JESHI la Polisi Kikosi cha Usalama Barabarani, limeanzisha operesheni na doria za kushitukiza, zitakazokuwa endelevu kufanyika mikoa yote nchini. Lengo la opesheni hizo ni kukamata mabasi ya abiria, yasiyozingatia sheria za usalama barabarani muda wa usiku.
Ili kukamilisha mpango huo, polisi watatumia kifaa maalumu cha kunasa mwendokasi maarufu kama tochi za usiku; na madereva watakaokamatwa, watachukuliwa hatua kali za kisheria. Operesheni hiyo ilianza mkoani Arusha juzi na kuendelea jana katika Mkoa wa Morogoro, ikiongozwa na Kamanda wa Kikosi hicho nchini, Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Polisi ( SACP), Fortunatus Musilimu.
Musilimu aliongoza opereshani hiyo usiku wa manane wa kuamkia Septemba 16, mwaka huu katika eneo la Dumila Wilaya ya Kilosa Mkoa wa Morogoro kwenye barabara kuu ya Morogoro- Dodoma.
Katika operesheni hiyo, polisi ilifanikiwa kukamata mabasi zaidi ya sita yaliyokuwa yakisafiri zaidi ya muda wa saa sita usiku huku mengine yakibainika kutembea mwendokasi na kutofuata sheria za barabarani, mengi yakitoka mikoa ya Mwanza, Kagera na Mara.
Kamanda huyo alisema baada ya kudhibitiwa na askari wa kikosi hicho katika muda wa asubuhi hadi jioni, baadhi ya madereva wameanza kufidia mwendo walioopoteza wakati wa usiku kwa kuendesha mwendo kasi, kitendo ambacho kinahatarisha maisha ya abiria na mali zao.
“Katika operesheni hii madereva wote wakaokamatwa kwa makosa ya uvunjifu wa sheria za barabarani muda wa usiku, basi watafutiwa umiliki wa leseni zao na zoezi hili ni endelevu, na doria hizi zitafanyika katika mikoa yote nchini.
“Madereva wanadanyanyika kwa kudhani tochi hizi hazifanyi kazi usiku... hizi ni tochi maalumu na zinafanya kazi nyakati zote mchana na usiku kama leo usiku huu wa saa sita kwenda saa saba tumewanasa madereva wa mabasi wakiwa na mwendeo kasi unaosomeka na namba ya gari lake,” alisema Musilimu.
Kamanda wa Kikosi cha Usalama Barabarani Mkoa wa Morogoro, Boniface Mbao alisema ataendelea kusimamia na kufanya operesheni za usiku na wale watakaokutwa na makosa mbalimbali, watawachukulia sheria kulingana na miongozo na Sheria za Usalama Barabarani.
No comments:
Post a Comment