Sunday 15 October 2017

THAMANI YA MWANAMKE WA KIJIJINI.




Na  Grace Kiondo.

Kila jinsia ina thamani sawa isiyo na shaka dhidi yanyingine.
Dhana ya kuthaminisha jinsia moja zaidi ya nyingine ni ukosefu wa fikira yakinifu na ikiwa yupo mwenye dhana hiyo anapaswa kutambua kwamba hayuko sahihi na bila shaka ni wakati wake kufunua Ubongo wake na kujifunza kwa wengine ni kwanini jinsia zote zina haki sawa na thamani isyoweza kutofautishwa sio tu kwa asilimia bali hata pia kwa mifano ya Ratili.



Linapokuja suala la kimaeneo hapa tunaweza kusema kwamba maeneo yanaweza kutofautishwa kulingana na hali ya kimazingira,Joto,Baridi,Ukame ikiwemo mila,Tamaduni na Desturi.baada ya utangulizi huo sasa najikita moja kwa moja katika hoja yangu ya msingi.
Kila mwaka October 15 Dunia inaadhimisha siku ya kimataifa ya Mwanamkea wa kijijini,bila shaka wakuu wa Dunia waliona umuhimu mkubwa wa kumtambua Mwanamke aliyeko kijijini kwa kuthamini mchango wake.mchango huo sio tu katika jamii yake kijijini bali pia nguvu ya Mwanamke wa kijijini hunufaisha kwa asilimia 75 ya wakaazi wa mijini.
Kadhalika ni muhimu kutambua kwamba nchini Tanzania 75% ya wakaazi waishio mijini wengi wao maisha yao yalianzia Vijijini.
Kwa mnasaba huo utagundua kwamba Wanawake wa vijijini idadi kubwa ndiyo wafanyao kazi za kilimo kote Duniani,wamejikita zaidi katika kuzalisha na kuandaa chakula.mazao wanayolima Wanawake wa Vijijini ndiyo ambayo hununuliwa na wafanyibiashara wa mijini na hatimaye kutawanywa katika maeneo mbalimbali.
Hata hivyo pamoja na juhudi zote hizo mabadiliko ya tabia ya nchi yamesababisha Wanawake hao kushindwa kuzalisha mazao mengi ikilinganishwa na miaka ya nyuma.ni wazi kwamba Wanawake hawa wanahitaji ubunifu mwingine ambao utawawezesha kuendelea kupata mazao bora ambayo hayataathiriwa na mabadiliko hayo.lakini kwa kuangalia mbinu za kiasili katika kutambua magonjwa ambayo yanakumba mazao bado tunashuhudia kufanikiwa kwa asilimia ndogo,hivyo ni jukumu la wataalamu binafsi,serikali kuona haja ya kuwatumia wanataaluma wa kilimo kuwapa elimu ya kukabiliana na mabadiliko ya tabia ya nchi ambayo inawaathiri katika kilimo.
Athari za mabadiliko ya tabia ya nchi,uharibifu wa mazingira unaosababishwa na kazi za binadamu,majanga ya asili ikiwemo hali ya ukame,vimewaathiri na wengine kulazimika kuhama katika maeneo yao,na kwenda kutafuta maeneo ambayo yatakuwa na unafuu.hali hiyo bado haijasaidia kwani inaendelea kuwapa wakati mgumu ambao unasababisha kuyumba kwa familia na ukuaji mdogo wa maendeleo.
Hata hivyo siku hii ya Mwanamke wa Kijijini itakuwa na faida kwao ikiwa Dunia itajikita katika kutekeleza sera za kumwinua Mwanamke huyo kwa vitendo,kwa kuangalia upya mikakati ambayo itampa nafuu huyu Mwanamke kama vile:
(i)Jumuiya ya kimataifa kuibua mbinu kwa kila nchi mwanachama kama mojawapo ya malengo.
(ii)Serikali kurejesha sera ya mabwana Shamba kwa kila Kijiji.
(iii)kugawa mbolea bure na kwa wakati.
(iv)kuwekwa Anuani maalum ambayo itawarahishia Wakulima Wanawake kupata mawasiliano.
(v)kuwawezesha wanawake kumiliki Ardhi bila ya mashariti au kuingiliwa na mila potofu za kumkataza mwanamke kutoweza kumiliki ardhi.
(vi)Sera ya viwanda kuelekezwa kwa Wanawake Wakulima.
Sasa kwa kuwa tunamwangalia Mwanamke wa kijijini ambaye ndiye mzalishaji wa chakula tufikirie pia ni kwanamna gani mwanamke huyu ataweza kupewa elimu ambayo itaweza kumsaidia haswa kwa kuzingatia kwamba Wanawake wengine hawana elimu kubwa ya Dasani wengi wao wakiwa ni wahitimu wa Darasa la Saba,au hata pengine kutojua kusoma na kuandika.kadhalika katika upatikanaji wa Soko lenye tija kwao ni muhimu sana,Wanawake wa Vijijini wengi wao sio watu wenye mbinu za kuuza maneno mengi kama ilivyo kwa Wanawake wa mjini hivyo kuna kila sababu ya kuwezeshwa kupata masoko yenye tija kwa wafanyabiashara wa ndani na nje ya nchi.
Visiwani Zanzibar Wanawake waishio maeneo ya Fukwe za Bahari ni wazalishaji wakubwa wa zao la Mwani.(SEAWEED) hili ni zao ambalo linatajwa kuanza tangu mwaka 1989,Mwani hutumika kutengenezea bidhaa nyingi japokuwa sio wananchi wengi wa Tanzania wenye kufahamu zao hili kwa kina.
Visiwani Zanzibar hili ni zao ambali hulimwa na Wanawake tu na sio rahisi kuona akina Baba wakijishughulisha na ulimaji wa zao hilo.huenda ni kueleze tu kwamba zao hilo hulimwa Bahari na ukulima wake sio kazi rahisi bali ni kazi ambayo huweza kuchukua siku nzima.kilo moja ya Mwani huuzwa kati ya Shilingi Mia Tatu mpaka Mia Tano.ukiangalia bidhaa zinazozaliswa na nchi za nje kama vile China ambayo ndiyo mununuzi mkubwa utagundua kwamba kununua kilo Moja kwa shilingi Mia Tatu au Mia Tano kwa Wakulima hao ni kiasi kidogo sana kwamba hakiwanufaishi Wanawake hao.
Mara kadhaa wakulima hao wamekuwa wakilalamikia bei hiyo kuwa ni ndogo na kwamba kelele hizo wamezianza muda mrefu na mafanikio yake yanakwenda kwa mwendo wa kusuasua.
Bi. Mwanaidi Mcha mkaazi wa kijiji cha Jambiani anasema yeye anategemea zao hilo kwa ajili ya familia yake ikiwemo chakula na kuwasomesha Watoto kutokana na kuwa yeye ndiye anayeangalia familia zaidi kuliko mume wake.
Bi.Faida Haji mkaazi wa Matemwe anasema kulinagan na hali ya Jiografia ya Kijiji cha Matemwe kuwa na ardhi ya Mwamba shughuli inayotegemewa na wakaazi wa hapo ni Wanaume kushiriki katika Uvuvi wa Samaki huku Wanawake wakijishughulisha na ulimaji wa zao la Mwani.hata hivyo Bi Faida anasema bado faida ya ukulima wa Mwani haijaweza kuwanufaisha Wanawake.
Pamoja na Wanawake hao wa maeneo ya Fukwe kujitahidi sana kujiletea maendeleo yao lakini bado kuna vuta nikuvute inayowakabili baina yao na wawekezaji wa Hoteli za kitalii kwani wawekezaji hao hawakubali kuona Wanawake wakiwa katika Fukwe zilizoko kwenye Hotel zao kwani wageni wao huhitaji Fukwe hizo kwa ajili ya kupunga upepo.
Bi Mwanakombo Faki kutoka kijiji cha Nungwi anasema hafurahishwi na kitendo cha wawekezaji kuwakataza kufanya shughuli zao katika Fukwe kwani shughuli hiyo wameirithi toka kwa Wazee wao waliowatangulia,yaani kabla ya utalii kuingia katika Visiwa vya Zanzibar.
Dr Flower Ezekiel Msuya kutoka Taasisi ya sayansi za mazao ya Baharini ya chuo kikuu cha Dar es salaam Tawi la Zanzibar anasema Mwani una faida nyingi mwilini kutokana na kuwa na Vitamini mbalimbali na virutubisho ambavyo husaidia kutibu ugonjwa wa Tezi ya Shingo.ikiwemo matatizo ya Tumbo na ugonjwa wa Ngozi.
Aidha Mwani hutumia kutengeneza Dawa za Meno,viturubisho vya Nywele,Ngozi,Sabuni na pia hutumika katika kutengeneza Keki.
Ni wazi kwamba serikali ya jamhuri ya Muungano kufuatia sera yake ya “Tanzania ya viwanda” ina kila sababu ya kuwaunganisha Wanawake wa Vijijini katika Viwanda kuwapa kipaumbele katika kununua bidhaa zao kwa bei ambayo itawanufaisha.
Wilaya ya Lushoto ni mojawapo ya Wilaya ambayo Wanawake kutoka Vijiji mbalimbali wanalima Mbogamboga pamoja na Mtunda kwa wingi,hii ni Wilaya ambayo ardhi yake inakubali kustawi matunda ya aina tofauti na matunda mengi ambayo yanastawi katika nchi za Ulaya pia hulimwa Lushoto na kustawi vyema.
Katika kuadhimisha siku hii ni vyema tukatafakari maeneo ambayo Mwanamke wa Kijijini ameachwa na sio katika kuwezeshwa katika kilimo pekee,masuala mengi yahusuyo maendeleo yamekuwa na mkwamo kwao katika kuwafikia.masuala ya kutambua haki zao za msingi bado ni changamoto ijapokuwa Taasisi kama vile TAMWA,TAWLA na TGNP yamesaidia sana katika kuwapa elimu akina Mama.lakini katika kumsaidia Mwanamke huyo hatuwezi kutegemea Taaisi hizo na nyingine bali kuweka sera na mijadala ambayo itakuwa ndiyo mwongozo rasmi ambao utafuatiwa na utekelezaji.
Uanziswaji wa Maktaba Vijijini ambazo zitakuwa na vitabu,Computer na Televisheni itasaidia kwa kiasi kikubwa kuongeza wigo wa kusambaza elimu,kwani mafunzo mengi ya kitaalamu ambayo yanaandikwa katika Mitandao haviwafikii Wanawake wa Kijijini.
Hata hivyo siku hii nchini Tanzania inaonekana kama haina mashiko sana kutokana na kutojulikana na wananchi ikiwemo hata Mwanamke mwenyewe wa Kijijini,huenda bado ni siku ambayo imo kwenye Makabrasha ya wasomi tu na wenye kuipanga.ikiwa kweli tunataka kumjali Mwanamke wa Kijijini tutoke maofisini na kwenda kumwaga sera kwa vitendo na sio kutunza maandishi yahusuyo Mwanamke huyo katika Computer zetu.

No comments:

 

ADVERTISE WITH US

AFRICAN FASHION

PLACE YOUR ADS HERE!