Monday, 12 February 2018

Pemba: Mwanaume mmoja atiwa mbaroni kwa kumlawiti mtoto wa kiume mwenye umri wa miaka minne

Image may contain: one or more people
Na Masanja Mabula -Pemba
BAKAR Khamis (25) mkaazi wa Mitondooni Wilaya ya Wete, anadaiwa kumnajisi (kumlawiti) mtoto wa kiume mwenye umri wa miaka minne huko Shehia ya Piki Wilaya hiyo.


Akizungumza na mwandishi wa habari hizi baba mzazi wa mtoto huyo alisema mtuhumiwa alimchukuwa mwanawe hadi Bahanasa na kuingia kwenye gari ya abiri na kumpeleka bonde la Hindi na kumfanyia ulawiti.

Alisema mtuhumiwa ni mgeni katika shehia hiyo, alikwenda kwa kutembea, ingawa alichokifanya ni kumchukua mtoto wake na kwenda kufanyia kitendo cha ulawiti, jambo ambalo linamtia huzuni kila anapofikiria.

“Huyo mtuhumiwa ni mgeni hapa kijijini kwetu, alipoona tu washamzoea watoto ndipo alipoamua kumchukua mwanangu kwenda kumlawiti na huko kwao tumesikia kaondoshwa kwa kuwafanyia watoto kitendo hicho”, alisema baba huyo.

Kwa upande wake mama wa mtoto, alisema aliondoka na kwenda mazikoni, ambapo mara baada ya kufika alipigiwa simu na kuambiwa kuwa mwanae amemfuata na ndipo alipofanya haraka ya kurudi, ingawa alipofika hakumkuta.

“Alimpelea katika bonde la Tangoni – Hindi na wakati anamlawiti wakatokea watoto wanaochuma mabungo na mtuhumiwa akakimbia, ndipo walipomuuliza anapoishi na kusema na wakamleta nyumbani”, alisema mama huyo.

Alieleza mara baada ya kufika mtoto wao walimuhoji na kusema kuwa kaka Bakar, alimchukua na kwenda kumfanyia kitendo cha ulawiti na kisha kumpa maandazi, ambapo aliporudi alikuwa nayo kwenye mfuko.

“Walikuja wazazi wa upande wa mtuhumiwa tufanye suluhu ili tusiifikishe kesi Polisi, lakini kwa kitendo alichofanyiwa mwanangu siwezi kusamehe, kwani huu ni ukatili”, alisema mama huyo.

“Huyu mtoto ana kawaidi ya kucheza na mwanangu, sasa alikuja mwanangu na kilio na kuniambia kaka ananikimbia, nikatoka nje nikamwita lakini na mtuhumiwa ikawa anamwita, sasa ikawa kama tunavutiana, ingawa sikuwa na wasiwasi nae nikaona labda anamfuata tu kwa vile washamzoea”, alisema jirani wa mtoto huyo.

Nae, kijana mmoja anaeishi mtaa huo, alisema alimshuhudia mtuhumiwa akiingia kwenye gari na mtoto huyo maeneo ya Bahanasa na kuteremka Mzambarauni majira ya saa 3:00, ingawa hakujua alikompeleka kutokana na yeye alikuwa anaenda Wete.

“Mimi sikufanya wasiwasi maana nilijua ni mdogo wake wa maduguni, kwa hiyo niliporudi ndio nikapata taarifa hiyo na ndipo nilipokumbuka wakati nilipomuona anapanda nae gari”, alisema kaka huyo.

Mratibu wa shehia ya Piki, Bikombo Shazil Makame, alisema tukio hilo limetokea katika shehia yake na tayari wameshalifikisha kituo cha Polisi Wete, ambapo aliwataka wazazi kuwa mstari wa mbele kwenda kutoa ushahidi mahakamani, ili kesi iweze kupata hatia.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kaskazini Pemba, Haji Khamis Haji, alisema tukio hilo lilitokea Januari 2 mwaka huu saa 6:00 mchana huko Piki, mtuhumiwa huyo alimnajisi mtoto wa kiume mwenye miaka minne shehia ya Piki Wilaya ya Wete.

Kamanda huyo, alisema mtuhumiwa huyo ameshakamatwa na Jeshi hilo linaendelea na upelelezi, ambapo watampeleka mahakamni mara baada ya uchunguzi kukamilika kujibu tuhuma zinazomkabili.

Matukio ya udhalilishaji kwa watoto ikiwemo ulawiti yamekuwa yakiongezeka kila siku, kutokana na sababu mbali mbali, ikiwemo wanajamii kukataa kutoa ushahidi pamoja na kesi kukaa muda mrefu mahakamani bila ya kupatiwa hukumu.

Chanzo: Mpekuzi

No comments:

 

ADVERTISE WITH US

AFRICAN FASHION

PLACE YOUR ADS HERE!