HOSPITALI ya Rufaa ya Kanda ya KCMC iliyoko mkoani Kilimanjaro, ilipokea jumla ya wagonjwa wa saratani 3,450 kati ya Desemba, 2016 na Desemba, 2017 katika kitengo cha saratani cha hospitali hiyo (KCMC CCC).
Idadi hiyo ni kubwa ikilinganishwa na mategemeo ya kupokea wagonjwa 600 lililowekwa na uongozi wa hospitali hiyo wakati kitengo hicho cha saratani kikianzishwa hospitalini hapo Desemba, 2016.
Hayo yalielezwa na Mkurugenzi Mtendaji wa Hospitali ya Rufaa ya Kanda ya KCMC, Dk Gileard Masenga, wakati wa maadhimisho ya siku ya saratani duniani, yaliyofanyika mwishoni mwa wiki, ambayo yalitanguliwa na matembezi ya hisani kwa ajili ya kuchangia ujenzi wa wodi na hosteli za wagonjwa wa saratani hospitalini hapo.
“Kabla ya kuanza kwa kitengo cha saratani, mwaka wa 2016 tulipokea wagonjwa 433 na ndipo tukaona umuhimu wa kuanzisha kitengo hiki”, alisema. Alisema kati ya wagonjwa hao 3,450, wagonjwa 746 walikuwa ni wapya na kwamba idadi hiyo imekuwa ikiongezeka mara kwa mara.
Dk Masenga alisema, kuwa hospitali hiyo inatarajia kuanza ujenzi wa wodi na hosteli za wagonjwa wa saratani ili kukabiliana na changamoto inayowakabili wagonjwa wanaopata tiba ya ugonjwa huo hospitalini hapo.
“Ujenzi huu ni awamu ya pili baada ya mpango wa kuboresha kitengo cha saratani hopsitalini hapa, ambapo katika awamu ya kwanzan ilihusisha ujenzi wa majengo ya utawala na maeneo ya kuwahudumia wagonjwa”, alisema.
Alisema, ili kutekeleza azma hiyo, hospitali hiyo inatarajia kufanya harambee kwa ajili ya kupata fedha za ujenzi wa wodi na hosteli hizo ambao unatarajia kugharimu zaidi ya shilingi bilioni mbili.
Kwa upande wake Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro, Anna Mghwira alitoa changamoto kwa watafiti hospitalini hapo kufanya utafiti unaohusiana na ugonjwa huo. “Tafiti zenu na matokeo yake utasaidia katika kupambana na ugonjwa huu hatari unaopoteza maisha ya watu wengi,” alisema.
Awali mkuu wa kitengo cha saratani hospitalini hapo, Dk Furaha Serventi, alisema kuwa moja wapo ya changamoto kubwa katika kukabiliana na ugonjwa huo ni elimu duni miongoni mwa wananchi wengi na ambayo alisema haina budi itolewe mara kwa mara ili kunusuru maisha ya watu.
No comments:
Post a Comment