Kiongozi huyo alisema matumizi ya pasipoti mpya za kielektroniki, yataondoa matumizi ya pasipoti za kawaida zinazotumika sasa.
Rais Magufuli alisema pasipoti za kisasa zitakazotolewa zinakidhi viwango vya kimataifa kwa kuwa zina alama nyingi za kiusalama, na siyo rahisi kuzighushi licha ya gharama yake kutokuwa kubwa.
"Pasipoti hii tunayoizundua leo ni ya kipekee sana, ni ya kielektroniki, ina alama nyingi za usalama."
Uzinduzi wa mfumo huo ulifanyika katika ofisi kuu ya uhamiaji jijini Dar es salaam Jumatano.
Kamishna Jenerali wa Uhamiaji Dkt. Anna Makakala amesema mfumo huo ni muunganiko wa mifumo mbalimbali ambayo imesanifiwa kufanya kazi kwa pamoja, kutoa taarifa kwa watumiaji na wadau wa huduma za kiuhamiaji.
Dkt Makakala amesema kwamba kupitia mfumo huo idara ya uhamiaji inatarajia kutoa pasipoti za kielektronikia (e-Passport), viza za kielektronikia (e-Visa), vibali vya ukaazi vya kielektronikia (e-Permit) na udhibiti wa mipaka wa kielektronikia (e-Border Management) kwa awamu nne hadi ifikapo mwisho wa mwaka huu 2018, pamoja na kutoa pasipoti ya kielektronikia ya Afrika Mashariki ya Tanzania.
Kabla ya kuzindua mfumo wa uhamiaji mtandao Rais Magufuli alikagua teknolojia iliyotumika katika mfumo huo ikiwa ni pamoja na kuchukuliwa alama za vidole na baadaye kupatiwa pasipoti mpya ya kielekektroniki (e-Passport) ambayo pia ilianza kutolewa Jumatano.
Rais wa Zanzibar Ali Mohammed Shein pia alipokezwa pasipoti hiyo mpya.
Dkt Magufuli aliishukuru idara hiyo kwa kuhakikisha mfumo huo wa kutoa pasipoti mpya ya kielektronikia ulifanikishwa kwa gharama ya Shilingi Bilioni 127.2 ikilinganishwa na makadirio yaliyowekwa awali ya Shilingi Bilioni 400.
"Hapa tumeokoa fedha nyingi za Watanzania, kuna watu walikuwa wamejiandaa kutupiga na kuchukua hizo Shilingi Bilioni 400, lakini tukatumia vyombo vyetu mbalimbali, tukafanya uchunguzi na tumefanikiwa kutekeleza mradi huu kwa gharama nafuu" alisema Dkt Magufuli.
Rais aliahidi kutoa Shilingi Bilioni 10 kwa ajili ya kujenga ofisi ya makao makuu ya idara hiyo mjini Dodoma.
"Kamishna Jenerali Dkt. Anna Makakala na timu yako mnafanya kazi nzuri, ndio maana nimewanunulia nyumba 103 kwa ajili ya wafanyakazi na leo nitawapa fedha nyingine Shilingi Bilioni 10 mkajenge ofisi nzuri ya makao makuu.
„Nyinyi endeleeni kuchapa kazi, endeleeni kukamata wahamiaji haramu na endeleeni kukusanya mapato vizuri," amesema Rais Magufuli.
No comments:
Post a Comment