Sunday, 24 September 2017

Rais ‘amwaga’ ajira 3,000 JWTZ, kuhamia Dodoma


RAIS John Magufuli amesisitiza azma yake ya kujenga Tanzania mpya, kwa kutangaza ajira 3,000 katika Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ), ujenzi wa reli ya kisasa ya umeme kipande cha Morogoro hadi Dodoma na yeye kuhamia Dodoma mwakani.

Alisema hayo kwenye Uwanja wa Sheikh Amri Abeid jijini Arusha jana, baada ya kutunuku Kamisheni kwa Maafisa Wanafunzi wapya 422 wa jeshi wa cheo cha Luteni Usu wa Kundi la 61/16. Miongoni mwa maafisa haowapya, 32 ni wanawake na wanaume ni 390. Wanafunzi waliotunukiwa vyeo hivyo, wanatoka Shule ya Anga, Shule ya Ubaharia na Chuo cha Kijeshi cha Monduli. Baada ya kutunukiwa vyeo vipya, maafisa hao wapya walivaa vyeo hivyo, kisha kutoa salamu huku wananchi, ndugu, jamaa na marafiki wakishangilia kwa nguvu.

Pia, walikula kiapo cha utii mbele ya Rais Magufuli na baada ya hapo ofisa mpya, Sikujua Peter alivalishwa bawa kwa niaba ya marubani wenzake. Awali, Rais Magufuli alitoa zawadi kwa mwanafunzi aliyefanya vizuri Shule ya Kijeshi ya Kibaharia, Jacob Soka, waliofanya vizuri darasani ni Ally Kitawala na Hamza Msuya, huku Benjamin Fanuel alipata zawadi kutokana na kufanya vyema katika masuala ya urukaji katika anga. Waliofanya vizuri zaidi katika Shule ya Kijeshi ya Monduli ni Hamis Mwantega, aliyefanya vizuri darasani ni Haji Kimaro.

Wanafunzi hao waliotunukiwa vyeo hivyo vipya, walipita mbele ya Rais kwa gwaride la mwendo wa pole na kasi, huku wakishangiliwa na watu mbalimbali waliofika uwanjani hapo kushuhudia kutunukiwa kwa kamisheni zao. Ajira mpya jeshini Rais alieleza kuwa amefurahi kutoa kamisheni kwa maafisa hao wapya 422, lakini pia jeshi ni lazima liwe pia na wanajeshi wa kawaida.

“Kwa kutambua hilo natangaza rasmi nafasi 3,000 za kuajiri wanajeshi wapya. Na hao watakaoajiriwa wawe wamemaliza Jeshi la Kujenga Taifa (JKT). Lengo ni tuwe na maaskari wa kutosha na jeshi la kisasa zaidi,” alisema Rais Magufuli, ambaye ni Amiri Jeshi Mkuu. Alipongeza JWTZ, Polisi, Zimamoto, Uhamiaji, Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (PCCB) na vyombo vingine vya ulinzi na usalama, kwa kazi nzuri ya kulinda amani ya nchi. Alitaka wananchi kuendelea kuunga mkono vyombo hivyo.

Kuhusu suala la ajira, Rais alisema katika mwaka huu wa fedha, serikali inatarajia kuajiri jumla ya watumishi 50,000 wa sekta mbalimbali, ikiwemo wanajeshi, madaktari na walimu. Kuhamia Dodoma Rais alisema uamuzi wa kuhamia Dodoma kutoka Dar es Salaam, ulitolewa na Serikali ya Awamu ya Kwanza ya Mwalimu Julius Nyerere mwaka 1973, lakini kwamba tangu wakati huo utekelezaji wake ulikuwa mgumu. Lakini, alisema serikali yake imedhamiria kuhamia Dodoma na kwamba hadi sasa watumishi 3,000 wamehamia Dodoma akiwemo Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa.

Alitangaza kuwa Makamu wa Rais, Samia Suluhu Hassan atahamia baadaye mwaka huu na yeye mwaka kesho. “Mwaka huu atahamia Makamu wa Rais na mwaka kesho nahamia mimi. Yule ambaye hatahamia huko na kukaa Dar kazi hana,” alisema Mkuu huyo wa Nchi. Ndege, reli ya umeme Rais alisema hatua mbalimbali ambazo Serikali ya Awamu ya Tano, imechukua kudhibiti matumizi ya serikali, zimeiwezesha kupata fedha za kutosha, hivyo kuiwezesha kujenga miradi mikubwa mbalimbali, mfano kununua ndege za kisasa sita, zitakazoboresha usafiri wa abiria wa kawaida na watalii.

Mradi mwingine ni ujenzi wa reli ya kisasa ya umeme (standard gauge). “Tumeanza kujenga reli ya kisasa kilometa 300 kutoka Dar hadi Morogoro. Na wiki ijayo tunatarajia mkataba mwingine mpya utasainiwa kwa ajili ya ujenzi wa kipande cha reli kutoka Morogoro kwenda Dodoma,” alitangaza. Madeni ya wanajeshi Rais Magufuli alisema juzi alikutana na Mkuu wa Majeshi, Jenerali Venance Mabeyo na makamanda wa juu jeshini, kujadili madeni na maslahi mbalimbali ya wanajeshi, ambapo walikubaliana wataanza kulipa madeni hayo kuanzia wiki ijayo.

Umeme Bonde la Rufiji Magufuli alisema serikali yake itatimiza ndoto ya Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere ya mwaka 1975, ambapo alitaka kujenga bwawa la kufua umeme la Stiegler’s Gorge katika Bonde la Mto Rufiji mkoani Pwani, kwa lengo la kuondoa kero ya umeme nchini. Alisema mradi huo wa Stiegler, utazalisha megawati 2,100 za umeme na kumaliza tatizo la umeme nchini. Alisema umeme unaozalishwa nchini kwa sasa ni megawati 1,460 tu ambazo hazitoshi, hasa wakati huu serikali inajenga uchumi wa viwanda na kukaribisha wawekezaji mbalimbali.

“Tumetangaza tenda ya kujenga Stieglers na tayari makampuni 50 ya kimataifa yameomba tenda hiyo,” alisema Rais na kuongeza kuwa fedha za kutekeleza mradi huo mkubwa zipo. Uchumi wapaa Rais alisema uchumi wa Tanzania unakua kwa kasi na Tanzania ni moja ya nchi tatu barani Afrika, zinazoongoza kwa uchumi kukua, ya kwanza ikiwa ni Ethiopia.

Uchumi wa Ethiopia unakua kwa asilimia 8, wakati wa Tanzania unakua kwa asilimia 7.1 na mwakani utakua kwa asilimia 7.2 sawa na wa India. Urais mateso Magufuli alisema urais ni msalaba, kazi ngumu mno na ya kujitoa msalaba. Alisema yeye amejitoa sadaka ili kunyoosha nchi na mafisadi. “Urais ni mateso. Ni shida kubwa kuwa Rais. Nayaona mateso.

Niliomba urais kwa kujaribu, nikasukumiziwa huko, hata hivyo nimejitoa sadaka kwa ajili ya nchi yangu na Watanzania,” alisema. Alisisitiza, “Niliingia bila kutoa rushwa. Hakuna aliyenichangia wakati nagombea urais, hivyo nitaendelea kunyoosha nchi. Hili la kutumbua, watu watatumbuka kweli kweli, nataka mafisadi watubu, nataka Tanzania mpya.” Mialiko safari za nje Rais alisema amepata jumla ya mialiko 60 ya kwenda nje ya nchi, lakini hakwenda, kwa sababu bado anasafisha nchi. “Nimeacha mialiko 60. Wengi tu wanaomba uje.

Nije kufanya nini? Nasafisha kwanza nyumba yangu. Niliomba urais si wa kutembelea nchi nyingi. Kwanza mimi nilishatembelea nchi nyingi kabla sijawa rais. Huu sasa ni wakati wangu wa kuchapa kazi,” alisema Rais. Viongozi walioshuhudia wanajeshi hao wapya wakitunukiwa vyeo ni Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa, Jaji Mkuu mstaafu, Augustino Ramadhani, Katibu Mkuu Kiongozi, Balozi John Kijazi, Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa (JKT), Hussein Mwinyi, Mbunge wa Ngorongoro William ole Nasha, Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Mrisho Gambo, wakuu wa wilaya za Arusha, wakurugenzi wa wilaya.

No comments:

 

ADVERTISE WITH US

AFRICAN FASHION

PLACE YOUR ADS HERE!