Wednesday 20 December 2017

‘Viongozi CCM msiwaogope watendaji wa serikali’

MWENYEKITI wa Chama cha Mapinduzi (CCM), Rais John Magufuli amesema viongozi wa chama, hawapaswi kuwaogopa watendaji wa serikali hususan kwenye kutetea maslahi ya wanyonge.


Alitoa kauli hiyo jana wakati akifungua Mkutano Mkuu wa tisa wa CCM, katika Ukumbi wa Jakaya Kikwete, mjini hapa. “Viongozi wa chama hawapaswi kuwaogopa watendaji wa serikali hususan kwenye kutetea maslahi ya wanyonge kwani serikali inayotawala ni ya CCM na wananchi wako chini yetu,” alisema.
Alisema kazi ya chama kilicho imara ni kusaidia wananchi na chama kina kazi ya kusemea wananchi. Alisema ni wajibu wa viongozi wakitekeleza wajibu wao ipasavyo na kuwa karibu na wananchi. “Nashangaa wananchi kutojua umuhimu wa kununua ndege, kujenga reli wakati huko waliko kuna viongozi wa CCM,” alisema.
Aliwataka viongozi wa serikali wanaoteuliwa na Rais, kutoa ufafanuzi vizuri kwa viongozi wa CCM kwa yale yanayotekelezwa na serikali ili waweze kutambua jinsi ilani inavyotekelezwa. Kuhusu rushwa Rais Magufuli aliwataka wana CCM kuchagua viongozi bila kuangalia maslahi urafiki, dini na kabila.
Alisema wasiwachague viongozi watoa rushwa, kwani rushwa ni adui wa haki. “Kiongozi anapaswa kuwa mfano kwa wanachama na wananchi, hatakiwi kutuhumiwa kwa sifa mbaya kama ujambazi, dawa za kulevya, rushwa,” alisema na kuongeza “Naomba ninukuu maneno ya Mwalimu Julius Nyerere aliyoyasema Juni 1968 kazi ya chama kilicho imara ni kuunganisha wananchi na serikali kwa kuwaondoa na umasikini wao,” alisema Magufuli.
“Kuna msemo maarufu unasema ‘Mke wa Mfalme hapaswi kutuhumiwa kwa kuchepuka’, siyo siri kuwa mageuzi tuliyoyafanya ni makubwa sana na hatuna budi kuyasimamia na viongozi waliochaguliwa ndiyo watakakuwa na majukumu hayo,” alisema.
Mageuzi ndani ya Chama Alisema kunatakiwa kuwa na mageuzi ndani ya Chama, uadilifu na usimamizi wa mali za Chama ili Chama kisitegemee wafadhili wakiwemo matajiri wachache. Alisema chama kina mali na rasilimali nyingi, kama zingetumika kadri inavyotakiwa, kingeweza kujitegemea.
Alisema kuna viwanja zaidi ya 5,000 vinavyomilikiwa na CCM, lakini havitoi mchango unaostahili kutokana na matumizi ya rasilimali zake kutoeleweka. “Tuko mbioni kutumia mfumo wa kielektroniki utakaokuwa ukikusanya mapato na halmashauri kuu imeridhia mfumo huo upitishwe.
“Hadi kufika 2020 kama kutakuwa hakuna hata kiwanda kimoja kilicho chini ya CCM ni aibu,” alisema Pia aliwataka viongozi kutumia njia sahihi za kufikisha mapungufu, wanayoyaona kwenye serikali.
Pia Mwenyekiti huyo aliwataka wanaCCM kuchangua viongozi waadilifu, wachapa kazi na wenye maadili kwa nia ya kuleta maendeleo kwa Taifa. Alisema ili Taifa kuwa na maendeleo mazuri ni lazima kama wanaCCM kuvunja makundi, yaliyoanzishwa kipindi cha uchaguzi na matokeo uchaguzi umekwisha, sasa ni wakati wa kuvunja makundi hayo kwa lengo la kuchapa kazi.
Pia aliwataka wanaCCM kuendelea kuwa wanaCCM wema ili kuleta manufaa na maendeleo ya nchi yetu. Aidha alisema serikali imepanga katika harakati ya kufikia uchumi wa kati na wa viwanda na mpaka sasa viwanda 3,306 tayari vimejengwa.
Pamoja na hayo, alisema jumla ya fedha za kigeni 5,824 zimeongezeka. Ajenda ya mkutano huo ni pamoja na utekelezaji wa Ilani ya CCM, kujenga na kuimarisha Chama. Hadi sasa CCM imetimiza miaka 40.

No comments:

 

ADVERTISE WITH US

AFRICAN FASHION

PLACE YOUR ADS HERE!