifu wa Kiarabu, Kihindi na Kijerumani huku mengine yakiwa na usanifu mchanganyiko. Miongoni mwa mali kale zinazopatikana kwenye mji mkongwe ni kama ifuatavyo. Ngome Kongwe Hili ni jengo kubwa lenye kupendeza machoni pa wengi huku wenyeji wengi wa Bagamoyo wakilifahamu kama “Jumba la Dhahabu”.
Ngome Kongwe ni jumba la kwanza la mawe katika mji huu mkongwe ambalo lilijengwa na mwarabu tajiri, Abdallah Selemani Marhabi kwenye miaka ya 1860 kama sehemu yake ya makazi. Jumba hili lilimvutia Sultani Barghash wa Zanzibar ambaye alilitumia kama sehemu ya kufikishia watumwa wake kuanzia mwaka 1870 hadi 1884.
Wajerumani walipotawala nao walilitumia jengo hili kama ngome yao ya jeshi kabla ya Waingereza nao kulitumia kama gereza kuanzia mwaka 1919 hadi 1961 tulipopata uhuru.
Kwa sasa jengo hili linahifadhiwa na Idara ya Mambo ya Kale na ni kivutio cha watalii Boma la zamani Ni moja ya majengo ya kuvutia katika mji mkongwe wa Bagamoyo. Boma ilijengwa na wajerumani mwaka 1895-1897 na kutumika kama makazi na ofisi za gavana.
Jengo hili la ghorofa mbili lina urefu wa mita 42 na upana wa mita 33, sehemu ya chini kuna ukumbi wa mikutano, vyumba sita vya ofisi, jiko, vyumba sita vya stoo, vyumba viwili vya kulala na choo kimoja.
Sehemu ya juu kuna jiko, vyumba 10 vya kulala, ukumbi mmoja na vyoo viwili. Jengo hili pia lilitumiwa na waingereza enzi za ukoloni.
Mnara wa Wissman Mnara huu ulijengwa na gavana Herman Wissman mwaka 1894 mbele ya Boma ikiwa ni kumbukumbu ya askari wa Kijerumani waliokufa katika mapigano dhidi ya Waarabu na Waafrika walioongozwa na Abushiri ibn Salim.
Mnara uliharibiwa na waingereza kwenye miaka ya 1940. Mbele ya mnara huu kulikuwa na uwanja wa wazi wenye urefu wa mita 200 ambao ulitumika kwa ajili ya michezo.
Mgahawa wa Kiarabu Huu ni mgahawa wa kale uliotumiwa na watu kupata chai na kahawa ambao ulijengwa kwenye miaka ya 1860 na Abdallah Selemani Marhabi.
Baadaye jengo la mgahawa huu maarufu kama (Arab Tea House) lilitumika kama hospitali mwaka 1912 na baadae Waingereza walilitumia kama shule, benki na ofisi. Kwa sasa jengo hilo bado lipo kwenye hali nzuri na linatumiwa na halmashauri ya wilaya Bagamoyo.
Posta ya zamani Ni jengo ambalo lilikuwa posta ya kwanza na kituo cha kwanza cha simu Afrika Mashariki. Jengo hili lilijengwa kwenye karne ya 19 na tajiri wa kihindi Sewa Haji kabla ya kuwapatia Wajerumani mwaka 1896.
Mwaka 2009 Millennium Hotel Group walilikarabati jengo hili na kuanza kulitumia kama hoteli kwa sasa linajulikana kama Millennium Old Post Office Hotel. Shule ya mwambao Ukiachilia mbali posta na simu ya kwanza, Bagamoyo pia ndipo ilijengwa shule ya kwanza Afrika Mashariki.
Shule hii ilijengwa na Sewa Haji ambaye aliwapatia Wajerumani mwaka 1896 kwa makubaliano ya wakoloni kuitumia shule hiyo kufundishia watoto wa rangi zote kuanzia Waafrika, Waarabu, Wahindi na Wazungu.
Makaburi ya Mwanamakuka Ni miongoni mwa makaburi maarufu yaliyopo kusini mwa jengo la Ngome Kongwe katikati ya makaburi ya Wajerumani na shule ya msingi Mwanamakuka mbele kidogo ya Chuo cha Sanaa.
Haya ni makaburi ya kale katika mji wa Bagamoyo na jumla yako 35. Kaburi kubwa kuliko yote ambalo limezungushiwa ukuta inasemekana lilikuwa ni la mtu tajiri kutoka Tabora aliyejulikana kwa jina la Mwanamakuka.
Makaburi haya ni ya mwaka 1793 hivyo basi kumbe na matajiri waafrika nao walikuwepo Bagamoyo tangu mwanzo. Eneo la kunyongea Katika eneo la Badeco beach hotel unakutana na mnara wa mashujaa ambao walinyongwa na Wajerumani baada ya kuupinga ukoloni.
Mashujaa hawa waliongozwa na Abushiri ambaye alikamatwa na kunyongwa kule Pangani mkoani Tanga mwaka 1889. Mashujaa walionyongwa mahali hapa ni pamoja na Jahazi, Simba Mbili, Marera, Mbomboma, Salim bin Abdallah, Pori, Kriolhe, Peni na Kisoko.
Makaburi ya Wajerumani Hapa kuna jumla ya makaburi 20, miongoni mwa hayo 18 ni ya askari wa Kijerumani waliofariki kwenye vita ya Abushiri. Kaburi moja ni la muuguzi Bi Antonie Baeumler na jingine la Gretel Schuller.
Pembeni mwa makaburi haya kuna kaburi moja la Mkuu wa wilaya Mwingereza, William Bamphilde ambaye inasemekana alijiua kwa kujipiga risasi baada ya kumfumania mke wake na mfanyakazi wao wa ndani.
Nyumba ya Liku Nyumba hii inapatikana ndani ya mji mkongwe wa Bagamoyo Ilijengwa mnamo karne ya 19 na Abdallah Suleimani Marhabi baadae ilikuja kuuzwa na Rhatu Bhimji kwa Wajerumani ambao waliitumia kama makao makuu yao ya utawala na sehemu ya makazi.
Mpelelezi maarufu kutoka Ujerumani, Emin Pasha alianguka kutoka ghorofa ya kwanza ya jengo hili wakati akishangilia. Soko la zamani Soko hili limekuwepo tangu karne ya 19 na hapo mwanzo lilikuwa ni eneo la wazi ambalo lilitumika kwa ajili ya biashara ya watumwa na pembe za ndovu.
Wenyeji wanaamini kulikuwa na tanuru kutokea kwenye soko hadi baharini ambapo watumwa walipitishwa wakiwa wamefungwa macho. Mwaka 1898 Wajerumani walijenga jengo kwenye eneo la soko la zamani kwa kiasi cha rupia 9,000 na kulitumia kama soko la kawaida lenye maduka na migahawa.
Hizo ni baadhi ya malikale zinazopatikana katika Mji Mkongwe wa Bagamoyo lakini kuna mambo mengi sana ambayo watu wengi hawayajui.
Ni vyema watanzania tukajenga utamaduni wa kutembelea maeneo yetu ya kihistoria ili tuweze kujifunza kwani serikali imeturahisishia sana kwa kuweka viingilio vidogo vya kutembelea maeneo haya kwa mfano kiingilio cha Mji Mkongwe ni 2,000/= tu kwa mtu mzima na mtoto ni 1,000/- unafaidi mambo yote haya.
No comments:
Post a Comment