Thursday 31 August 2017

SABABU YA EID-AL-ADHA KUITWA 'SIKUKUU YA KUCHINJA'





Na Jumia Travel Tanzania

Eid al-Adha ni miongoni mwa sikukuu kubwa kwa waumini wa dini ya Kiislamu ukiachana na Eid- al-Fitr inayosherehekewa kila mwaka duniani kote. Kwa mwaka huu sikukuu hii inatarajiwa kusherehekewa siku ya Ijumaa ya Septemba mosi ambapo kwa waumini wa dini hiyo ni kipindi cha kujitolea, kuonyesha ukarimu kwa marafiki, familia na watu wenye uhitaji.




Kama zilivyo sikukuu nyingine kuna baadhi ya watu huwa hawajui ni kwa nini huwa zinaseherehekewa namna zinavyosherehekewa. Jumia Travel kupitia makala haya imekukusanyia mambo ya msingi kuhusu maana ya sikukuu hii na namna ya kusherehekea.


Waislamu huisherekea sikukuu ya Eid al-Adha kwa kuchinja mnyama ikiwa ni kuheshimu kitendo alichokifanya Ibrahim au Abraham (anavyoitwa na Wakristu na Wayahudi). Ibrahim aliamriwa na Mungu kumtoa mtoto wake pekee kiume kama sadaka kwa kumchinja ambapo alikubali kutii amri hiyo bila ya kupinga. Kabla ya kumtoa sadaka mtoto wake sadaka, Mungu aliingilia kati kwa kumtuma Malaika wake ambaye altaka amchinje kondoo badala ya mtoto wake.

Katika kuadhimisha tukio hilo kubwa la kiimani, kila mwaka sikukuu hii inaposherehekewa waumini wa Kiislamu huchinja mnyama halali kwa mujibu wa imani. Mnyama huyo anaweza kuwa ni ng’ombe, ngamia, mbuzi au kondoo inategemea na uwezo wa mtu. Baada ya kuchinja, nyama hugawanywa katika mafungu matatu ambapo la kwanza hubakia kwa familia; la pili hugawiwa kwa ndugu, jamaa na marafiki; na kisha la tatu hugawiwa kwa watu masikini na wenye uhitaji.
Hivyo basi sikukuu hii husherehekewa kama ni ishara ya kukumbuka utiifu wa Ibrahim mbele ya Mungu lakini pia huashiria tamati ya safari ya Hijja. Kila mwaka Waislamu wote duniani huenda kuhiji mjini Macca uliopo nchini Saudi Arabia. Eid al-Adha ni tofauti na Eid al-Fitr ambayo yenyewe husherehekewa baada ya kuisha kwa mfungo mtukufu wa mwezi wa Ramadhan.

Katika kalenda ya mwezi wa Kiislamu, sikukuu ya Eid al-Adha hutukia siku ya 10 ya mwezi wa 12 na hudumu kwa muda wa siku nne mpaka siku ya 13. Kwa mwaka huu itaanza siku ya Ijumaa ya Septemba mosi na kufikia ukomo siku ya Jumanne ya Septemba 5. Maadhimisho ya sikukuu hii hubailika kila mwaka kulingana na mabadiliko ya kalenda, hivyo haimaanishi mwaka ujao sherehe zitaangukia tarehe sawa na za mwaka huu.
Kama ilivyo kwa Eid al-Fitr, Waislamu huanza kusherehekea Eid al-Adha asubuhi kwa kwenda msikitini kwa ajili ya sala, kusikiliza mawaidha kisha kufuatiwa na kutakiana heri ya sikukuu pamoja na kugawiana zawadi. Baada ya hapo wanyama huchinjwa ikiwa ni sehemu ya sherehe na kisha nyama hugawiwa kwa ndugu, jamaa na marafiki ikiwemo masikini na watu wasio na uwezo. Lakini pia watu wenye uwezo huwagawia pesa watu masikini na wasio na uwezo ili nao waweze kusherehekea kwa furaha kama watu wengine.
Kwa mfano, kwenye mitaa mbalimbali ya jiji la Dar es Salaam ni rahisi kugundua kwamba ni sikukuu kutokana na shamrashamra zinavyoonekana. Mitaa, maduka, migahawa, sehemu za kutembelea kama vile fukwe ya bahari ya Hindi hufurika watu wakifanya manunuzi, kula chakula na kufurahia kwani mara nyingi huwa ni mapumziko ya kitaifa. Jumia Travel inaamini kwamba utakuwa umeelewa ni nini maana ya Eid al-Adha na namna inavyosherehekewa ili kutopoteza maana yake. 

No comments:

 

ADVERTISE WITH US

AFRICAN FASHION

PLACE YOUR ADS HERE!