Saturday, 30 December 2017

Polisi yachunguza waliotapeli wanawake kupitia mitandaoni

POLISI imeanza kuchunguza waliotapeli wanawake kwa kutumia mitandao huku wengine zaidi wakijitokeza na kukiri kutapeliwa na mzungu aliyetajwa na gazeti hili katika toleo lake la jana.


Aidha Jeshi la Polisi Kitengo cha Viwanja vya Ndege limesema litawafuatilia wafanyakazi wake ambao majina yao yanatumika katika utapeli huo. Katika toleo la jana, gazeti hili lilieleza kuwa kupitia ahadi ya zawadi kubwa ikiwemo fedha na kutekwa kimapenzi kwa njia ya mtandao, mamia ya wanawake wa Jiji la Dar es Salaam wamejikuta wakitapeliwa mamilioni ya fedha na mzungu anayejitambulisha kwa jina la Don Collins raia wa Uingereza.
Hilo lilibainika baada ya gazeti hili kufanya uchunguzi kwa muda wa zaidi ya mwezi mmoja na kuzungumza na wanawake mbalimbali ambao ni waathirika wa utapeli huo, ambao chanzo chake ni uhusiano wa Facebook.
Matapeli walio katika mtandao wa mzungu Collins huwafuatilia wanawake kwenye mitandao ya kijamii hasa Facebook ambapo huanza kwa kuwaomba urafiki wa kimapenzi na kisha kupeana namba za simu na ndipo mwanzo wa mawasiliano ya kina yanapoanza na baadaye kutapeliwa.
Kutokana na habari hiyo baadhi ya vituo vya televisheni na redio jana viliisoma habari hiyo katika vipindi vinavyorushwa moja kwa moja (live) ambapo wanawake wengi zaidi walipiga simu na kueleza ama wao wenyewe au rafiki, na ndugu zao nao kutapeliwa.
Miongoni mwa televisheni zilizotoa nafasi kwa wananchi kutoa maoni yao au kueleza kama wamewahi kukumbana na mkasa huo, ni Kituo cha Televisheni cha Channel Ten, ambapo mwendeshaji wa kipindi cha magazeti asubuhi, Mary Edward alisema pia amewahi kukumbana na mkasa huo ingawa alishituka kabla ya kutapeliwa.
“Yaani mimi baada ya kuisoma ile habari ya kwenye gazeti lenu, zilimiminika meseji za wanawake wakilalamika kuibiwa kwa staili kama hiyo, sasa hapo ndiyo nikabainisha kuwa kumbe janga ni kubwa zaidi la wizi kwa kutumia staili hii,” alisema Mary.
Mtangazaji huyo alisema, matapeli wa aina hiyo wengi wao wapo hapa hapa nchini na kuwa mara nyingi huwafuatilia na kuwajua wanawake wanaowavizia ili kuwaibia huku wakitumia mbinu za kuwataka kimapenzi na kuwapa ahadi kemkem.
Akizungumzia sakata hilo, Kamanda wa Polisi Kitengo cha Viwanja vya Ndege nchini, Matanga Mbushi alisema kikosi chake kinafuatilia kiundani wizi unaofanywa na matapeli hao na kuhusisha viwanja vya ndege. Alisema matukio kama hayo yanaathiri taswira ya viwanja vya ndege nchini na kuongeza kuwa matapeli wa aina hiyo wanapaswa kusakwa na kuchukuliwa hatua kali za kisheria.
Hata hivyo, alitoa mwito kwa wananchi kuwataka waepuke kutuma fedha za malipo ya aina yoyote ile yanayohusiana na viwanja vya ndege kwa njia za mawasiliano ya simu bila ya kuwa na uhakika wa nani wanamtumia. Pia aliweka wazi kuwapo kwa mfumo madhubuti wa ulipwaji wa fedha kwenye viwanja vya ndege, ambao si rahisi kwa matapeli kuutumia. Alisema kwa wananchi ambao wanaambiwa kutuma fedha ili mizigo yao ipitishwe kwa njia zisizokuwa halali katika viwanja vya ndege wanafanya makosa kisheria na ni sawa na kushirikiana na wezi.
“Sasa kama wewe upo Dar es Salaam halafu mtu anataka utume fedha ili mizigo yako iachiwe kwenye Kiwanja wa Ndege wa Julius Nyerere (JNIA) ni kwa nini usije mwenyewe kiwanjani kuona nini cha kufanya. “Sasa unajikuta ukiibiwa fedha nyingi huku mwenyewe ukidhani kuwa unacheza dili ya kupitisha mzigo isivyo halali kiwanjani,” alisema Kamanda Mbushi.
Aliongeza; “hili suala hebu ngoja nilifuatilie kiundani ili kubainisha ni kwa nini kwanza wanatumia majina ambayo yanaendana na wafanyakazi wa ndani ya viwanja vya ndege, ninawashauri matapeli hao kuacha kuchafua hadhi ya viwanja vya ndege kwa kufanyia utapeli wao,” aliongeza.
Msaidizi Mkuu wa Kitengo cha kukabiliana na uhalifu kwa njia ya mtandao, Mwangasa Joshua kupitia gazeti hili aliwataka wanawake au watu wengi ambao wametapeliwa na mtandao huo kufika Polisi ili kutoa taarifa ili waweze kusaidiwa badala ya kuhofia.
Uchunguzi wa gazeti hili ulibaini kuwa wengi wa wanaofanyiwa utapeli huo wanasita kwenda Polisi kutoa taarifa wakiamini kuwa watakamatwa kwa kuhusika na mtandao wa usafirishaji wa fedha isivyo halali, na hivyo kujikuta wakiugulia maumivu ndani kwa ndani.
Jana dada mwingine aliyejitambulisha kwa jina la Jania Abdul alisema aliwahi kutapeliwa Sh 200,000 baada ya kutakiwa kutuma ili kuwapa hongo askari wa Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Kilimanjaro (KIA) ili kupitisha mzigo aliotumiwa na mzungu Collins na alipobaini kuwa ametapeliwa alishindwa kutoa taarifa Polisi kwa kuhofia na yeye kukamatwa.
Mbinu inayotumika Matapeli hao huwafuatilia wanawake kwenye mitandao ya kijamii hasa Facebook ambapo huanza kwa kuwaomba urafiki na kisha kupeana namba za simu na ndipo mwanzo wa mawasiliano ya kina yanapoanza. Mtandao huo wa matapeli hutumia namba mbalimbali za simu katika kuwatapeli wanawake zikiwemo namba za Ulaya, Marekani na za nchi jirani katika kuwasiliana na walengwa wao kwa njia za ujumbe mfupi wa maneno, huku gia yao ya kwanza ikiwa ni kuomba uhusiano wa kimapenzi.
Vyanzo vya kuaminika vilivyozungumza na gazeti hili, wakiwemo baadhi ya wanawake ambao tayari wametapeliwa fedha nyingi, vilisema wazungu hao baada ya kuomba urafiki na kukubaliwa huendeleza mawasiliano kwa njia ya ujumbe mfupi au mazungumzo na wahusika kwa kasi ili kuwaaminisha juu ya uhusiano wao.
Wakati wote wa mawasiliano wazungu hao hutoa ahadi mbalimbali kwa wanawake huku wakiwaahidia kuwatumia zawadi mbalimbali kama simu za gharama kubwa, kompyuta mpakato, Ipad na fedha Dola za Marekani kati ya 20,000 na 30,000, huku lengo lao mahususi ikiwa ni kuwatapeli.

No comments:

 

ADVERTISE WITH US

AFRICAN FASHION

PLACE YOUR ADS HERE!