Sunday, 17 September 2017

Tanzania: Hatuungi mkono nyuklia za Korea Kaskazini

SERIKALI ya Tanzania imekanusha kuwa na uhusiano wa karibu na Jamhuri ya Korea Kaskazini, kama taarifa ya Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa (UN) waliyoipokea Septemba 5, mwaka huu inavyodai.


Hayo yalisemwa Dar es Salaam jana na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Dk Augustine Mahiga alipozungumza na waandishi wa habari. Kwa mujibu wa Dk Mahiga, taarifa hiyo ya Baraza la Usalama la UN, haisemi kuhusu madai ya awali ya kupeperushwa kwa bendera ya Tanzania kwenye meli za Korea Kaskazini, misaada ya hospitali wala mambo ya kidemokrasia ambayo kimsingi yalishafanyiwa kazi na Tanzania, bali inasema madai mapya kuwa Tanzania bado inaendeleza uhusiano na Korea Kaskazini katika baadhi ya mambo, ikiwemo ukarabati na uimarishaji wa vifaa fulani.
Alisema kuwa taarifa hiyo ya Baraza la Usalama la UN, imepitwa na wakati na Serikali itaijibu. Alisema wakati mwingine taarifa kama hizo zinazoandaliwa na wataalamu wao, huchelewa kulifikia Baraza hilo hata kwa miezi 12 au 18.
Aliongeza kuwa Tanzania haiungi mkono nchi yoyote, kutengeneza na kuzifanyia majaribio silaha za maangamizi ikiwemo nyuklia. “Sisi hatuna uhusiano wa kihivyo na Korea Kaskazini.
Tumeshachukua hatua kupunguza uhusiano wa kidemokrasia na Korea Kaskazini, kuhakikisha bendera yetu haipeperushwi tena na tunaungana na Jumuiya ya Kimataifa kulaani vitendo vinavyofanywa na Korea Kaskazini vya kutengeneza silaha za maangamizi na kuzifanyia majaribio, kwa kuwa tishio hilo ni la watu wote kwa kutambua madhara ya nyuklia,” alisema Waziri Mahiga.
Alisema Tanzania imetakiwa kutoa taarifa inayolingana na hali halisi, kuthibitisha kama wataalamu hao kutoka Korea Kaskazini bado wapo nchini, jambo ambalo linaonesha kuwa hata Baraza hilo la Usalama halina taarifa mpya (up todate).
Alisema taarifa hizo zote, zitawafikia kabla ya yeye kwenda huko. Mahiga alisema kuwa Tanzania ni miongoni mwa nchi 11, zilizotajwa kuwa na uhusiano wa karibu na Korea Kaskazini na kwa uhusiano huo, inakwenda kinyume na uamuzi wa Baraza la Usalama la UN ya kuiwekea Korea Kaskazini vikwazo vya kisiasa, kidiplomasia, kiuchumi, kisiasa, kijeshi na mawasiliano.
Alisema Tanzania haina ugomvi na Korea Kaskazini, lakini kitendo chao cha kutengeneza na kuzifanyia majaribio silaha hizo ni kinyume cha heshima ya ustaarabu na usalama duniani, ndiyo maana hatua za kupunguza uhusiano nao na kuunga mkono vikwazo walivyowekewa vianze kuwabana.
Kwa mujibu wa Mahiga, Tanzania ilikuwa na uhusiano wa kibiashara na kampuni za Korea Kaskazini, lakini si Serikali ya Korea Kaskazini. Alisema uhusiano huo wa Tanzania na kampuni hizo za Korea Kaskazini, ulikuwa katika kusaidia vitu fulani kwa ajili ya ulinzi na usalama wa jeshi, jambo ambalo pia Baraza la Usalama walitaka liachwe mara moja.
Alisema katika kuitikia mwito huo, Serikali ilitengeneza utaratibu wa kuondoa uhusiano wa kijeshi na Korea Kaskazini na tarehe ambayo Serikali iliiweka katika kutekeleza hilo ni mwaka 2014. “Nimewaita wawakilishi wakubwa wa kudumu wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa na kuwaeleza kuwa taarifa hiyo si sahihi.
Kuna magazeti mengine yanashabikia taarifa hiyo, lakini kesho nitakwenda Umoja wa Mataifa kwenye mkutano wa kila mwaka wa Umoja huo ambako pia nitawapa majibu haya haya ninayowapa ninyi,” alieleza Mahiga.
Kuhusu uhusiano wa Tanzania na Korea Kusini, Mahiga alisema kuwa uhusiano kati ya nchi hizo mbili ni mkubwa na Korea Kusini imeichagua Tanzania kuwa ni nchi itakayopata misaada mingi kutoka huko miongoni mwa nchi za Bara la Afrika.

No comments:

 

ADVERTISE WITH US

AFRICAN FASHION

PLACE YOUR ADS HERE!