BODI ya Mikopo ya Elimu kwa Wanafunzi wa Elimu ya Juu nchini (HELSB) imesema wanafunzi ambao hawajapangiwa mkopo ni pamoja na waliokuwa na udahili katika chuo kikuu zaidi ya kimoja nchini na hata waliothibitisha awali wakitaja chuo watakachokwenda lakini baadaye wakabadilisha.
Imesema jana jijini Dar es Salaam, kundi lingine la waliokosa mikopo ni pamoja na waliowasilisha maombi yakiwa na dosari kadha wa kadha na wengine wakiwa na sifa pungufu za uhitaji wa mkopo.
Bodi hiyo imesema hayo huku wanafunzi waliokosa mikopo wakiendelea kung’ang’ania kwenye ofisi za bodi hiyo, wakishinikiza wasikilizwe shida zao waendelee na masomo kwani vyuo vimeshafunguliwa.
Katika kusaidia, HELSB imeahidi kufungua dirisha la rufaa ya kupata mikopo kuanzia Jumatatu ijayo, Novemba 13, mwaka huu ili kuwapa fursa wanafunzi ambao hawajaridhika kuwasilisha rufaa zao kupitia vyuo walivyopata udahili, na majina ya watakaofanikiwa kupata mikopo, yatatolewa Novemba 30, 2017.
Mkurugenzi Mtendaji wa HELSB, Abdul-Razaq Badru alisema hayo jana wakati akitoa ufafanuzi kuhusu wanafunzi wa elimu ya juu kukosa mikopo na kusababisha wavamie ofisi za bodi Mwenge tangu juzi.
Badru alisema kwa takwimu za jana (juzi) wanafunzi 200 awali walikuwa wamethibitisha vyuo ambavyo wamechaguliwa lakini wakaenda vyuo vingine wakati fedha za mkopo zikiwa zimepelekwa kabla ya vyuo kufunguliwa na wanafunzi kati ya 400 na 500 walikuwa na sifa pungufu katika kupata mkopo hiyo.
Kuhusu wasiopata mkopo, Badru alisema wale waliopangiwa vyuo na wakaenda vyuo vingine, bodi inawasiliana na vyuo ili kufanya usajili wa wanafunzi haraka na taarifa zao zifikishe HELSB ili ifanye kazi ya kuwasilishia fedha zao katika vyuo walivyoripoti kabla ya mwisho wa mwezi huu wa Novemba.
“Wale ambao taarifa zina upungufu na wana sifa za wazi yatima, walemavu au waliosomeshwa na taasisi, taarifa zao zitapokewa na kufanyiwa kazi na zitakazokamilika watapangiwa mikopo wiki hii,” alisema.
Kuhusu dirisha la rufaa, alisema awali lilikuwa likifunguliwa kwa siku 90 baada ya vyuo kufunguliwa lakini kufuatia suala hilo, Bodi imeamua kulifungua tena kuanzia wiki ijayo ili kuwapa fursa nyingine waombaji wote ambao hawajaridhika kuwasilisha rufaa kupitia vyuo walivyopata udahili wapangiwe.
“Tunatoa mwito kwa uongozi wa vyuo vyote kupokea maombi ya rufaa za wanafunzi na kuwasilisha kwa Bodi iweze kutoa orodha ya waombaji waliofanikiwa rufaa zao ifikapo Novemba 30,2017,” alisema.
Kuhusu upangaji wa mikopo kwa mwaka 2017/18 alisema bajeti ya jumla ya mikopo kwa kipindi hicho ni Sh bilioni 427.54 kwa ajili ya wanafunzi 122,623 na fedha hiyo inajumuisha malipo ya ada za wanafunzi wenye mikopo pamoja na fedha za chakula na malazi, vitabu, ada na mahitaji ya vitivo.
Alisema fedha zilizohitajika kwa ajili ya robo ya kwanza ya mwaka 2017/18 ni Sh bilioni 147.06 ambazo tayari bodi imeshapokea kutoka serikalini ambapo hadi kufikia Novemba 6, 2017 jumla ya wanafunzi 29,578 wa mwaka wa kwanza wamepangiwa mikopo yenye thamani ya Sh bilioni 96.5.
Alisema fedha hizo tayari zimeshatumwa vyuoni ili kuwawezesha kuanza masomo na fedha za mikopo ya wanafunzi wote wanaoendelea na masomo zimetumwa vyuoni ili kuwawezesha kuendelea na masomo.
Alisema kati ya wanafunzi wa mwaka wa kwanza 29,578, yatima ni 937, wenye mzazi mmoja 5,118, walemavu 486, wenye uwezo mdogo au kipato duni 23,037, wanawake 9,940 na wanaume ni 19,638.
Kuhusu sifa za msingi za kupata mkopo alisema ni uyatima, ulemavu, walio na kipato duni wakitoka familia zenye kipato duni, na wenye barua za uthibitisho walisomeshwa kabla ya kujiunga elimu ya juu.
No comments:
Post a Comment