SERIKALI imewasilisha bungeni Muswada wa Sheria ya Marekebisho ya Sheria Mbalimbali Namba 5 wa Mwaka 2017 ambao pamoja na marekebisho mengine, umelenga kufanya marekebisho ya Sura Namba 113 ya Sheria ya Ardhi. Sehemu hiyo ya sheria, inaweka masharti kuhusu kutumia ardhi kupata mikopo (mortgage).
Hata hivyo, sheria hiyo ya ardhi haikuainisha masharti kuhusu matumizi ya mkopo unaopatikana kwa kuweka rehani hati ya kumiliki ardhi. Hayo yalisemwa na Mwanasheria Mkuu wa Serikali, George Masaju wakati akiwasilisha muswada huo bungeni jana katika mkutano wa 10 katika kikao cha kwanza. Masaju alisema kutokana na kukosekana kwa masharti hayo, baadhi ya wamiliki wa ardhi wakiwemo wawekezaji, wamekuwa hawatumii mikopo hiyo kuendeleza ardhi husika.
Alisema wamiliki wengine walikuwa kitumia mikopo hiyo, kuweka dhamana ya ardhi ya nchi nje ya nchi badala ya kufanya uwekezaji huo hapa nchini na hivyo, kusababisha ardhi waliyopewa kutoendelezwa na kutelekezwa. Alisema Muswada huo unapendekeza kuongeza vifungu vipya kuhusu masharti ya mkopo unaotokana na kuweka dhamana ardhi pamoja na masharti kuhusu matumuzi ya mkopo huo.
“Mtu anaweza kutumia ardhi kama dhamana ya kupata mikopo kutoka benki au taasisi ya fedha ya ndani au nje ya nchi kwa ajili ya kuendeleza ardhi husika au kwa ajili ya uwekezaji mwingine, iwapo ardhi husika itakuwa imeendelezwa, mkopo huo utapaswa kutumika kwa ajili ya kuendeleza zaidi ardhi hiyo, uwekezaji au kwa ajili ya matumizi mengine,” alisema. Muswada huo unaonesha kwamba, kama ardhi iliyowekwa rehani itakuwa haijendelezwa au imeendelezwa kidogo, mkopo huo utapaswa kutumika kwa ajili ya kuendeleza ardhi yote au sehemu ya ardhi husika.
Aidha unaonesha kwamba, mmiliki wa ardhi (mkopeshwaji) amepewa wajibu wa kuwasilisha kwa Kamishna wa Ardhi taarifa kuhusu namna mkopo husika ulivyowekezwa katika kuendeleza ardhi iliyowekwa rehani. Taarifa hiyo itawasilishwa ndani ya miezi sita tangu mikopo husika kutolewa. Pia unaeleza kwamba mkopo uliotolewa na benki au taasisi ya fedha ya ndani au nje ya nchi kutokana na ardhi kuwekewa rehani, utatumika kwa ajili ya uwekezaji hapa nchini.
Aidha benki au taasisi ya fedha ya ndani au nje inayotoa mkopo unaohusisha dhamana ya ardhi itapaswa kuwasilisha kwa Kimishina wa Fedha tamko kwamba mkopo husika unawekezwa nchini. Sheria nyingine iliyowasilishwa ili kufanyiwa marekebisho ni sheria kuhusu kustaafu kwa maprofesa wa vyuo vikuu vya umma na madaktari bingwa wa binadamu wa hospitali.
“Umri wa kustaafu maprofesa na wahadhiri waandamizi wa vyuo vikuu vya umma pamoja na madaktari bingwa wa binadamu wa hospitali kwa wanaostafu kwa hiari uwe 60, na miaka 65 wanaostaafu kwa lazima,” alisema Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Masaju wakati akiwasilisha muswada huo.Alisema, marekebisho hayo yanatokana na uzoefu uliopo kwamba, maprofesa na wahadhiri waandamizi na madaktari bingwa wa binadamu wa hospitali za umma, wamekuwa wakijihitajika kuendelea kutoa huduma, utalaamu na uzoefu wao, licha ya kufikisha umri wa kustaafu na hivyo kulazimika kuajiriwa na serikali kwa mikataba, hatua hiyo imekuwa ikiongeza gharama kwa serikali.
Alisema muswada huo unapendekeza kwamba marekebisho ya sheria ya utumishi wa umma sura ya 298, ni kwamba umri wa kustaafu kwa hiari kwa watumishi wengine utakuwa miaka 55 na kwa lazima utakuwa miaka 60 tofauti na umri wa maprofesa.
Mwanasheria Mkuu Masaju alisema, marekebisho hayo yataiwezesha serikali kuendelea kupata huduma, utalaamu na uzoefu wa watumishi hao na pia kupunguza gharama ambazo serikali imekuwa ikiingia kwa kuwaajiri wa kimataba mara wanapostaafu. Muswada huo pia umegusa Sheria ya Bajeti Sura ya 239 inayolenga kubadilisha Mpango na Mwongozo wa Bajeti ya Serikali uliokuwa ukiwalishwa bungeni katika Mkutano wa Bunge mwezi Febaruri kila mwaka au wiki ya kwanza baada ya Bunge kuitishwa iwapo hakuna Mkutano wa Bunge mwezi huo.
No comments:
Post a Comment