MKEMIA kutoka Ofi si ya Mkemia Mkuu wa Serikali, Dominician Dominic (42) ameieleza Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, matokeo ya uchunguzi kuhusu sampuli ya mkojo wa mfanyabiashara Yusuf Manji.
Alisema matokeo hayo yalionesha kwamba alikutwa na kemikali aina ya benzodiazepines na morphine ambazo hutumika hospitalini kwa ajili ya kupunguza maumivu makali na kumsaidia mgonjwa kupata usingizi.
Aidha, shahidi huyo wa tatu wa upande wa mashitaka alishindwa kuthibitisha kama kweli mkojo huo ni wa Manji au Polisi kwa kuwa alidai hakuwepo wakati sampuli hiyo inatolewa.
Akiongozwa na Wakili wa Serikali, Timon Vitalis, shahidi huyo alidai mbele ya Hakimu Mfawidhi, Cyprian Mkeha kuwa Februari 9, mwaka huu majira ya saa 5 asubuhi alipokea askari akiwa na watuhumiwa wawili kwa ajili ya kutoa sampuli ili kupima mkojo.
Wakili Vitalis: Je, unakumbuka watuhumiwa waliokuja ofisini hapo kwa majina yao na askari aliyewaleta? Shahidi: Ndio, watuhumiwa waliofikishwa ofisini hapo ni Mchungaji Gwajima na Manji ambao waliletwa na Koplo Sospeter mwenye namba E 1135.
Wakili: Jinsi gani ulianza kufanya uchunguzi? Shahidi: Kuna maliwato maalumu ambayo askari anaingia na mtuhumiwa kutoa sampuli ambapo nilimpatia kontena niliyoipa namba ya maabara 367/2017 ambayo sampuli hii ilikuwa ya Manji.
Wakili: Je, kuna chochote kiliwasilishwa kwako na nani aliwasilisha fomu namba 001? Shahidi: Sampuli iliwasilishwa na fomu maalumu kwa mujibu wa sheria ya dawa za kulevya ambayo Koplo Sospeter ndiye aliyeiwasilisha.
Wakili: Je, ukiiona fomu hiyo utaweza kuitambua? Pia uieleze mahakama baada ya kuchukua sampuli ya mkojo ulifanya nini? Shahidi: Fomu hiyo naweza kuitambua kwa kuwa ina saini yangu na jina la mtuhumiwa aliyeletwa kwa ajili ya uchunguzi, pia naomba ipokelewe kama ushahidi katika kesi hii.
“Nilifanya uchunguzi wa awali kwa kutumia kifaa kinachoitwa ‘Diaquicky multipanel urine test’ na matokeo yalionesha kuwa mkojo ulikuwa na kemikali inayoitwa benzodiazepines.
Kuwepo kwa dawa hizi wakati mwingine hutumika kupunguza maumivu na matumizi mengine kulingana na daktari anavyosema,” alidai Dominic. Wakili: Baada ya hatua ya kwanza ulifanya nini kwa hatua ya pili kuthibitisha dawa hizo?
Shahidi: Kemikali hizi zipo za aina nyingi lakini ili kupata majibu kama kweli anatumia dawa za kulevya nilichukua kemikali hiyo na kuunganisha na dawa za kulevya kulinganisha. Katika sampuli hii niligundua kwamba mkojo una kemikali aina ya morphine.
Alidai kemikali hiyo ya morphine ilikuwa ndani yake na chembechembe ya dawa za kulevya aina ya heroine. Dawa hii pia hutumika hata wakati wa upasuaji hospitalini. Akiulizwa maswali na Wakili wa utetezi Ndusyepo ambaye alimuhoji shahidi huyo kueleza kama mkojo ni wa Manji au Polisi?
Shahidi: Sijui kama mkojo ni wa Manji au Polisi kwa sababu sikwenda nao maliwatoni wakati wa kutoa sampuli ila nililetewa sampuli na Polisi, nilikuwa nje. Wakili Ndusyepo: Ulitumia sampuli kiasi gani kufanya uchunguzi hatua ya pili?
Shahidi: Sampuli inayohitajika ni ujazo wa milimita 10. Wakili Ndusyepo: Unafahamu kama benzodiazepines na morphine zinatolewa na madaktari na hutumika kupunguza maumivu makali na kumpatia mtu usingizi?
Shahidi: Ndio, nafahamu zinatolewa na madaktari pia unaweza kununua katika maduka ya dawa na pia zinaweza kupatikana kinyume na taratibu. Dawa hizi zinaweza kutumika kupunguza maumivu na kumpatia usingizi mgonjwa kwani hazijakatazwa kutumika na hazijaorodheshwa katika kundi la dawa za kulevya.
Kemikali ya morphine pia inaweza kutumika kupunguza maumivu na kuwepo kwa narcotic kwenye mkojo huenda wakati fulani alitumia dawa za kulevya aina ya heroin au la siwezi kujua. Wakili Ndusyepo: Kwa uzoefu wako kemikali ya benzodiazepines zinakuwaje?
Shahidi: Kwa uzoefu wangu kemikali hizi pia hutumika na heroin. Hata hivyo, Wakili wa Serikali, Vitalis waliomba mahakama kufunga ushahidi wake kwamba hawana mashahidi wengine zaidi. Hakimu Mkeha alisema kesi hiyo ilipangwa kusikilizwa mfululizo na kwamba Ijumaa wiki hii, mahakama itatoa uamuzi kama mshitakiwa ana kesi ya kujibu au la.
No comments:
Post a Comment