LICHA ya Sera ya Wazee kuelekeza wapatiwe matibabu bure, huduma hizo zimekuwa na changamoto kubwa katika baadhi ya hospitali, vituo vya afya na zahanati nchini.
Wakizungumza kwa nyakati tofauti katika Kongamano la Wazee lililofanyika mjini hapa likiwa ni sehemu ya maadhimisho ya Siku ya Wazee Duniani, Raphael Chandalo kutoka Kasulu Kigoma alisema wamekuwa wakinyanyaswa sana wakati wakipata huduma hizo za afya. “Wazee tunapofika katika vituo vya afya ili kupewa huduma bure tumekuwa tukinyanyaswa na kukandamizwa hata kuwekwa pembeni kabla ya kupewa huduma hizo,” alisema.
Mzee mwingine, Albert Sagembe alisema “Ukienda hospitali wazee bado tunapata usumbufu kwenye matibabu kutokana na maneno ya kejeli na kudharauliwa, wengine tunaona bora kwenda hospitali ya binafsi kujigharamia.” Mwanahamisi Juma, alisema kuna baadhi ya halmashauri chache zinatekeleza vyema sera hiyo lakini zilizo nyingi bado hazijawapa wazee heshima yao wanayostahili katika kutoa huduma hiyo. Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Mtandao wa Mashirika ya Wazee nchini, Sebastian Bulegi, aliiomba serikali kutunga sheria itakayosimamia Sera ya Wazee ili iweze kufanya kazi ipasavyo, kuliko ilivyo sasa.
No comments:
Post a Comment