Sunday 15 October 2017

Rais Magufuli atoa sababu tatu za kutofuta Mwenge wa Uhuru

Rais  John  Magufuli akipokea Mwenge wa Uhuru 
Rais John Magufuli amesema zipo sababu tatu za msingi zitakazomfanya asiufute mwenge wa Uhuru wakati wa uongozi wake licha ya kuwapo kwa baadhi ya watu wanaotaka aufute.

Mwenge wa Uhuru ulianzishwa Desemba 9, 1961 kwa kupandishwa juu ya kilele cha Mlima Kilimanjaro siku ambayo Tanganyika ilipata uhuru wake kutoka kwa Waingereza.
Akihutubia kwenye maadhimisho ya kumbukumbu ya kifo cha Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere na sherehe za kuzima Mwenge wa Uhuru zilizoambatana na wiki ya vijana katika Uwanja wa Amaan visiwani Zanzibar, Rais Magufuli alisema anawashangaa watu wanaotaka aufute.
Alisema hawezi kuufuta mwenge huo kwa sababu unachochea ukuaji wa maendeleo, unawaunganisha Watanzania na kuendelea kuimarisha muungano uliopo.
“Mimi siwezi kukubali Mwenge ufutwe na ninajua (Rais wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, Ali Mohammed) Dk Shein hawezi kukubali mwenge ufutwe katika kipindi chake,” alisema.
Aliwataka Watanzania kuwapuuza na kuwasuta watu wanaosema ufutwe kwa kuwa uliasisiwa na Baba wa Taifa kabla ya Uhuru na ni moja kati ya tunu za Taifa zinazopaswa kuenziwa.
“Kwa sababu kama umezaliwa Tanzania na unaijua historia ya nchi hii huwezi kuzungumza maneno eti ya kusema Mwenge ufutwe,” alisema Rais Magufuli.
Alisema kwamba moja ya dhana zinazotumiwa na wanaopinga mbio za Mwenge ni gharama japo haina mashiko.
“Nafahamu kuwa mwaka huu Serikali ilitenga milioni462 tu kugharamia mbio za Mwenge, sasa ukilinganisha na kiasi cha fedha zilizotumika kwenye miradi ya maendeleo iliyozinduliwa, hoja hii haina mashiko,” alisema Rais Magufuli.
Alifurahishwa na ripoti ya walioukimbiza Mwenge huo iliyokuwa imeambatana na maagizo ya kutaka kuchukuliwa hatua kwa waliohusika kuhujumu baadhi ya miradi iliyopitiwa.
“Ripoti hiyo tutaifuata ukurasa kwa ukurasa, nukta kwa nukta, kituo kwa kituo ili yote yaliyopendekezwa yaweze kushughulikiwa kikamilifu,” alisema.
Katika taarifa yake, kiongozi wa mbio za Mwenge wa Uhuru 2017, Amour Hamad Amour alisema walibaini kuwapo kwa usimamizi usioridhisha katika utekelezaji wa miradi ya maendeleo kwenye baadhi ya halmashauri na wilaya.
Kiongozi huyo alisema baadhi ya miradi katika sekta ya maji, elimu, barabara na uwezeshaji kiuchumi haikuzinduliwa na mbio za Mwenge kutokana na kuwapo kwa matumizi mabaya ya fedha.
“Kulikuwa na taarifa za utekelezaji zenye mkanganyiko na ubora usioridhisha hivyo kutokana na hali hii Mwenge wa Uhuru uliwataka wahusika wote wawajibishwe kwa mujibu wa taratibu na sheria za nchi,” alisema.
Amour alisema kwamba kutokana na hali hiyo waliiagiza taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) kuanza kuchunguza miradi hiyo kwa kina ili kuwabaini waliohusika.
Rais Magufuli alisema isingekuwa mbio za mwenye utekelezaji hafifu wa miradi hiyo usingebainika jambo linaloongeza umuhimu wake.
Alisema kiuhalisia mbio za mwenge zimekuwa zikiambatana na uzinduzi wa miradi mbalimbali ya maendeleo yenye shabaha ya kukuza utu na ustawi wa Watanzania.
Rais alisema katika kipindi cha miaka mitano iliyopita mwenge huo umezindua miradi 6,838 yenye thamani ya takriban Sh2.51 trilioni.
Aliongeza kuwa mwaka huu umezindua zaidi ya miradi 1,500 yenye thamani ya zaidi ya Sh1.1 trilioni.
Pia, alisema kuwapo kwa viwanda 148 vilivyozinduliwa na mwenge huo kutasaidia kuongeza ajira na hivyo kukuza uchumi wa nchi.
Kuhusu ufisadi
Rais Magufuli alisema Serikali itaendelea kupambana na ufisadi japokuwa wapo Watanzania wasiohusika watakaoathirika na suala hilo ili kuenzi jitihada za Baba wa Taifa zilizosababisha kuanzishwa kwa Azimio la Arusha.
“Mfano umemkamata mwizi wa fedha za umma, kama alikuwa anatumia fedha alizoiba kujenga nyumba yake ni lazima ujenzi wa nyumba hiyo utasimama na ukisimama atakayeathirika sio yeye peke yake, bali hata wajenzi, mama lishe, bodaboda na hata wauza maji,” alisema.
Rais alisema kwa sababu lengo ni kupambana na wizi, athari hizo haziwezi kukwepeka kwa kuwa mabadiliko ya aina yoyote yana athari.
Aliwataka Watanzania kuvumilia kwa sababu athari hazitadumu kwa kipindi kirefu na hata zikidumu, watakaonufaika ni kizazi kijacho.
“Mabadiliko ni magumu mwanzoni, yatakuwa machungu yakifikia katikati lakini mwishoni ni mazuri au matamu. Nawaomba Watanzania tuvumilie kipindi hiki cha mpito baada ya muda mfupi mambo yatakuwa mazuri. Uzalendo ni kujitolea kwa ajili ya wengi na vizazi vijavyo,” alisisitiza.
Awali, Waziri wa Sera, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na Walemavu, Jenista Mhagama alisema mwenge huo ulikimbizwa kwa siku 195 nchi nzima na kwamba, kilele cha maadhimisho hayo mwakani kitakuwa mkoani Tanga.
Alisema mkakati wa Serikali ni kuendelea kutokomeza rushwa na kutilia mkazo sera ya ujenzi wa viwanda nchini.
Maadhimisho hayo yaliambatana na dua iliyosoma na viongozi mbalimbali wa dini.
Baadhi ya viongozi waliohudhuria katika sherehe hizo ni Makamu wa Rais Samia Suluhu Hassan na Waziri Mkuu Majaliwa Kassim.

No comments:

 

ADVERTISE WITH US

AFRICAN FASHION

PLACE YOUR ADS HERE!