WATU wawili wanaosadikiwa kuwa majangili sugu wameuawa kwa kupingwa risasi za moto baada ya majibishano makali kati yao wakiwa saba, askari polisi na askari wa Hifadhi ya Taifa ya Katavi wilayani Mpanda.
Katika majibishano hayo ya risasi yaliyodumu kwa zaidi ya saa mbili watu watano wanaosadikiwa kuwa majangili sugu walizidiwa nguvu na kujisalimisha mikononi mwa askari polisi na askari wa Hifadhi ya Taifa ya Katavi.
Kamanda wa Polisi Katavi, Damas Nyanda alisema kuwa katika mapambano hayo jeshi la polisi na askari wa Hifadhi ya Taifa ya Katavi walifanikiwa kukamata silaha nzito tatu aina ya SMG pamoja na magazine tano na risasi 16.
Aliongeza kuwa pia walifanikiwa kukamata nyara za Serikali zenye thamani ya Sh milioni 37.9. Kamanda Nyanda alisema nyara hizo ambazo ni vipande vinne vya meno ya tembo kwa pamoja vikiwa na uzito wa kilo 6.6 vyenye thamani ya Sh milioni 35 na nyama ya pofu yenye uzito wa kilo 20 ikiwa na thamani ya Sh milioni 3.9 kwa pamoja viikuwa vimefichwa kwenye mifuko ya sandarusi.
Kamanda Nyanda alisema kuwa tukio hilo lilitokea usiku wa manane wa kuamkia jana katika kijiji cha Kapalamsenga mwambao mwa Ziwa Tanganyika wilayani Tanganyika. “Jeshi la Polisi kwa kushirikiana na askari wa Hifadhi ya Taifa ya Katavi tulifanya msako kwa pamoja kwa wili tatu tukiwasaka ‘majangiri’ hawa sugu usiku na mchana, ndipo tulipobaini maficho yao nao wakajihami kwa kuanza kuturushia risasi na ndipo mabishano makali ya risasi yalipotokea baina yao na sisi,” alieleza Kamanda Nyanda.
Alieleza kuwa watuhumiwa hao watano wanaendelea kuhojiwa ili kuweza kubaini mtandao wao wa ujangiri ambapo watafikishwa mahakamani mara tu baada ya uchunguzi wa awali wa kesi yao kukamilika. Kwa upande wake, Mku wa Hifadhi ya Taifa ya Katavi, Izumbe Msindai alisema ushirikiano wa Jeshi la Polisi na askari wa Hifadhi hiyo umefanikisha kukamatwa kwa watuhuimiwa hao.
No comments:
Post a Comment