Tuesday 26 December 2017

EAC yajivunia maarifa kujikinga na ebola

USHIRIKIANO wa kikanda, kibara na hata kidunia, unadhihirisha kuwa wa muhimu katika ujenzi wa misingi imara ya maendeleo, ambayo nguzo yake kuu na ya awali kabisa ni afya, na sasa Afrika Mashariki inajivunia makubwa iliyopata juu ya ebola na kujikinga nayo.


Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) ilituma wataalamu wake Afrika Magharibi, kwenye umoja mwingine kama huu (ECOWAS) kwa ajili ya kujifunza, kubadilishana uzoefu kisha kurudi nchini na kuona yapi yanayofaa kwa ukanda huu.
Katika mazungumzo yake na ‘HABARILEO – Afrika Mashariki’ mjini hapa, Mkuu wa Idara ya Mawasiliano na Umma katika Sekretarieti ya EAC, Owora Othieno, alisema kwamba wamepata mafunzo makubwa kwa baadaye, hivyo kwamba watakuwa na uwezo mkubwa wa kujikinga na maambukizi sampuli hiyo.
Othieno alisema wataalamu wa EAC, walijifunza juu ya mapambano dhidi ya ebola, kwa sababu Afrika Magharibi walipata kuathiriwa kwa kiasi kikubwa hata kwa vifo. Wataalamu hao walikuwa huko hadi mwezi uliopita. Baada ya kurejea, EAC kwa kushirikiana na wadau wake iliandaa warsha ya siku tatu iliyofanyika nchini Kenya.
Wadau wa EAC walioshiriki kuandaa mkutano huo ni Shirika la GIZ la Ujerumani, Benki ya Maendeleo ya Ujerumani na mtandao wa nchi za EAC wa kukabili magonjwa yanayoambikiza.
Naibu Katibu Mkuu wa EAC (Fedha na Utawala), Jesca Eriyo alisema ilikuwa muhimu kupeleka wajumbe wenye utaalamu Afrika Magharibi kujifunza, akisema “magonjwa hayana wala hayahitaji pasi za kusafiria – yanaweza tu yenyewe kuvuka mipaka.”
Alisema hiyo ilikuwa warsha ya kwanza ya aina yake katika jumuiya, ikienda kwa siku tatu, ambapo ilijumuisha madaktari, wauguzi na wataalamu waliobobea katika magonjwa ya kuambukiza wapatao 50 miongoni mwa 500 waliomo Afrika Mashariki.
Pamoja nao, walikuwamo maofisa wengine wengi wa masuala ya afya. Walikuwamo pia wataalamu waliohatarisha maisha yao kwa kujitolea kupelekwa Afrika Magharibi kupambana na ebola, ugonjwa uliolipuka mwaka 2014 na 2016.
Kwa mujibu wa Shirika la Afya Duniani (WHO), maradhi hayo yaliua watu zaidi ya 11,000 wakati wengine zaidi ya 30,000 waliambukizwa na kulikuwa na hofu kubwa kwamba ugonjwa huo ungeweza kusambaa hadi Afrika Mashariki na maeneo mengine.
Othieno alisema kwamba wataalamu hao pamoja na viongozi wengine, walisikia mambo yaliyotokea Afrika Magharibi juu ya ebola, hatua zilizochukuliwa, changamoto, mafanikio na kipi kinatakiwa kufanyika kwa ajili ya kujilinda dhidi ya maambukizi ya aina hiyo.
Katika majumuisho yao, washiriki waliona kwamba ili kufanikisha makabiliano dhidi ya ugonjwa huo lazima kuwapo utashi wa kisiasa, mipango ya kitaifa na kikanda iwekwe kwa ajili ya makabiliano ya dharura na kupatiwa rasilimali za kutosha

No comments:

 

ADVERTISE WITH US

AFRICAN FASHION

PLACE YOUR ADS HERE!