NCHI zote 54 za Afrika katika Umoja wa Mataifa zimemtaka Rais wa Marekani, Donald Trump kuomba radhi baada ya kuripotiwa kutumia maneno machafu, alipokuwa akizungumzia wahamiaji kutoka Afrika, Haiti na Salvador.
Baada ya kikao cha dharura cha mabalozi wa nchi za Afrika katika Umoja wa Mataifa, mabalozi hao wamesema wana wasiwasi na mtindo unaozidi kujitokeza kutoka utawala wa Marekani wa kuwadharau Waafrika na bara la Afrika na kulaani vikali matamshi ya kibaguzi na chuki dhidi ya wageni yaliyotolewa na Rais Trump.
Pia Umoja wa Afrika umemshutumu Trump kwa matamshi yake ukisema umeshtushwa na umesikitishwa na umemtaka aombe radhi. Msemaji wa Umoja wa Afrika, Ebba Kalondo alisema matamshi ya Rais wa Marekani si ya kiungwana.
Umoja wa Mataifa pia umelaani matamshi ya kiongozi huyo wa Marekani na kusema ni ya kutia aibu na kibaguzi. Hata hivyo, Rais Donald Trump amekanusha kutumia maneno machafu juu ya nchi kadhaa, ikiwa ni pamoja na za Afrika, akijitetea kwa kusema alikuwa tu akielezea kile watu wengi wanafikiria lakini hawadiriki kusema kuhusu wahamiaji kutoka nchi masikini.
“Lugha inayotumiwa na mimi katika mkutano wa wabunge ilikuwa ngumu, lakini hii haikuwa lugha inayotumiwa na vyombo vya habari,” aliandika kwenye ukurasa wa twita yake. Taarifa ya mmoja wa washirika wake wa karibu ambaye hakutaka kutaja jina lake, alisema Trump hajutii kauli ya kuziita nchi za Afrika na nyinginezo zilizooza, na akikanusha kuwa ni mbaguzi na kuvilaumu vyombo vya habari kwa kupotosha maana ya kauli yake
No comments:
Post a Comment