Monday, 19 February 2018

Marufuku kutangaza dawa za kuongeza makalio

MAMLAKA ya Chakula na Dawa Tanzania (TFDA) kwa kushirikiana na Jeshi la Polisi nchini, imepiga marufuku matangazo ya biashara za vipodozi na dawa za kuongeza maumbile kwenye mitandao ya kijamii kama vile Instagram, Facebook, Twitter na blogs.


Akizungumza na waandishi wa habari jana Dar es Salaam, Kaimu Mkurugenzi wa TFDA, Agnes Kijo alisema matangazo hayo yanatakiwa kukoma mara moja na wahusika wanastahili kufika katika mamlaka hizo kuomba kibali.
Alisema kumekuwepo na wimbi la watu mbalimbali wanaotangaza vipodozi kwa lengo la kujichubua na dawa za kuongeza maumbile kwenye mitandao hiyo ya kijamii wakifanya kinyume na Sheria ya Mamlaka ya Chakula, Dawa na Vipodozi sura ya 219.
Alisisitiza kuwa matangazo ya vipodozi na dawa hizo yamekuwa na madai mbalimbali kama vile kuongeza makalio, kuongeza nyonga, sehemu za siri za mwanaume, kurudisha bikira kwa wanawake na kuondoa mabaka sugu.
Alisema bidhaa hizo zipo kwenye hali mbalimbali mathalani vidonge, jeli, losheni, mafuta, krimu na dawa za kunywa. Kijo alisema baadhi ya watu wamekuwa wakipotosha umma kuwa bidhaa zao zimethibitishwa na TFDA kitu ambacho si kweli.
Kwa upande wake, Msaidizi Mkuu kutoka Kitengo cha Uhalifu wa Makosa ya Kimtandao, Joshua Mwangasa alisema uwepo wa matangazo katika mitandao ya kijamii ni kinyume na sheria ya mtandao na kwamba inaleta upotoshaji kwa jamii.
Mwangasa ambaye pia ni Mrakibu Msaidizi wa Polisi alisema, “watu ambao wanatumia vibaya mitandao ya kijamii kwa kuweka matangazo ya dawa na vipodozi vya kuongeza makalio na kukuza maumbile waache mara moja na wayafute matangazo hayo kwenye kurasa zao za mitandao ya kijamii.”
Alisema jeshi hili linaendelea na uchunguzi kuwabaini wale wote wanaofanya hivyo na kisha watachukuliwa hatua za kisheria.

No comments:

 

ADVERTISE WITH US

AFRICAN FASHION

PLACE YOUR ADS HERE!