Mahakama Kuu Kanda ya Sumbawanga imewahukumu kifungo cha miaka 20 jela, washtakiwa sita kwa makosa ya kula njama na jaribio la kuua mtoto mlemavu wa ngozi (albino).
Akisoma hukumu hiyo jana, Jaji Adam Mambi alisema Mahakama imeridhishwa na ushahidi wa kiungo uliotolewa na upande wa mashtaka uliokuwa na mashahidi 12 wakiwamo daktari na mkemia.
Kiungo hicho kilipelekwa kuchunguzwa vinasaba (DNA) kwa lengo la kuthibitisha iwapo kilikuwa cha mtoto huyo aliyeuawa.
Jaji Mambi alisema washtakiwa hao walithibitika kutenda kosa hilo katika Kijiji cha Msia, wilayani Sumbawanga Februari 15, 2013 kwa kumvamia mtoto Mwigulu Matomange alipokuwa akichunga ng’ombe na kumkata kiungo cha mkono na kutoweka nacho.
Alisema baada ya watuhumiwa hao kutoweka na kiungo hicho, walikamatwa na polisi Aprili 20, 2013 mkoani Tabora wakiwa katika harakati za kutafuta mnunuzi.
Washtakiwa sita kati ya kumi waliofikishwa mahakamani hapo, ambao walikutwa na hatia ni Ignas Sungura, James Paschal, Ibrahim Tela, Faraja Jailos, Weda Mashilingi na Nickson Ngalamila. Walioachiwa ni Kulwa Mashilingi, Peter Said, Hamis Rashid na James Ngalamila waliokuwa wakitetewa na mawakili wanne ambao ni Bartazar Chambi, Charles Kasuku, Peter Kamyalile na Mathias Budodi.
Jaji Mambi alisema Mahakama imejielekeza katika mambo kadhaa ya msingi ili kuthibitisha makosa hayo; iliangalia ushahidi wa mazingira; kitendo cha washitakiwa kukutwa na kiungo cha binadamu wakitafuta soko; na nia ovu ya kutenda kosa na kusababisha maumivu makali au kifo.
Alisema kosa la kula njama ya kuua, adhabu yake ni kifungo cha miaka 14 jela kwa kuzingatia kifungu cha Sheria Namba 215 ya kanuni ya adhabu sura 16, huku kosa la kufanya jaribio la kutaka kuua adhabu yake ni kifungo cha maisha jela.
Hata hivyo, Jaji Mambi alisema Mahakama kwa kuangalia mazingira ya kesi na hoja za upande wa utetezi imewapunguzia adhabu kutoka kifungo cha maisha kwa kosa la pili kuwa kifungo cha miaka 20 huku kosa la kwanza wakitumikia kifungo cha miaka 14 hivyo watatakiwa kutumikia vifungo vyote kwa pamoja.
Awali, Wakili wa Serikali Fadhili Mwandoloma aliitaka mahakama kutoa adhabu kali kwa watuhumiwa hao ili iwe fundisho kwa watu wengine wanaotenda makosa kama hayo.
Nao, mawakili wa upande wa utetezi waliiomba mahakama kupunguza adhabu kwa wateja wao kwa kuwa tayari wamekaa mahabusu kwa zaidi ya miaka minne kitu ambacho ni funzo tosha kwao hivyo hawawezi kurudia kutenda tena makosa hayo.
No comments:
Post a Comment