ZAIDI ya watu 10,000 wamepatiwa huduma ya matibabu na vipimo kwa madaktari kutoka China waliokuja na meli ya uchunguzi na matibabu ya China (Peace of Ark) huku wagonjwa wengi wakibainika kuwa na magonjwa yasiyoambukiza ikiwemo kisukari, presha na moyo.
Wakati watu hao wakitibiwa, Rais Magufuli ameishukuru Serikali ya China kwa kuleta meli hiyo na kutoa matibabu wananchi wengi waliokuwa wanahitaji tiba na kusema kuwa Tanzania inaikaribisha kwa wakati mwingine wowote ili isaidie juhudi za kutoa matibabu kwa wananchi.Aliiomba China ije iwekeze katika ujenzi wa vituo vya tiba Tanzania.
Akizungumza katika hafla iliyofanyika juzi ya kuwaaga madaktari hao zaidi ya 380, Mganga Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Dk Grace Maghembe alisema watu waliosajiliwa ni zaidi ya 11,000 ambayo ni mara nne ya walengwa kwani kwa muda wa siku tano madaktari hao walitarajia kuwahudumia wagonjwa 3,000 ambao mkoa wa Dar es Salaam ulipanga waje.
Alisema watu waliohudumiwa ni asilimia 88 ya waliojitokeza ambapo wagonjwa 3,244 sawa na asilimia 31 walipatiwa matibabu ndani ya meli hiyo huku wagonjwa wengine zaidi ya 7,248 sawa na asilimia 69 ya wagonjwa wakionwa na madaktari wazawa na waliobaki 800 bila kupatiwa huduma wakishauriwa kwenda katika hospitali mbalimbali za mkoa huo.
Grace alisema wagonjwa 23 walifanyiwa upasuaji ndani ya meli na kati yao wanane walifanyiwa upasuaji wa macho, sita upasuaji wa henia, sita upasuaji wa uvimbe mbalimbali na watatu walifanyiwa upasuaji wa koo, masikio na pua na wengine 88 walifanyiwa upasuaji na madaktari wa Taasisi ya Mifupa (MOI) na Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete (JKCI).
Pia alisema wagonjwa 681 walifanyiwa vipimo vya Ultrasound, wanawake 473 wanaume 208, wagonjwa 721 walifanyiwa vipimo vya mionzi (X-ray) wanawake 319, wanaume 402 na wagonjwa 293 walifanyiwa kipimo cha CT-scan wanawake wakiwa 171 wanaume 122.
Dk Maghembe alisema wagonjwa 2,465 walitakiwa kupewa dawa kati yao asilimia 99 walipatiwa dawa kulingana na magonjwa yao na dawa zilizotolewa zilikuwa za maumivu, magonjwa ya ngozi, presha, kisukari, dawa za viuasumu pamoja na dawa za asili za Kichina.
Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda alimshukuru Balozi wa China nchini, Jeshi la China na madaktari waliowahudumia wananchi na kueleza dhamira ya Serikali ya Awamu ya Tano kugusa maisha ya wananchi kwa kutatua changamoto kwa kuboresha sekta ya afya.
“Ni upendo wa pekee kwa nchi ya China kwa Watanzania kwa kuwa wamewahudumia Watanzania kwa upendo kwa kuwapa chakula, malazi na matibabu, hii ni kwa sababu ya mahusiano mazuri aliyoyaanzisha hayati Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere. Tunaishukuru Serikali yenu kwa kuwa na meli hii inayogusa maisha ya wengi,” alisema Makonda.
Kiongozi wa meli hiyo, Meja Jenerali Guan Bailin ameishukuru Serikali kwa mapokezi mazuri na kumshukuru Makonda aliyesema alionesha ushirikiano mkubwa hata walipokwama alisaidia na kazi ikaendelea lengo ikiwa ni kuhakikisha kila aliyejitokeza anapatiwa huduma. Alisema hawezi kusema meli hiyo itarejea lini nchini kwa kuwa inazunguka katika nyingi na kwamba siyo mara ya kwanza kuja hivyo ipo siku itarejea tena na kutoa huduma kwa watu.
Rais Magufuli, kabla ya kufanya ziara ya kushtukiza katika maeneo ya utunzaji wa magari yaliyokaa bandarini kwa muda mrefu jana, alitembelea meli hiyo ya China ambayo tangu Novemba 20, mwaka huu ilikuwa ikitoa huduma za matibabu ya bure kwa wananchi. Meli hiyo ni hospitali yenye vifaa vyote vya uchunguzi na dawa, madaktari 115, wauguzi na wafanyakazi 266 na vitanda vya kulaza wagonjwa 300.
Kwa wiki moja, imetoa huduma za matibabu kwa wagonjwa 6,421 wakiwemo 31 waliofanyiwa upasuaji. Iliondoka nchini jana. Kamanda aliyeongoza timu ya madaktari, wauguzi na wafanyakazi katika meli hiyo, Guan Bailin alisema meli hiyo imekuja kwa mara ya pili nchini Tanzania na China inafanya hivyo kwa kutambua uhusiano na ushirikiano wa kihistoria na kidugu kati ya Tanzania na China.
Akizungumza baada ya kutembelea vitengo mbalimbali ya uchunguzi na matibabu ndani ya meli hiyo, Rais Magufuli aliishukuru Serikali ya China kwa kuleta meli na kutoa matibabu wananchi wengi na akaikaribisha wakati mwingine isaidie kutoa matibabu kwa wananchi.
Rais Magufuli alimkabidhi Kamanda Bailin barua ya shukrani kwa Rais wa China, Xi Jinping yenye shukrani zake kwa ujio wa meli hiyo na pia amemuomba Rais Xi kuisadia Tanzania kupata meli kama hiyo na kuendelea kuwaleta madaktari kutoka China kusaidia matibabu. “Kwa wiki moja mmetoa matibabu kwa wananchi 6,421.
Nimeambiwa waliojiandikisha walikuwa zaidi ya 10,000 hii inaonesha kuna mahitaji makubwa ya tiba kwa hiyo natoa wito kwa ndugu zetu wa China mje muwekeze katika ujenzi wa vituo vya tiba,” alisema Rais Magufuli.
Aliwashukuru madaktari wa China waliotoa huduma na madaktari wa nchini walioshirikiana nao na akampongeza Makonda kwa kusimamia shughuli hiyo na ametaka wakuu wa mikoa yote nchini waige mfano wa Makonda kuwapenda na kuwapigania wananchi wao.
No comments:
Post a Comment