RAIS Yoweri Museveni (pichani) amepinga kuingizwa kwa nguo zilizotumika maarufu kama mitumba nchini Uganda kwa kuwa unadumaza maendeleo ya sekta ya nguo. “Mitumba inaua sekta ya nguo Uganda.
Uendelezaji wa viwanda kwenye hii sekta una manufaa si tu kwa Uganda, lakini pia kwa Marekani. Kama washirika kunakuwa na ongezeko la kiwango cha biashara na kuongeza mapato,” alisema Rais Museveni jijini New York wakati akizungumza na Waziri Mdogo wa masuala ya Siasa wa Marekani, Thomas Shannon.
Alisema, wakati Uganda na Marekani zinashirikiana kutatua changamoto za kiusalama katika nchi za Somalia, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC) na Sudan Kusini, ni muhimu kwa taifa hilo lenye nguvu kubwa kiuchumi kuyafanyia kazi maeneo yenye uhalisia ukiwemo uwekezaji na biashara kwa kuwa yanachangia amani kwenye nchi hizo. Rais Museveni alikwenda Marekani kuhudhuria Mkutano wa 72 wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa.
Mkutano wa Museveni na Shannon ulihudhuriwa na Waziri wa Mambo ya Nje wa Uganda, Sam Kutesa na Mkuu wa Majeshi wa Uganda, Jenerali David Muhoozi. Kiongozi huyo wa Uganda aliunga mkono kauli ya Rais Donald Trump wa Marekani kwa viongozi wakuu wa nchi kwamba wanapaswa kujali maslahi ya nchi zao kwanza. Kwa mujibu wa Rais Museveni, siku za nyuma Marekani ilipoteza muda mwingi kwenye vitu visivyo na manufaa badala ya kuhimiza maslahi ya pande zote kwenye biashara na uwekezaji.
No comments:
Post a Comment