Monday, 11 September 2017

'Nilichelewa kuteua jaji mkuu kwa kuwa sikutaka mla rushwa'

RAIS John Magufuli amefichua siri ya kumteua Profesa Ibrahim Juma kuwa Kaimu Jaji Mkuu Januari 18, mwaka huu, na kubainisha kuwa alichukua hatua hiyo, kwa kuwa hakuwa na historia ya kutosha kuhusu sifa za majaji waliopo nchini.


Aidha, ameelezea kuridhishwa na sifa za Profesa Juma na hivyo kumteua kuwa Jaji Mkuu, huku akimtaka kuhakikisha vyombo vya Mahakama vinashughulikia ipasavyo kesi zote za rushwa na ufisadi nchini.
Pamoja na hayo, kwa upande wake, Jaji Juma, alianika mikakati yake ya kuboresha sekta ya Mahakama nchini ikiwa ni pamoja na kuboresha majengo ya Mahakama nchi nzima na Mahakama kuanza kutumia Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA) na uendeshwaji na utolewaji maamuzi ya kesi kwa uwazi.
Akizungumza Ikulu Dar es Salaam jana katika hafla ya kumuapisha rasmi Jaji Juma kuwa Jaji Mkuu wa Tanzania, Dk Magufuli alisema kazi ya Jaji Mkuu ni nyeti hivyo uteuzi wake unahitaji umakini ili kuteua Jaji ambaye ataleta mapinduzi ya kweli katika eneo la haki kwa watanzania.
“Nilipoingia madarakani ilikuwa ni kipindi kidogo tu Jaji Mkuu aliyekuwepo Othman Chande alistaafu, sikuwa na historia ya majaji wengi, nikaona nijipe muda kwanza na kuamua kutumia kifungu cha Katiba kilichopo kinachoniruhusu kuteua Kaimu Jaji Mkuu,” alieleza.
Alisema katika kipindi hicho hakutaka kuteua jaji ambaye baada ya miaka miwili au mitatu, analazimika kuteua jaji mwingine au jaji aliyepo baada ya muda mfupi anastaafu.
“Nilitaka kuteua jaji mwenye sifa ninazozitaka ambaye anaweza kushika nafasi hiyo hata kwa miaka 10,” Pamoja na hayo, Rais Magufuli alisema alitumia muda mwingi kuchekecha aina na sifa ya Jaji Mkuu anayemtaka ikiwemo namna anavyolichukulia suala zima la rushwa kutokana na ukweli kuwa tatizo la rushwa nchini bado ni kubwa na kila mahali lipo.
Alisema hata baada ya kuchaguliwa na watanzania kuwa rais wao, alikuwa akimuomba Mungu kila siku ampatie kiongozi ambaye atamsaidia kulisimamia tatizo hilo la rushwa ipasavyo.
Alisema na katika kuhakikisha anapata mtu mwenye sifa hizo, na katika uchambuzi wake wa majaji waliopo nchini, Profesa Juma alimuidhinisha kuwa na sifa hizo ikiwemo uwezo na weledi wake katika utendaji.

No comments:

 

ADVERTISE WITH US

AFRICAN FASHION

PLACE YOUR ADS HERE!