Wednesday 11 October 2017

LHRC wataka adhabu ya kifo ifutwe nchini

KITUO cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC) kimeiomba serikali kubadilisha sheria ya adhabu ya kifo na badala yake iweke adhabu mbadala kama vile kifungo vya muda mrefu gerezani.


LHRC imeomba Sheria ya Kanuni za Adhabu Sura ya 16 na Sheria ya Ugaidi ya mwaka 2002 ifutwe ili kuridhia mkataba wa Nyongeza wa Haki za Kiraia na Kisiasa, kama ilivyopendekezwana Mpango wa Kujitathmini wa nchi wanachama wa Umoja wa Mataifa mwaka 2016 ili kuhakikisha utekelezaji wa masuala ya haki za binadamu yanazingatiwa.
Mwito huo umetolewa na Mkurugenzi Mtendaji wa kituo hicho, Dk Hellen Kijo-Bisimba wakati akizungumza na waandishi wa habari, Dar es Salaam jana kuhusu maadhimisho ya Siku ya Kupinga Adhabu ya Kifo Duniani.
Alidai kwa kuwa Rais John Magufuli alishatoa msimamo wake wa kupinga adhabu hiyo, basi ni muda mwafaka wa kuiondoa adhabu hiyo rasmi kwenye sheria nchini ili isije kuja kutekelezwa hata miaka ya baadae.
“Kituo kinampongeza Rais wetu na kitaendelea kumuombea awe na msimamo huo huo, ila sasa ni lazima katika sheria adhabu ya kifo ifutwe kabisa na isiwepo, ila iwepo adhabu mbadala kama kifungo cha muda mrefu,” alisema Kijo- Bisimba.
Alisema, kwa kuwa katika katiba kuna sheria kama vile Sheria ya Kanuni ya Adhabu na Sheria ya Ugaidi inayotoa adhabu ya kifo kwa makosa ya mauaji, uhaini na ugaidi, ambazo zote zinatakiwa kufutwa ili ibakie hukumu isiyodhalilisha utu wa mwanadamu.
Alidai kuwa hadi mwaka juzi watu ambao walitajwa kuwepo magerezani nchini, wakingojea adhabu ya kunyongwa walikuwa 228 huku wengine 244 wanangojea maamuzi ya rufaa zao. Aliiomba serikali kuiondoa adhabu hiyo ya kikatili.
Alisema kaulimbiu ya maadhimisho ya mwaka huu inasema, “Umaskini na Haki ni mchanganyiko hatari,” hivyo serikali na jamii ihakikishe kuwa hata watu wa kipato cha chini ambao wengi wao ndio wanakumbwa na adhabu hiyo, wanaepushwa nayo kwa kuiondoa kabisa ili wapate adhabu nyingine za kawaida.
Bisimba alisema katika juhudi za kulinda na kuimarisha ulinzi wa haki za binadamu, Tanzania imeridhia mikataba mbalimbali ya kikanda na kimataifa, inayoweka wajibu kulinda haki hiyo pamoja na kuipa ulinzi ndani ya sheria za nchi.
Mikataba hiyo ni pamoja na Tamko la Kimataifa la Haki za Binadamu (UDHR) la mwaka 1948, Mkataba wa Haki za Kiraia na Kisiasa (ICCPR) wa mwaka 1966 na Mkataba wa Afrika wa Haki za Binadamu na Haki za Watu wa mwaka 1981.

No comments:

 

ADVERTISE WITH US

AFRICAN FASHION

PLACE YOUR ADS HERE!