Wednesday 24 January 2018

Watoto 15 wenye matatizo ya moyo wafanyiwa upasuaji wa bila kufungua kifua


Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) kwa kushirikiana na Taasisi ya Okoa Moyo wa Mtoto (Save a Child’s Heart-SACH) ya nchini Israel na Kituo cha Moyo cha Berlin (Berlin Heart Center) cha nchini Ujerumani wamefanya upasuaji wa bila kufungua kifua (Catheterization) kwa watoto 15 wenye matatizo ya Moyo.


Upasuaji huo unaotumia mtambo wa Cathlab umefanyika katika kambi maalum ya matibabu iliyoanza tarehe 20/01/2018 inatarajia kumalizika kesho tarehe 25/01/2018. Matibabu yaliyofanyika ni ya kuzibua matundu kwenye moyo na kutanua mishipa ya moyo kwa watoto wenye umri wa kuanzia mwezi mmoja hadi miaka 18.
Kambi hii ilienda sambamba na uchunguzi wa moyo kwa watoto 32 ambapo watoto 20 watafanyiwa matibabu katika kambi hii na wengine 12 waliobaki watatibiwa na madaktari wetu wa ndani kuanzia wiki ijayo.
Tumepanga kufanya matibabu kwa watoto 20 tunaamini hadi kambi itakapomalizika watoto wote hawa watakuwa wamepata matibabu. Watoto 15 waliopata matibabu wengine wameruhusiwa na waliobaki hali zao zinaendelea vizuri na wataruhusiwa pindi afya zao zitakapoimarika.
Aidha kambi hii imeenda sambamba na utoaji wa elimu ya upasuaji wa moyo wa bila kufungua kifua kwa watoto na jinsi ya kuwahudumia watoto waliofanyiwa upasuaji huo. Mafunzo haya yamewajengea uwezo wafanyakazi wetu wakiwemo madaktari, wauguzi, wataalam wa kutoa dawa za usingizi na wataalam wengine wa chumba cha upasuaji. Mafunzo hayo yatawasaidia kuongeza ufanisi katika kazi zao.
Tangu mwaka 2015 Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete ilianza kushirikiana na Taasisi ya Okoa Moyo wa Mtoto (Save a Child’s Heart- SACH) na Berlin Heart Center hadi sasa jumla ya watoto 46 wamefanyiwa upasuaji wa moyo nchini Israel.
Gharama za matibabu ya watoto hawa zinagharamiwa na Taasisi hizi za Israel na Ujerumani kwa makubaliano ya kirafiki na Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete. Kwa upande wa watoto waliotibiwa katika kambi maalum za matibabu zilizofanyika hapa nchini ni 79 mchanganuo wake ni kama ifuatavyo: Mwaka 2015 walitibiwa watoto 11, mwaka 2016 watoto 48, mwaka 2017 watoto 20.
Tunawashukuru sana wenzetu hawa wa SACH na Berlin Heart Center kwa kuona umuhimu wa kutoa huduma ya matibabu bila malipo kwa watoto wenye matatizo ya moyo. Watoto waliotibiwa wamepona na wale ambao ni wanafunzi wanaendelea na masomo yao.
Kwa upande wa wazazi na walezi tunawaomba wasisahau kupima afya za watoto wao pale watakapoona kuna hali ya tofauti katika ukuaji wa mtoto kwani magonjwa mengi ya moyo yanaanzia utotoni.
Mtoto akianza kuuguwa magonjwa ya moyo wazazi wengi wanadhani ni matatizo ya kifua baada ya kumfikisha Hospitali na kufanyiwa vipimo ndipo inagundulika mtoto anasumbuliwa na magonjwa ya moyo.
Kwa wamama wajawazito wafanye uchunguzi (Fetal Echocardiography) wa kuangalia kama mtoto aliyeko tumboni anamatatizo ya moyo au la. Kupitia kipimo hiki mtoto akigundulika kuwa na tatizo la moyo ataweza kupatiwa matibabu kwa wakati na hivyo kuwa na afya njema kama watoto wengine.
Kama mnavyofahamu matibabu ya moyo ni ya gharama hivyo basi tunaendelea kuwahimiza wananchi kujiunga na Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya ambao utawasaidia kulipa gharama za matibabu pindi watakapouguwa na kuhitaji kupata matibabu. Kwa wale wasiojiweza kabisa kambi kama hizi zinatumika na Taasisi kuwahudumia bila malipo yoyote yale.

No comments:

 

ADVERTISE WITH US

AFRICAN FASHION

PLACE YOUR ADS HERE!