RAIS John Magufuli amewaambia wajumbe wa Mkutano Mkuu wa Jumuiya ya Tawala za Mitaa (ALAT) kwamba serikali yake inachofanya sasa ni kuhakikisha inajali maendeleo ya wananchi.
Pia, amesema kwamba madiwani ambao hawaridhiki na kiwango cha posho cha Sh 350,000, wajiuzulu kwa kuwa kwa sasa serikali haiwezi kuongeza kiasi hicho cha fedha. Akifungua Mkutano Mkuu wa 33 wa ALAT Dar es Salaam jana, Rais Magufuli alisema anatambua kazi kubwa inayofanywa na mamlaka za Serikali za Mitaa kwa sababu hata kwenye ukaguzi wa vyeti vya watumishi wa umma, wao ndio waliosaidia kazi hiyo kwenda vizuri na kufanikiwa kwa kuwaondoa watumishi hewa zaidi ya 20,000.
Kwa mujibu wa Rais Magufuli, watumishi hewa walikuwa wanaigharimu serikali Sh bilioni 19.848 kwa mwezi na kwa mwaka Sh bilioni 238.176, wakati wafanyakazi waliokuwa na vyeti feki walikuwa 12,000 na waliigharimu serikali Sh bilioni 11.9 kwa mwezi na kwa mwaka Sh bilioni 142.9, hivyo kwa mwaka gharama iliyokuwa inatumika kuwalipa wenye vyeti feki na wafanyakazi hewa ilikuwa Sh bilioni 381. Mbali na wafanyakazi hewa na wenye vyeti feki, Rais alisema pia zilikuwepo kaya hewa na wanafunzi hewa ambavyo vyote vilikuwa mianya ya kufuja fedha za umma.
Dk Magufuli aliongeza kuwa kulikuwa na kaya hewa 57,000 na wanafunzi hewa 65,000. Rais alisema mifumo hiyo ya kufuja fedha za umma, kwa sasa imedhibitiwa na kuongeza nidhamu na weledi kwenye utumishi wa umma. Kuhusu posho hizo za madiwani, Rais Magufuli aliwakumbusha wajumbe kuwa wakati walipogombea udiwani, walijaza fomu maalumu ambayo moja ya vipengele vilimtaka diwani awe na kazi maalumu ya kumwingizia kipato. Alisema kama wapo madiwani waliojaza fomu hii na hawana kazi ya kuwapatia kipato, wajiuzulu udiwani.
“Ninyi ndio wasimamizi wa miradi, mafanikio tuliyoyapata kwa miezi hii 23, pia yanatokana na mchango wenu. Mlisimamia vizuri suala la madawati, lakini bado kuna changamoto ya upungufu wa madarasa, nyumba za walimu, vyoo, nawaomba mkatatue matatizo haya, himizeni wananchi kuwapeleka watoto shule,” alieleza Rais Magufuli. Rais Magufuli aliwataka wajumbe wa mkutano huo pamoja na wakuu wengine wa mikoa, kujifunza ubunifu alionao Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda namna anavyofanya kazi zake.
Alisema Makonda amekusanya Sh milioni 180 kwa ajili ya shughuli za maendeleo kwenye mkoa wake. Katika mkutano huo, Makonda aliwaomba wajumbe wamchangie mifuko ya saruji. Alisema wananchi wanaposhirikishwa kuchangia mambo ya maendeleo hawana shida, tatizo linakuja kwenye namna fedha hizo zinavyotumika. Aliwataka wakurugenzi, madiwani, mameya na wenyeviti wa halmashauri, kusimamia vyema fedha za wananchi katika kuwaletea maendeleo
No comments:
Post a Comment