Saturday 23 December 2017

Walimu wapya 3,000 kuripoti kazini J’tano

SERIKALI imewataka walimu wapya 3,033 wa shule za msingi na sekondari, kuripoti katika vituo vya kazi kuanzia Desemba 27, mwaka huu hadi Januari 7.


Kati ya walimu hao, walimu 266 ni wa sekondari na walimu 2,767 ni shule za msingi. Hayo yamesemwa na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), Selemani Jafo alipokuwa akitoa taarifa ya ajira mpya kwa walimu wa msingi na sekondari.
Alikuwa akitangaza nafasi za ajira kwa walimu 3,033 wa shule hizo, watakaoziba nafasi zilizoachwa wazi na walimu waliondolewa kwenye utumishi wa umma baada ya kubainisha kuwa na vyeti vya kugushi.
Alionya kuwa walimu watakaobainika kuchukua posho ya kujikimu na baadaye kuondoka kwenye vituo vyao vya kazi na ikibainika, watachukuliwa hatua kwa mujibu wa sheria. “ Walimu hawa wanatakiwa kuripoti katika vituo vya kazi kuanzia Desemba 27 mwaka huu hadi Januari 7 mwakani, wakiwa na vyeti vya kidato cha nne na sita, vyeti vya taaluma vya kuhitimu mafunzo ya ualimu kwa ngazi husika na cheti cha kuzaliwa.
Walimu wanaoajiriwa, watatakiwa kuripoti katika ofisi za wakurugenzi wa halmashauri zilipo shule walizopangiwa na kisha watakwenda kuripoti kwenye shule husika...vituo vyao vya kazi ni shule za msingi na sekondari kwa waliopangiwa kufundisha elimu ya msingi au sekondari na si makao makuu ya halmashauri,” alisema.
Jafo aliongeza kuwa, “ kila mwalimu amepangiwa kwenye shule ambayo haina walimu wa somo husika au kuna upungufu mkubwa shuleni.” Alisema waajiriwa wapya, hawatahamishwa kutoka shule moja kwenda shule nyingine, ndani au nje ya halmashauri au mkoa, bila ridhaa ya ofisi ya Rais Tamisemi.
“Nachukuwa fursa hii kuwataka wakurugenzi katika halmashauri ambazo walimu hawa wataripoti, kuwapokea walimu hao kwa kuzingatia taratibu na kanuni za utumishi wa umma na baadaye kutoa taarifa ya kuripoti kwao,” alisema waziri huyo

No comments:

 

ADVERTISE WITH US

AFRICAN FASHION

PLACE YOUR ADS HERE!