ASKARI wa Jeshi la Wananchi nchini (JWTZ) Ramadhan Mlaku (28) leo amefikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu akikabiliwa na shtaka la mauaji ya askari mwenzie, Simon Nestory.
Mshtakiwa huyo amesomewa shtaka lake na Wakili wa Serikali, Mosie Kaima, mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu,Thomas Simba, ambapo ameiambia mahakama kuwa mshtakiwa anakabiliwa na kosa moja la mauaji.
Imeelezwa mahakamani hapo kuwa mshtakiwa huyo ambaye ni mwanajeshi wa Kambi ya Makongo alitenda kosa hilo Oktoba 30, 2017 akiwa Makao Mkuu ya JWTZ Upanga, Ilala, Dar es Salaam ambapo alimuua askari mwenzie Sajenti Nestory.
Baada ya kusomewa shtaka hilo, Hakimu Simba amesema mshtakiwa haruhusiwi kukiri wala kukana kosa hilo kwa sababu mahakama hiyo haina mamlaka ya kusikiliza kesi za mauaji.
Simba amesema kosa hilo halina dhamana kwa mujibu wa sheria na wakili Mosie ameiambia mahakama kuwa upelelezi wa kesi hiyo haujakamilika, akaiomba kesi iahirishwe hadi tarehe nyingine.
Hakimu Simba ameutaka upande wa mashtaka kuhakikisha unakamilisha upelelezi kwa wakati, ambapo ameahirisha kesi hiyo hadi Machi 28, mwaka huu.
No comments:
Post a Comment