Saturday, 13 January 2018

Wakurugenzi 2 matatani ubadhirifu wa mil.495/-


BARAZA la Madiwani la Halmashauri ya Wilaya ya Rombo, limeagiza watumishi saba, kati ya 14 waliokuwa watumishi wa halmashauri hiyo, wakiwemo wakurugenzi watendaji wawili, kurejea wilayani hapa, kutoa ufafanuzi wa matumizi holela ya zaidi ya Sh milioni 495.5.


Ufafanuzi wa fedha hizo ni majibu ya hoja za Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali za Mitaa (LAAC), iliyotaka ufafanuzi wa matumizi ya fedha hizo kwa mwaka 2015/2016. Akizungumzia suala hilo, Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri hiyo, Magreth John alisema tayari watumishi hao, wameandikiwa barua ya kuwapa siku 14 kutoa majibu, vinginevyo watachukuliwa hatua ikiwemo kufikishwa mahakamani.
“Katika fedha hizi, kiasi cha shilingi milioni 243.5 kilitumika kinyume na taratibu huku kiasicha shilingi milioni 251 kilitumika bila viambatanisho... tayari tumewapa barua wahusika ili kutoa ufafanuzi tangu Januari 2, mwaka huu, wapo walioanza kutoa majibu,” alisema.
Alisema miongoni mwa watumishi ambao wanahitajika, saba wapo katika halmashauri nyingine nchini na tayari barua imeandikwa kutoka ofisi ya Katibu Tawala wa Mkoa (RAS) Mkoa Kilimanjaro, kwenda katika mamlaka yao ya uteuzi ili warejee wilayani humo kujibu hoja zinazowahusu. Mkurugenzi alisema watumishi wengine watano wapo wilayani Rombo, mmoja amestaafu na mwingine mmoja aliondolewa kazini wakati wa uhakiki wa vyeti feki wilayani humo.
Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya hiyo, Evarist Silayo alikiri baraza hilo kuazimia kurejeshwa kwa watumishi hao, kwani kinyume na hapo watafikishwa mahakamani. Alisema jambo hilo walijadili katika Kamati ya Fedha, Uongozi na Mipango Desemba 28, mwaka jana na kesho yake Baraza la Madiwani lilitoa azimio la kurejeshwa kwa watumishi hao, kwani hoja inayowahusu inaharibu sifa ya halmashauri hiyo.

No comments:

 

ADVERTISE WITH US

AFRICAN FASHION

PLACE YOUR ADS HERE!