WANANCHI wengi hawajui haki zao katika vyombo vya usafiri hali ambayo husababisha baadhi kupata manyanyaso bila sababu za msingi. Utafiti uliofanywa na Baraza la Ushauri la Sumatra (SUMATRA CCC) mwaka 2012 ulionesha asilimia 54 ya watumiaji Tanzania hawajui haki na wajibu wao.
Hata hivyo kujua na kutenda ni vitu viwili tofauti. Mazingira kama haya husababisha watoa huduma wasio waaminifu kutumia mazingira hayo kuwalalia watumiaji hao na kuwaacha wanalalamika.
Hivyo ni vema kila mmoja kufahamu sheria, taratibu, kanuni na kuwa makini kuzifuata ili kuepuka migogoro isiyokuwa ya msingi. Wananchi wengi hawajui haki zao katika vyombo vya usafiri, lakini ni vema wakazijua sheria, kanuni na taratibu wanazopaswa kuzizingatia kila wanapopata huduma katika vyombo vya usafiri, ziweze kuwasaidia.
Kwa kutokujua sheria, imekuwa ni chanzo kikubwa kwa wengi kukosa fursa walizotakiwa kuzipata. Kwa mfano, kulipa nauli halali, kuchagua chombo cha usafiri ukitakacho, kulipwa fidia, kukata tiketi mapema, kurudishiwa sehemu ya nauli basi linapoharibika kabla ya kufika mwisho wa safari na kulinda usalama wao wawapo safarini hasa majira ya mwisho wa mwaka na mwanzo wa mwaka.
Katika kufuatilia ni namna gani abiria wa vyombo vya usafiri hususani magari, treni na vivuko, ukweli unathibitika kuwa wengi hawajui. Mathalani, kurudishiwa nauli pale gari linaposhindwa kuendelea na safari au linapochelewa kuanza safari iliyopangwa, baadhi ya abiria wanasema wamekuwa wakisikia kuwa kuna sheria kama hiyo ya kurudishiwa nauli.
Mmoja wa abiria katika kituo kikuu cha mabasi Ubungo, Datuu Sari anasema hajui kama kuna sheria kama hiyo ya kumtaka alipwe nauli yake pale gari linapochelewa ama kushindwa kuondoka kwa siku hiyo.
Anasema anachokijua ni kwamba, kama gari limeshindwa kuondoka kwa siku husika, hupewa siku inayofuata aondoke na gari lingine la kampuni husika ama hilo walilokuwa waondoke nalo baada ya kutengenezwa Abiria huyu hajui kuhusu Kanuni namba 21 (2) ya sheria za Sumatra za mwaka 2008 inayotoa haki kwa abiria kurudishiwa nauli pale chombo cha usafiri kinapochelewa kuanza safari baada ya kupita saa moja ya muda uliopangwa kwenye ratiba ya tiketi kupita au saa mbili zikipita tangu basi liharibike.
Sari anawakilisha kundi la watu ambao hawafahamu sheria mbalimbali zinazowasaidia kupata haki katika vyombo vya usafiri. Kwa mfano, wakati ipo kanuni namba 23 (1) (2) ya Sumatra inayotoa haki kwa abiria kutolipia mzigo usiozidi kilogramu 20 kwa mtu mzima na kilo 10 kwa mtoto anayesafiri, bado abiria wamekuwa wakinyanyaswa na wafanyakazi wa kwenye mabasi wakitakiwa kulipia hata mzigo mdogo.
Kwa kanuni hii, wengi wamepata shida, manyanyaso na hata kudhalilishwa na watoa huduma kuhusu kulipia mizigo ambayo kimsingi na kwa mujibu wa sheria hawakupaswa kuilipia. Ila wale wanaozijua na kuthubutu kuzitumia, hupata haki zao. Abiria kutoka mkoani Mbeya, Lusia Jacob anasema: “Tangu napanda basi hili wamenisumbua sana kwa kuniambia nilipie mzigo wangu ili nisafiri salama.
“Nilimwomba nitamlipa mwisho wa safari yangu na hata tulipofika stendi, aliniambia hawezi kushusha mzigo huo mpaka nimpatie Sh 5,000,” anasema. Lusia anaweka bayana kuwa hafahamu kanuni zinazomlinda abiria za kutolipa mzigo usiozidi kilogramu 20. Anasema jambo hilo halijui kabisa na kushauri elimu itolewe kupitia vyombo vya habari ili kila mmoja aelewe na kuchukua hatua.
Nicholas Kinyayiri ambaye ni Ofisa Elimu Sumatra CCC anasema elimu imekuwa ikitolewa kupitia vyombo vya habari, semina, na shuleni kwa kuwafikia wanafunzi wa shule ya msingi na sekondari. Vile vile kupitia matukio maalumu pamoja na wiki ya nenda kwa usalama, elimu imekuwa ikitolewa.
Kinyahiri anasema ni kweli wapo abiria wasiojua haki zao na wengine wanazijua lakini ni waoga kuzilinda, na kama wangezijua na kuwa jasiri wao wangekuwa wa kwanza kutoa elimu hiyo kwa wahusika wa usafiri wanaoutumia. Katika hili la ulipiaji mizigo, ni nadra kukuta mizani ya kupimia mizigo ya abiria katika vituo vya mabasi ingawa sheria inataka iwepo. Utozaji wa mizigo na vifurushi vya abiria unatajwa kutumiwa na madereva na makondakta kwa ajili ya kupata kipato cha ziada.
Ofisa Elimu huyo wa Sumatra CCC, anasema ujio wa kanuni mpya za leseni za mwaka 2017 umezingatia watoa huduma kupima mizigo inayobebwa katika maeneo ya vituo vya mabasi au ofisi. Kondakta Abdul Rajab na dereva wake Suleiman Suleiman ni miongoni mwa wafanyakazi wa mabasi wanaokiri kutofahamu kama kuna haki na sheria zinazohusu abiria ama mizigo waliyonayo wawapo safarini.
Wanatoa sababu kuwa kanuni hazifundishwi kwenye vyuo vya madereva ingawa wanasema tajiri wao huwafahamishwa wanapokata leseni. Lakini kondakta mwingine Robert John anasema hana haja ya kujua sheria na kanuni hizo kwa kuwa katika eneo hilo ndipo anapojipatia kipato chake cha ziada.
“Hata kama kuna sheria za namna hiyo utekelezaji wake kwangu utakuwa mgumu, kwani kupitia fedha hizo ninazotoza kwenye mizigo ya abiria ndio kipato chetu cha ziada na dereva. Kinatuwezesha kutoa nyumbani kwa matumizi ama kujilisha wenyewe,” anasema.
No comments:
Post a Comment