Thursday, 23 November 2017

Kafulila ang’oka Chadema akisema hana imani na upinzani

ALIYEWAHI kuwa Mbunge wa Kigoma Kusini (NCCR-Mageuzi), David Kafulila amejivua uanachama wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema). Amefanya hivyo kwa kile alichodai kuwa hana imani tena na upinzani, kama jukwaa salama la kupambana na ufisadi.


Kafulila amesema kuwa vyama vya upinzani nchini vimepigwa ganzi na kupooza ghafla katika harakati zake za kupambana na ufisadi, baada ya Rais Dk John Magufuli kuendesha vita hiyo kwa mafanikio makubwa.
Alisema mafanikio hayo ya Rais Magufuli, yameufanya upinzani kuwa siyo jukwaa salama tena katika vita dhidi ya ufisadi; na ndiyo maana kwa hiari na utashi wake, ameamua kujivua uanachama wa Chadema.
“Tangu Rais Magufuli aingie madarakani, vita ya miaka mingi dhidi ya ufisadi imechukua sura mpya. Watuhumiwa na wahusika wa rushwa kubwakubwa ambao walikuwa hawaguswi, tunashuhudia wakifikishwa mbele ya vyombo vya sheria, juhudi hizi zinapaswa kuungwa mkono na watu wote na vyama vyote vilivyojipambanua kupambana na ufisadi,” alieleza Kafulila.
Kwa mujibu wa Kafulila, ambaye siku zote alijipambanua na kujitoa muhanga kupambana na ufisadi kupitia jukwaa la Bunge, vyama vya siasa na shughuli za kijamii kwa ujumla, baada ya uchaguzi mkuu wa mwaka 2015, vyama vya upinzani nchini vinaonekana kupigwa ganzi na kupooza katika juhudi zake za kupambana na ufisadi.
Baada ya kujivua uanachama, Kafulila alisema kuwa atatangaza siku za hivi karibuni jukwaa jipya la harakati zake dhidi ya ufisadi. Maamuzi hayo ya Kafulila yanakuja siku moja tu baada ya wanasiasa sita kutoka vyama vya upinzani kujiunga na Chama Cha Mapinduzi (CCM) juzi Ikulu jijini Dar es Salaam.
Wanasiasa hao ni Katibu Mkuu wa Wizara ya Maji na Umwagiliaji, Prof. Kitila Mkumbo (ACT-Wazalendo), Lawrence Masha (Chadema), Patrobas Katambi (Chadema), Edna Sunga (ACT-Wazalendo), Samson Mwigamba (ACTWazalendo) na Albert Msando (ACT-Wazalendo).
Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM, Humphrey Polepole alisema jana kuwa kuna wanasiasa zaidi ya 200, wameomba kujiunga na chama hicho tawala. Ikumbukwe kuwa mwaka jana Kafulila alihama NCCR-Mageuzi na kujiunga Chadema, akieleza kuwa alikwenda huko kwa kuwa ni muhimu kwa watu wenye nia ya mabadiliko kuwa katika chama kimoja ili kufupisha safari.
Katibu Mkuu wa Chadema, Dk Vincent Mashinji alisema kuwa anamtakia kila heri Kafulila, lakini akaeleza kuwa Kafulila si mkaaji kokote anakoenda. Dk Mashinji alisema, “Kama Chadema tunamtakia kila la heri, sisi hatuna shida na yeye kuhama kwa sababu amekuwa akihama kila siku. Alianza Chadema, akaenda NCCR -Mageuzi, kisha akarudi Chadema. Sasa sijui anaenda CCM lakini si mkaaji.” Imeandaliwa na Matern Kayera na Regina Mpogolo

No comments:

 

ADVERTISE WITH US

AFRICAN FASHION

PLACE YOUR ADS HERE!