MAMLAKA ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) inatarajia kufanya majaribio ya kusajili laini za simu kwa kutumia alama za vidole, ambayo itafanywa kwa mfano katika mikoa minne nchini kwa mtu asiye na laini.
Mfumo huo mpya utatumia njia ya kielektroniki, kusajili laini za simu za mkononi, ukitumia taarifa kutoka Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (NIDA). Akizungumzia mfumo huo jijini Dar es Salaam jana, Naibu Mkurugenzi anayeshughulikia masuala ya watumiaji wa huduma na bidhaa kutoka TCRA, Thadayo Ringo aliitaja mikoa itakayofanyiwa majaribio hayo kuwa ni Pwani, Tanga, Singida na Iringa.
Alisema mfumo huo unatarajiwa kufanyika kwa mwezi mmoja, kuanzia Februari 5 hadi Machi 5, mwaka huu na utawahusu wasiokuwa na laini za simu na katika usajili huo hawataulizwa jina wala kupigwa picha.
Ringo alisema katika mfumo huo, tayari vimetengwa vituo sita vya mfano kwa ajili ya utekelezaji. Alisema kwamba mikoa hiyo, imechaguliwa kutokana na NIDA kumaliza utaratibu mzima wa kuandikisha wananchi kupata vitambulisho vya Taifa. Alisema kuanzia mwaka 2009, serikali ilitoa tamko la kusajiliwa kwa laini za simu na mwaka 2010 ilitungwa sheria na kanuni zake kutoka 2011 ambapo zilihitaji kila mmoja kusajili laini.
Alisema tangu mwaka 2010, kumekuwepo na changamoto mbalimbali kwa watoa huduma, ambazo wamekuwa wakikumbana nazo ambazo zinahusu utolewaji wa taarifa zisizo sahihi katika usajili. Ringo alisema kutokana na changamoto hizo, watoa huduma za mawasiliano kwa kushirikiana na TCRA, wamebuni utaratibu ambao utaweza kubaini kwamba anayesajiliwa ndiye mhusika halisi, hivyo kuweza kumtambua mtu kwa uhakika.
Alisema watatumia njia ya elektroniki kusajili laini za simu za mkononi na kwamba Mamlaka hiyo, itatumia taarifa za NIDA. Vitu viwili vitahitajika wakati wa usajili huo, navyo ni namba ya utambulisho ya Kitambulisho cha Taifa inayojulikana kama NIN na alama za vidole ili kuthibitisha mhusika halisi.
No comments:
Post a Comment