Martha Malambi (25), baada ya shambulio hilo la Februari 17 lililosababisha kumpoteza mtoto wake wa kiume, Godfrey David (mwaka mmoja na miezi miwili) ambaye alikufa na baadaye maiti yake kusombwa na maji, kwa sasa anaendelea na matibabu katika Taasisi ya Mifupa na Mishipa ya Fahamu Hospitali ya Muhimbili (MOI).
Ni saa 11:00 jioni katika kijiji cha Ukutu, Kata ya Bwakilachini, Martha akiwa amembeba mwanaye mgongoni, anafika katika Mto Mgeta baada ya kutembea mwendo wa nusu saa akitafuta maji.
“Nilikwenda mtoni kuchota maji nikiwa nimembeba mwanangu, baada ya kujitwisha kichwani wakati naanza kutoka mtoni mamba mkubwa alinivamia kwa nyuma, alinikamata mguu sehemu ya msuli na paja akanivuta mtoni,” anasimulia Martha aliyepambana kijasiri na mamba huyo. Anasema baada ya kudondoka mamba huyo alimvuta mpaka mtoni kwenye kina kirefu kisha kumzamisha chini ya maji, “Nilimhisi mwanangu namna alivyohangaika na maji aliyokuwa anakunywa baada ya sekunde chache alituibua tena juu hapohapo kitenge kikafunguka na mtoto akaondoka na maji, nilipata uchungu mkubwa,” anasema.
Anasema mamba alizidi kumbana zaidi na kumvutia bondeni. Wakati wa purukushani hizo alikuwa amembana mguu kwa meno yake na kuacha kiwiliwili, hivyo akawa anapiga kelele kuomba msaada huku akiendelea kupambana naye.
Mama huyo wa watoto wawili, huku mmoja aliyemuacha nyumbani akiwa na umri wa miaka mitano, anasema alitumia nguvu zaidi kupanua mdomo wa mamba ili kumpa maumivu, lakini aliendelea kumshinda nguvu kutokana na urefu wa mnyama huyo kuwa maradufu ya urefu wake.
“Kutokana na purukushani ile, aliona hajanidhibiti vizuri kwa sababu alinishika mguu mmoja, akajaribu kusogea kwenye kina kifupi cha maji ili anikamate vizuri,” anasimulia Martha.
Anasema hatua ya mamba huyo kusogea kwenye kina kifupi cha maji ya mto kutoka kina kirefu, kilimsaidia kuyafikia matete (magugu maji) hivyo aliyashika na kuyang’ang’ania kwa nguvu huku akiomba msaada kwa kupiga kelele.
Mwanamke huyo anasema ilikuwa bahati kwake, kwani kulikuwa na wavulana ambao hawakuwa mbali na mto huo ambao walisikia kelele za kuomba msaada na kuwahi eneo hilo, wawili wakiwa na magongo wawili wengine mapanga hivyo kuingia kwenye maji na kuanza kumshambulia mamba huyo.
Pamoja na msaada huo wa watu, mamba aliendelea kung’ang’ania mguu wake lakini mashambulizi yalivyozidi mamba alionekana kuchoka na kupata maumivu, hivyo kuuachia mguu na kuzama majini.
Hata hivyo, Martha anasema kabla hajaokolewa alikata tamaa kwani alihisi tayari amekufa: “Yule mamba mkubwa karibu mara mbili ya mwili wangu aliniogopesha sana, sikuwa nimewahi kumuona kwa macho yangu kabla ya siku hiyo. Viboko nawajua vizuri kwa sababu nimewahi kuwaona mara nyingi kijijini.
“Wale vijana walinichukua na kunipeleka nchi kavu baadaye Zahanati ya Lukumi, ambako walinipatia huduma usiku kucha, asubuhi ya Februari 18 walinisafisha vizuri maeneo yote yaliyoathiriwa na kucha na meno ya mamba huyo.”
Anasema kutokana na ukubwa wa majeraha hayo na mguu kuvunjika, alihamishiwa Hospitali ya Mkoa wa Morogoro ambako baada ya kuhudumiwa takriban siku tano walimweleza kuwa tatizo lake inabidi apelekwe Muhimbili. Safari yake kwenda MOI ilianza akiwa yeye na wauguzi tu, alipofika alipokelewa na kupelekwa chumba cha upasuaji ambako alirekebishwa maeneo ya nyonga ambayo pia yaliathiriwa.
“Nimefika MOI nikiwa peke yangu. Sina ndugu hapa Dar es Salaam wala ndugu yeyote kutoka nyumbani ambaye amefika hospitali tangu siku hiyo. Nashukuru wauguzi na madaktari wamekuwa wakinisaidia wakati wote, ninapata matibabu vizuri, ninapata chakula, nashukuru kwa hilo” anasema na kusisitiza kuwa familia yake ni maskini, hivyo hana mawasiliano nao kwani simu aliyoitegemea ilisombwa na maji.
Uhaba wa maji Ukutu
Martha anayeishi na wazazi wake kijijini hapo, anasema hawawezi kuepuka kufuata maji mtoni kwa kuwa hakuna chanzo kingine cha maji kijijini zaidi ya mto Mgeta, miaka yote wamekuwa wakichota maji hapo.
“Miaka yote tuliyoishi pale hatujawahi kusikia tukio la shambulio la mamba eneo hilo. Nimezaliwa na kukulia hapo na wazazi wangu pia wamezaliwa na kukulia hapohapo. Wanyama wapo kwenye huo mto, hasa viboko, maji yakijaa wanatembea hadi kwenye makazi ya watu lakini mamba hawakuwahi kuwapo eneo hilo zaidi na maeneo ya mbali,” anasema.
Martha ambaye ni mkulima wa mpunga na mahindi anaainisha kuwa miaka kadhaa iliyopita, kulikuwa na mabomba matatu ya jumuiya katika kijiji chao lakini kwa zaidi ya miaka minne sasa hayafanyi kazi tangu yalipoharibika.
MOI kumfanyia upasuaji
Daktari bingwa mwandamizi wa upasuaji mifupa MOI, Paul Marealle anathibitisha kumpokea Martha na kwamba, tayari wameanza kumpatia matibabu kinachosubiriwa ni upasuaji.
“Alipata jeraha kubwa la kuvunjika mfupa wa paja na vidonda kwenye eneo la paja na mguu wa kulia,” anasema Dk Marealle na kuongeza:
“Wagonjwa wengi wa namna hii wanakuwa wamepoteza damu, hivyo tunawaongezea na tunawapatia huduma ya karibu kabisa, kwa sasa tumemtibu na majeraha yake yamepona, kwa hivyo tutamrudisha chumba cha upasuaji kushughulika na mfupa wake ambao umevujika.
“Tunajaribu kuondoa uchafu na sumu yote ambayo inaonekana kwa macho na wanawekwa kwenye antibiotic maalumu na kurudishwa chumba cha upasuaji mara kwa mara.”
Huduma kwa majeruhi wa mamba
Anasema huduma ya kwanza ambayo mgonjwa aliyeng’atwa na mamba anafaa kupewa ni kuzuia damu isitoke, kwa kuwa hupoteza damu nyingi huku akisisitiza majeruhi yeyote lazima aangaliwe kwa namna anavyobebwa na kuhudumiwa kulingana na majeraha yake.
“Mamba anakula vitu vingi hivyo ana sumu kali ya vijidudu vinavyokaa kwenye meno yake vinavyotokana na uchafu, kwa hivyo kitu cha kwanza lazima kuhakikisha kidonda kimesafishwa vizuri hata na maji yanayotiririka,” alisema.
Dk Marealle anasema iwapo mgonjwa asipopewa tiba ya antibiotic kwa haraka, kinachoweza kutokea ni kufa kwa ngozi, misuli na mishipa ya fahamu hivyo madhara yake ni kukatwa sehemu husika.
No comments:
Post a Comment