MAHAKAMA ya Hakimu Mkazi Mwanza inatarajiwa kutoa uamuzi wa dhamana ya washtakiwa wanne wanaokabiliwa na kesi ya kujihusisha na vitendo vinavyoashiria mapenzi ya jinsia moja na makosa ya mtandao keshikutwa Ijumaa, Desemba 15.
Katika kesi hiyo, washtakiwa ni Milembe Suleiman na Janeth Shonza ambaye ni mwanafunzi wa kozi ya Sheria katika Chuo Kikuu cha Mtakatifu Augustine (SAUT) wanaodaiwa kuvishana pete ya uchumba licha ya wote wawili kuwa na jinsia ya kike. Wengine wanaokabiriwa katika kesi hiyo ni Aneth Mkuki anayedaiwa kufanikisha sherehe wanawake hao kuvishana pete na Richard Fabian, anayekabiriwa na kwa kosa la kusambaza video za tukio hilo mitandaoni.
Hakimu Mkazi Mwandamizi Mfawidhi anayesikiliza kesi hiyo, Wilbert Chuma ameahirisha baada ya kusikiliza hoja kuhusu hati ya kiapo iliyowasilishwa na Jamhuri kuzuia dhamana ambapo hati iliyosainiwa na Mkuu wa Upelelezi Mkoa (RCO) wa Mwanza, John Ndibalema, Wakili wa Serikali Emmanuel Luvinga ameiomba Mahakama kuzuia dhamana ya washtakiwa kwa madai kuwa wakiwa nje wanaweza kuingilia upelelezi wa kesi ambao haujakamilika.
Aidha, Wakili Luvinga amedai kitendo walichokifanya washtakiwa hao ni kinyume cha maadili, jambo linaloweza kusababisha wadhuriwe na jamii iliyoangalia video ya wao kuvishana pete kupitia mitandaoni.
Kwa upande wa Mawakili wa utetezi Mashaka Tuguta, Jebra Kambole na Ogastini Kulwa waliwasilisha hati ya kupinga hoja hizo wakieleza kuwa licha ya dhamana kuwa haki ya washtakiwa na shauri linalowakabili kuwa na dhamana, msingi wa hoja za zuio ni hisia tu. Wameeleza kuwa upelelezi na ulinzi wa washtakiwa ni jukumu la upande wa Jamhuri, hivyo hoja hiyo isiwe kigezo cha kuwanyima haki washtakiwa hao.
No comments:
Post a Comment