Monday 16 October 2017

Taarifa za huduma za afya nchini kuwa za kidijiti

MPANGO Shirikishi wa Takwimu ambao Wizara ya Afya nchini umesema utatumika katika kuunganisha zahanati, vituo vya afya, hospitali za wilaya na mikoa hadi taifa ni muhimu katika kupata taarifa sahihi za wagonjwa na ubora wa huduma za afya wanazopata.


Mpango huo wa takwimu wa kielektroniki ambao utagharimu dola za marekani milioni 75(zaidi ya Sh bilioni 150), ni mpango wa miaka mitano na utakapokamilika utaisaidia serikali kupata taarifa za huduma za afya kwa uhakika kwa ngazi zote za afya chini na hivyo kuachana na mfumo wa kutunza kumbukumbu kwa njia ya vitabu au mafaili.
Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu, amewaomba wadau mbalimbali kujitokeza kuchangia fedha dola milioni 75 (zaidi ya Sh bilioni 160) baada ya Mwenyekiti Mwenza wa Taasisi ya Bill na Melinda Gates, Bill Gates kuchangia dola za marekani milioni 15 (zaidi ya bilioni 15) ili kuufanikisha.
Bill Gates amechangia fedha hizo wakati wa uzinduzi wa awamu ya pili wa Mpango Shirikishi wa Takwimu uliofanywa na Waziri Ummy Mwalimu kwa kushirikiana na Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaawa (TAMISEMI), George Simbachawene pamoja na Bill Gates hivi karibuni wizarani hapo jijini Dar es Salaam.
Mfumo wa kutunza kumbukumbu za wagonjwa, huduma za afya na watoa huduma za afya kwenye makaratasi umepitwa na wakati kutokana na ukweli kwamba siyo mfumo salama na wa uhakika.
Kumbukumbu za wagonjwa kwa ngazi zote za kutolea huduma za afya zimekuwa zikipotea na hivyo kuharibu historia ya matibabu ya mgonjwa, kuleta ugumu wa kumjua mhudumu aliyehusika kutoa matibabu na taifa kukosa takwimu sahihi za huduma za afya zinazotolewa nchini.
“ Kwenye Hospitali ya Taifa ya Muhimbili, kwa siku yalikuwa yanapotea mafaili 70 ya wagonjwa, lakini baada ya kuanza kutumia mfumo wa taarifa wa kielektroniki, upotevu huo wa taarifa za wagonjwa haupo tena,” anasema Waziri Ummy.
Serikali imeweka bayana kuwa lengo la Mpango Shirikishi wa Takwimu ambao utakuwa wa kielektroniki au kidijiti ni kuimarisha usimamizi wa mfumo wa afya nchini, kuboresha utoaji wa huduma na kusaidia maendeleo ya miundombinu ya kitaifa ya kielektroniki katika matumizi bora ya takwimu.
Mfumo wa matumizi ya takwimu wa kielektroniki umeelezwa kufanya vyema katika Mpango Bora wa Takwimu za chanjo katika Mkoa wa Arusha. Katika awamu ya kwanza (2015-2017), Bill Gates alichangia dola za marekani milioni 1.6 (zaidi ya Sh bilioni 3) ambazo zimesaidia kuanzishwa kwa matumizi ya mfumo wa kielektroniki wa chanjo kwa Mikoa ya Tanga na Arusha.
Katika mikoa hiyo, taarifa za chanjo kwa watoto zimeweza kupatikana na kuhifadhiwa kwa usahihi. Kwa mujibu wa Mfamasia Msimamizi wa takwimu na upatikanaji wa chanjo kutoka Mpango wa Taifa wa Chanjo, Ngwegwe Bulula, watoto 85,000 katika mikoa ya Arusha na Dodoma wamesajiliwa kupitia mfumo wa takwimu wa kielektroniki.
Mbali na idadi hiyo ya watoto, Bulula anasema jumla ya watumishi 900 katika mikoa hiyo wamefundishwa namna ya kuutumia mfumo wa kielektroniki ambao unatumika katika vituo zaidi ya 600 Arusha na Tanga.
Bulula anafafanua kuwa katika ngazi ya vituo vya afya, mfumo huu unajulikana kama Usaili wa Chanjo Kielektroniki na kwa ngazi ya wilaya na mkoa hujulikana kama Mfumo wa Usimamizi wa Taarifa za Chanjo (VIMS).
Mtaalamu huyo wa Chanjo anaeleza kuwa, mfumo wa upatikanaji wa taarifa za chanjo kwa watoto kielektroniki katika mikoa ambako unafanya kazi, umesaidia kuondoa changamoto mbalimbali kama vile tatizo la ubora wa takwimu lililokuwepo.
Bulula anasema awali hakukuwa na uhalisia kati ya kiasi cha chanjo kinachotakiwa na idadi halisi ya watoto. “Unaweza kukuta zinapelekwa dozi 1,000 za chanjo kwenye kituo cha afya wakati mahitaji halisi ya watoto wanaohitaji chanjo ni 2,000.
Lakini kupitia mfumo huu, tumeweza kuwafikia watoto kwa asilimia 90 kwa sababu unapomsaili unajua namna ya kumfuatilia kwa kuwa taarifa zake unakuwa nazo,” anaeleza Bulula. Mafanikio ya kutumia mfumo wa taarifa wa kielektroniki yameanza kuonekana kama anavyoeleza Mwuguzi-Mkunga wa Kitengo cha Mama na Mtoto katika Kituo cha Afya Ngamiani jijini Tanga, Millen Nkuzi.
Nkuzi anasema kuwa mfumo wa takwimu wa chanjo wa kielektroniki umewawezesha kujua historia ya chanjo ya mtoto husika. Kupitia mfumo huo, Nkuzi anaeleza kuwa imekuwa rahisi kwa watoa huduma wa afya kujua namba ya utambulisho wa mtoto, taarifa zake cha chanjo, kujua kiasi cha chanjo na idadi ya watoto wanaotakiwa kupata chanjo kwa siku husika, kujua akiba ya chanjo iliyopo ili ziagizwe kulingana na mahitaji, lakini pia kujua taarifa za mama na baba au mlezi wa mtoto.
Faida zingine za mfumo wa kielektroniki zinazopatikana maeneo yaliyotekelezwa mradi huo ni kupunguza ulazima kwa watoa huduma kusafiri kutoka kituo cha afya kwenda wilayani au wilayani kwenda vituo vya afya au mkoani kwa ajili ya kupata taarifa, bali taarifa hizo hupatikana kwa njia ya mtandao au kielektroniki.
Nkuzi anasema pia umeleta urahisi wa kujua idadi ya watoa huduma kwa kila kituo cha afya na ufanisi wa huduma wanazotoa. “ Pia umesaidia kwenye suala zima la usimamizi wa mapato katika vituo vya afya na hospitali za wilaya.”
Waziri Simbachawene amesema serikali imeajiri wahasibu 500 kwenye vituo vya kutolea huduma ili kuongeza uwazi na kujua matumizi ya fedha. “Kupeleka fedha kwenye vituo vya kutolea huduma kama zahanati, vituo vya afya, hospitali za wilaya na mikoa bila kuwa na mfumo kama huu ni vigumu kudhibiti.
Anaongeza: “Matumizi ya mifumo ya kielektroniki ni kuleta mapinduzi katika utoaji wa huduma za afya nchini.” Aidha, Simbachawene anawataka wananchi kuchangamkia huduma bora za afya kwa kujiunga kwenye mifuko ya bima ya afya na kwa kufanya hivyo itarahisisha upatikanaji wa huduma bora za afya.
Ili kuhakikisha Serikali inakuwa na taarifa sahihi za huduma za afya na watoa huduma nchini, Mkurugenzi wa Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (Tehama) wa Wizara ya Afya, Hermes Rulagirwa ameeleza kuwa kupitia mfumo wa kielektroniki, vituo vya kutolea huduma ya afya vitakuwa vikiwasiliana na taarifa za vituo vyote kufika makao makuu.
Anasema kukamilika kwa Mpango Shirikishi wa Takwimu kutaboresha upatikanaji wa takwimu kielektroniki kuanzia ngazi ya utoaji huduma hadi taifa lakini pia matumizi bora ya takwimu hizo.
“Mfumo utaongeza uwajibikaji, kuwaunganisha wadau wa maendeleo kuweza kufikia vituo vingi kwa haraka, kuongeza mapato, kuongeza uwezo wa kufuatilia dawa tangu zinavyotoka Bohari Kuu hadi inapofika kwa mgonjwa, kujua idadi ya watumishi kwa kila kituo cha afya na ufanisi katika utendaji kazi wao,” anaeleza ºRulagirwa.

No comments:

 

ADVERTISE WITH US

AFRICAN FASHION

PLACE YOUR ADS HERE!