SERIKALI imezuia utoaji wa hati za kusafi ria za makundi. Hatua hiyo imechukuliwa baada ya kuwepo tabia ya vijana kuchukuliwa nchini na kupelekwa nje ambako huwekwa rehani na kufanyiwa vitendo vya ukatili.
Akizungumza na watendaji wa Idara ya Uhamiaji jana Dar es Salaam, Waziri wa Mambo ya Ndani, Dk Mwigulu Nchemba alisema kuwa wamezuia utoaji wa hati hizo kuanzia jana hadi hapo watakapotangaza utaratibu mwingine.
Alisema makundi ya vijana yamekuwa yakitolewa nchini na kupelekwa nje ya nchi kwa ahadi ya kupatiwa ajira lakini mamboyanakuwa tofauti pindi wanapofika katika nchi hizo ambapo wanawekwa rehani kwa dawa za kulevya, kupokonywa hati za kusafiria na kufanyiwa vitendo vya ukatili. “Tutatangaza utaratibu rasmi na ulio mzuri kuhusu utoaji wa hati za kusafiria za makundi ikiwemo wale watu ambao wanadanganya vijana kuwa wanakwenda kuwatafutia ajira nchi hizo tutahakiki kwa kuwasiliana na serikali husika kama kweli wanauhitaji wa aina hiyo ili kujiridhisha,” alisema Dk Mwigulu.
Hata hivyo, aliagiza watu waliowaweka rehani vijana wakamatwe na kutiwa mbaroni kwa makosa ya kuwaingiza katika matendo ya ukatili na kuleta majonzi katika familia zao. Aidha, amezitaka kampuni sita zinazojishughulisha na kuwachukua vijana waripoti kwa Kamishna wa Vibali na Mipaka wa Uhamiaji kwa ajili ya kutoa maelezo vibali walivyoviomba wanavitumiaje kwa kuwa yapo madai wanakiuka vibali kwa kuwafanyisha vitu tofauti.
Alizitaja kampuni hizo kuwa ni Neel Ltd au Dhakhan Night Club & Restaurant iliyopo Msasani Kimweri; Dhoom Entertainment Centre Ltd iliyopo Kinondoni Makaburini; Dhamaal Management Ltd iliyopo Shoppers; Talk of the Town iliyopo Msasani kwa Mwalimu; MSM International Ltd na Keypee Arts Ltd iliyopo Kinondoni barabara ya kwenda Chuo Kikuu Huria, ambazo zimetakiwa kuripoti kwa kamishna kujieleza.
“Serikali imesaini mikataba ya kimataifa ya kutosafirisha binadamu hivyo wale wanaofanya biashara hiyo wakamatwe,” alisema. Katika hatua nyingine, Serikali imesitisha shughuli za Wakala Binafsi wa Huduma za Ajira nchini baada ya kubainika kukiukwa kwa sheria ikiwemo wafanyakazi wanaokwenda kufanya kazi mataifa ya nje kufanyiwa vitendo vya kibaguzi na unyanyasaji katika ajira, mishahara na stahiki mbalimbali.
Imetangaza pia kuzifutia usajili kampuni tatu za Uwakala Binafsi wa Huduma za Ajira baada ya kubainika kukiuka taratibu za usajili. Katika hatua nyingine imetangaza kufanya ukaguzi wa kina ndani ya siku 14 kuanzia jana kwa kampuni zote zinazotoa huduma hiyo hapa nchini ili kujiridhisha kama kampuni hizo zinazingatia sheria na kanuni na pia hazifanyi ujanja ikiwemo kukwepa kodi za serikali.
Hayo yalisemwa jana na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu Jenister Mhagama alipozungumza na vyombo mbalimbali vya habari huku akieleza kuwa msingi wa hatua hizo zilizochukuliwa na serikali unatokana na kupokelewa kwa malalamiko mengi. Alisema kutokana na malalamiko hayo, ofisi yake ilifanya uchunguzi kuhusu suala hilo na kubaini kuwa kumekuwepo na ukiukwaji wa matakwa ya Sheria ya Huduma za Ajira Namba 9 ya Mwaka 1999 na Kanuni zake za Mwaka 2014.
Akizungumzia hatua zilizochukuliwa kutokana na kubainika kwa ukiukwaji huo mkubwa wa sheria, Waziri Mhagama alisema Serikali imeamua kuzifutia usajili kampuni tatu za Sasy Solution Company Limited, Bravo Job Center Agency na Competitative Manpower International. “Kwa tamko hili, kampuni hizo haziruhusiwi tena kujihusisha na shughuli za Uwakala Binafsi wa Ajira nchini,” alisema. Alisema ofisi yake pia imesitisha mara moja shughuli za Mawakala 40 Binafsi wa Huduma za Ajira wanaohusika na kuwatafutia kazi wafanyakazi nje ya nchi hadi hapo Serikali itakapoleta mfumo wa kusimamia jambo hilo na kutoa taarifa kwa umma
No comments:
Post a Comment