WIZARA ya Afya ya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar (SMZ), imesema watu 6,500 wapo katika hatari ya kupata matatizo ya upofu wa macho baada ya kushindwa kupata matibabu kwa wakati.
Hayo yalisemwa na Waziri wa Afya, Mahmoud Thabit Kombo wakati akizindua kambi ya macho iliyotayarishwa kwa pamoja na Chuo Kikuu cha Tunguu Zanzibar. Kombo alisema watu 3,500 wanaweza kupona katika matatizo yanayowakabili ya macho kama watapata matibabu kwa wakati. “Maradhi ya macho siyo moja ya tatizo kubwa la afya ya wananchi, lakini tunawataka wajitokeze mapema na kuchunguzwa afya zao ili kupata matibabu sahihi kwa wakati,” alisema.
Alifahamisha kwamba SMZ kwa kushirikiana na taasisi mbalimbali binafsi itaendelea kutoa huduma za afya bila ya malipo ikiwa ni sehemu ya utekelezaji wa sera ya serikali. Matibabu ya macho kwa wananchi wa Wilaya ya Kati jimbo la Tunguu yameishirikisha Wizara ya Afya pamoja na Chuo kikuu cha Tunguu kwa kuleta madaktari bingwa kutoka India na Pakistan.
Mkuu wa Chuo cha Tunguu, Professa Mustafa Roshashi alisema wameamua kuunga mkono na kushirikiana na serikali katika kuimarisha na kutoa huduma za afya za macho kwa wananchi. Zaidi ya wananchi 5,000 walijitokeza kuchunguzwa afya zao huku wengine wakiahidiwa kufanyiwa upasuaji katika Hospitali ya Jeshi iliopo Bububu mjini Unguja.
No comments:
Post a Comment