Saturday, 18 November 2017

Tanesco, Wizara wapewa Siku 30 kubomoa majengo

MENEJA wa Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS) Mkoa wa Dar es Salaam, Julius Ndyamukama amesema wametoa notisi ya mwezi mmoja kwa Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) na Wizara ya Maji na Umwagiliaji kubomoa sehemu ya majengo yao ili kupisha ujenzi wa barabara za juu katika makutano ya Ubungo (Ubungo Interchange).


Juzi Rais Magufuli aliwaagiza Tanroads kuvunja sehemu ya majengo hayo yaliyopo katika hifadhi ya barabara ili kupisha ujenzi huo unaotarajiwa kugharimu zaidi ya Sh bilioni 188.71 hadi kukamilika kwake Septemba, 2019.
Akizungumza na gazeti hili kwa njia ya simu jana, Ndyamukama alisema wameanza kutoa notisi jana ili kuwapa muda wamiliki hao kuhamisha mali zao. Alisema majengo hayo yote yapo katika hifadhi ya barabara na yanatakiwa kuondoka, ila Rais alisema kama ikishindikana waondoe sehemu ya majengo hayo.
“Zoezi la ubomoaji huwa lina utaratibu wake ni lazima tuwape notisi, hivyo tumewapa notisi ya mwezi mmoja ili waanze kuhamisha mali zao na kubomoa wakishindwa baada ya hapo sisi ndiyo tutabomoa,” alieleza Ndyamukama.
Kwa upande wake, Katibu Mkuu Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano- Ujenzi, Joseph Nyamhanga alisema watatekeleza kwa haraka maagizo hayo ili mradi huo ukamilike kwa wakati na kwa muda uliopangwa na kuondoa changamoto ya msongamano wa magari katika Jiji la Dar es Salaam.
Mradi huo ni kati ya miradi mikubwa inayotekelezwa ikiwa ndani ya Ilani ya Uchaguzi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) ya 2015- 2020 waliyoiahidi wakati wa kampeni za Uchaguzi Mkuu wa 2015 na umelenga kupunguza msongamano wa magari katika barabara za Morogoro, Nelson Mandela na Sam Nujoma.
Nyamhanga alisema zaidi ya magari 65,000 yanapita kila siku katika makutano ya barabara za Morogoro, Mandela na Sam Nujoma eneo la Ubungo hali inayosababisha msongamano katika barabara ya Morogoro ambayo ndiyo lango kuu la kuingia na kutoka jijini Dar es Salaam.
“Sisi tumepokea maagizo hayo na kinachotakiwa ni utekelezaji, kwa hiyo Tanesco na Wizara ya Maji watapewa notisi ili waweze kujiandaa kuvunja jengo hilo kwa muda unaotakiwa na kama watashindwa tutalivunja sisi wenyewe,” alifafanua.
Alisema kwa kawaida mtu ambaye ameingia katika hifadhi ya barabara hutakiwa kuvunja mwenyewe ila anaposhindwa au kuchelewa kufanya hivyo wanamsaidia kuvunja na yeye kutakiwa kulipa gharama.
Aidha, aliwataka watu wote waliojenga kwenye hifadhi ya barabara nchi nzima kuondoa nyumba zao na maendelezo hayo kutoka kwenye hifadhi ya barabara vinginevyo sheria itachukua mkondo wake.

No comments:

 

ADVERTISE WITH US

AFRICAN FASHION

PLACE YOUR ADS HERE!