MAHAKAMA ya Hakimu Mkazi Kisutu, Dar es Salaam imepanga Aprili 11, mwaka huu kuwasomea maelezo ya awali aliyekuwa Rais wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), Jamal Malinzi na wenzake wanaokabiliwa na mashitaka ya utakatishaji fedha, baada ya upelelezi kukamilika.
Mbali ya Malinzi, washitakiwa wengine ni aliyekuwa Katibu Mkuu wa TFF, Mwesigwa Selestine na aliyekuwa Mhasibu, Nsiande Mwanga ambao wanadaiwa kutakatisha dola za Marekani 375,418.
Mwendesha Mashtaka wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru), Leonard Swai amedai leo mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Wilbard Mashauri kuwa upelelezi wa kesi hiyo umekamilika.
Ameiomba mahakama hiyo kupanga tarehe nyingine kwa ajili ya kuwasomea washtakiwa maelezo ya awali.
Hakimu Mashauri ameahirisha kesi hiyo hadi Aprili 11, mwaka huu kwa ajili ya washitakiwa kusomewa maelezo ya awali.
Washitakiwa kwa pamoja wanakabiliwa na mashtaka 28, ikiwemo ya utakatishaji fedha ambazo ni Dola za Marekani 375,418 na washtakiwa wote wamerudishwa rumande.
No comments:
Post a Comment