Lishe bora wakati wa ujauzito ni muhimu sana, kwani lishe hii hutumika kwa mama na mtoto anaendelea kukua tumboni. Kwa kawaida mahitaji ya chakula na virutubisho mwilini mwa mwanamke huongezeka wakati wa ujauzito na kadri ujauzito unavyoendelea kukua, virutubisho hivyo hutumika kujenga mwili wa mama na mtoto.
Hivyo maamuzi ya lishe au lishe mama anayopata huathiri pia maendeleo ya mtoto anayekua mwilini mwake. Tutaona vyakula muhimu vya kuzingatia lishe bora wakati wa ujauzito na baadhi ya vitu vya kukwepa.
Mlo kamili
(balanced diet), ni muhimu kwa ajili ya maendeleo mazuri ya afya ya
mjamzito na mtoto tumboni. Pamoja na mlo kamili mjamzito hupewa
virutubisho ziada (supplements) kwa ajili ya kuongeza madini kama ya
chuma na Foliki. Mlo kamili unajumuisha vyakula vya wanga, protini,
mafuta, vitamini, madini na maji kama inavyochambuliwa hapa chini;
Nafaka na Vyakula vya Wanga.
Vyakula hivi
huupa mwili nguvu za kufanya kazi ikiwemo ukuaji wa mtoto tumboni.
Vyanzo vya wanga ni kama nafaka mbalimbali(mahindi,mtama,ulezi n.k),
viazi, ndizi, mihogo. Ni vizuri mjamzito awe anapata nafaka kamili(whole
grains) kama mahindi, ngano na mchele usiokobolewa; cereals n.k
Nyama, Samaki na Vyakula vya Protini.
Hivi ni
muhimu kwenye kuujenga mwili, hasa kipindi cha miwezi wa 4 mpaka wa 9
ambacho viungo mbalimbali vya mtoto vinajengwa. Ni muhimu mama apate
vyakula vya protini vya kutosha ili kuhakikisha ukuaji wa mtoto unaenda
vizuri. Nyama za kuku, ng’ombe, mbuzi, senene, panzi na wanyama wengine ;
vyanzo vya protini za mimea kama maharage, soya, njugu, njegere,
karanga,korosho n.k . Samaki, maziwa, mayai ni vyanzo vingine vya
protini muhimu.
Vyakula vya Mafuta.
Hutumika
kwenye kuupatia mwili nguvu pamoja na ujengaji wa seli za mwili. Mara
nyingi vyakula kama nyama, karanga, ufuta, alizeti,senene, panzi, samaki
na matunnda kama maparachichi huwa na mafuta. Ni vizuri kutumia mafuta
yatokanayo na mimea ili kupunguza mafuta yenye lehemu(cholesterol)
nyingi.
Mboga za Majani na Matunda.
Matunda na
mboga za majani ni sehemu muhimu sana ya mlo wakati wa ujauzito, kwani
huupatia mwili vitamini, madini na kambakamba kwa ajili ya kulainisha
chakula. Vitamini husaidia kuimarisha kinga ya mwili sambamba na
ufanyaji kazi wa mwili. Madini kama ya chuma, kalsiamu, zinki, madini
joto(Iodine) na magneziamu ni muhimu kwa ukuaji salama wa mtoto tumboni
mwa mama.
Vitamini B9
(Foliki asidi) na madini ya chuma hutolewa kama virutubisho ziada
kliniki wakati wa ujauzito ili kutosheleza mahitaji ya mwili na kuzuia
hatari ya upungufu wa damu kutokea.
Maji ni
muhimu kwenye mmenyenyo na unyonywaji wa chakula, pia husaidia kuzuia
choo kigumu, mwili kuvimba na maambukizi ya mfumo wa mkojo (UTI).
Inashauriwa mjamzito anywe maji si chini ya lita 2.3 kwa siku, yanaweza
kuwa katika chai, juisi, soda, au maji yenyewe. Ni vema zaidi kama
akinywa maji kama maji zaidi na kupunguza vinywaji kama soda.
Mfano wa Mpangilio wa Mlo.
Ili kuhakikisha mlo kamili mjamzito anaweza kufuata mfano wa mpangilio wa mlo ufuatao;
Mfano,
- Mlo wa Asubuhi: A - Chungwa/ Embe/ Ndizi mbivu/ Parachichi, B - Mkate/ Maandazi/ Chapati/ Vitumbua,Uji C - Karoti D - Mayai, E - Maziwa/ Mtindi/ Siagi/ Maziwa ya Soya
- Mlo wa Mchana: A - Parachichi/ Papai/ Ndizi/ Embe na chungwa, B - Ugali/ Wali/ Ndizi/ Makande/ Tambi C - Mchicha/ matembele/ Mnavu/ Kisamvu/ Spinach/ Kabeji, D - Maharage/ Samaki/ Kuku/ Njugu/ Nyama/ Dagaa E - Maziwa/ Mtindi/ Siagi/ Maziwa ya Soya.
- Mlo wa Usiku: A - Parachichi/ Papai/ Ndizi/ Embe na Chungwa, B - Wali/ Ndizi/ Viazi/ Tambi/ Chapati C - Mchicha/ Matembele/ Mnavu/ Kisamvu/ Spinach/ Kabeji, D - Maharage/ Samaki/ Kuku/ Njugu/ Nyama/ Dagaa E - Maziwa/Mtindi/Siagi/Maziwa ya Soya.
Vitu na Vyakula vya kuepuka/kupunguza
- Matumizi ya Pombe wakati wa ujauzito huathiri mtoto. Haishauriwi kutumia pombe kabisa!
- Uvutaji Sigara
- Kupunguza unywaji wa kahawa au vinywaji vyenye caffeine nyingi.
- Samaki aina ya papa, swordfish, tilefish na king mackerel kwani wana mekuryi kwa wingi amabayo ni mbaya kwa afya.
No comments:
Post a Comment