TAASISI ya Matibabu ya Mifupa na Mishipa ya Fahamu (MOI) sasa itakuwa na nafasi nzuri zaidi ya kuhudumia majeruhi wake katika hatua za kibingwa, baada ya kuzinduliwa kwa benki ya damu katika taasisi hiyo.
Benki hiyo ya damu iliyopatikana kwa ufadhili wa Mfuko wa Kuwait kwa gharama ya Sh milioni 220 sawa na Dola za Kimarekani 100,000, imezinduliwa na Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu.Kuwapo kwa benki hiyo kutasaidia kuongeza kiwango cha akiba ya damu katika taasisi hiyo ambayo inahudumia zaidi majeruhi wa ajali mbalimbali.
Awali damu kwa ajili ya kusaidia kupatikana kwa tiba za majeruhi wa ajali ilikuwa inapatikana kutoka Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH) ambayo nayo imekuwa ikizidiwa. Wakati mahitaji halisi ya damu kwa siku ni uniti 13 hadi 20, lakini uniti zinazopatikana kwa sasa ni kati ya 5 hadi 10 na hivyo kuwapo kwa benki hiyo kutawezesha kuwapo kwa kampeni ya kuiwezesha benki hiyo kuwa na akiba ya kutosha.
Akizungumza katika uzinduzi wa benki hiyo jana Dar es Salaam, Waziri Ummy Mwalimu alisema ipo haja kwa Watanzania kujenga tabia ya kuchangia damu ili kuokoa maisha ya wagonjwa nchini. Alisema wananchi wengi wanampigia simu wakimwomba awasaidie ili wagonjwa wao walioko kwenye hospitali mbalimbali waweze kupatiwa damu. “Tunakushukuru sana Balozi wa Kuwait kwa msaada mnaotupatia kwani unaisaidia serikali kutatua changamoto kwenye sekta ya afya lakini pia kupunguza idadi ya wagonjwa wanaotakiwa kupelekwa kimatibabu nje ya nchi,” alisema.
Alisema kuwapo kwa damu ya kutosha kutawezesha upasuaji mkubwa ambao kwa kawaida huhitaji damu ya kutosha kuwapo. “Lengo la serikali ni kuimarisha matibabu ya kibingwa ili Watanzania watibiwe hapahapa nchini badala ya kutumia gharama kubwa kuwapeleka nje ya nchi,” alieleza Waziri Ummy. Kwa upande wake Balozi wa Kuwait nchini, Jasem Al Najeem alisema kwamba Kuwait kupitia taasisi zake za Kiserikali na za Misaada inajisikia fahari kushirikiana na Serikali ya Tanzania katika kuimarisha sekta ya afya nchini.
Alisema ataendelea kuuomba Mfuko wa Kuwait wa kuwasaidia wagonjwa kuendeleza misaada yake kwa benki hiyo ya damu kama sehemu ya kuunga mkono kampeni ya kuchangia damu. “Maabara hii ina viwango vya kimataifa na vile vilivyowekwa na Wizara ya Afya ya Tanzania. Kama tulivyosaidia Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete kwa kutengeneza chumba cha upasuaji na kufunga vifaa vya kisasa vyenye thamani ya Dola za Kimarekani 135,000, leo hii tunazindua Maabara ya Benki ya Damu yenye thamani ya Dola za Marekani 100,000,” alisema Balozi wa Kuwait, Jasem Al Najeem.
Baada ya uzinduzi huo, Balozi wa Kuwait alikuwa wa kwanza kuchangia damu, lakini pia akina mama 40 kutoka Taasisi ijulikanayo kama ‘Wanawake Kwenye Usukani’ nao walifika kuchangia damu. Mafanikio kwenye Sekta ya Afya nchini Waziri wa Afya alitumia fursa hiyo ya uzinduzi wa benki ya damu jana kuelezea baadhi ya mafanikio ambayo Serikali ya Awamu ya Tano imeyapata kwa kipindi cha miaka miwili tangu iingie madarakani.
Ummy alisema kwa mwaka 2015/2016, Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete ilikuwa inawafanyia upasuaji wagonjwa 30 kwa mwezi, lakini kwa sasa imeongezewa uwezo na inawafanyia upasuaji wagonjwa 60 kwa mwezi. Pia rufaa za wagonjwa kupelekwa nchini India kwa matibabu imepungua kutoka 66 mwaka 2015 hadi kufikia wagonjwa 33 kwa sasa baada ya kuimarishwa kwa Taasisi hiyo ya Moyo.
“Mwaka 2015, wagonjwa 423 walipelekwa nje kwa matibabu ya magonjwa mbalimbali kama vile moyo, saratani, figo, masikio na mishipa ya fahamu, lakini mpaka mwezi wa kumi mwaka huu, idadi hiyo imepungua hadi kufikia wagonjwa 209. “Mwaka 2015, Chumba cha Uangalizi Maalumu (ICU) kilikuwa na vitanda 21, lakini mpaka leo kuna vitanda 75,” alieleza Waziri Ummy.
Mafanikio mengine aliyoyataja ni uwezo wa kupandikiza vifaa maalumu kwa wagonjwa wenye matatizo ya kusikia. Alisema ilikuwa inagharimu Sh milioni 100 kupata huduma hiyo nje ya nchi, lakini kwa sasa inapatikana hapa nchini kwa Sh milioni 34. Ili kusaidia upatikanaji wa damu na kuwafanya wananchi kuchangia kwa urahisi, Waziri Ummy alisema kuwa serikali imeamua kushusha huduma ya uchangiaji damu kwenye ngazi za mikoa badala ya kutegemea Mpango wa Taifa wa Damu Salama pekee. Alisema mpaka sasa huduma hiyo inapatikana kwenye mikoa saba na mikoa mingine mitano itafuata. Aliwataka MOI kuitunza benki hiyo ya damu kwani ni ukombozi wa Watanzania wote.
No comments:
Post a Comment