Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu leo August 9, 2017 imeukatilia upande wa Serikali kutaka Mfanyabiashara Yusuf Manji ahojiwe na Mamlaka ya Mapato Tanzania, TRA kuhusu masuala ya kodi.
Maombi ya kutaka Manji ahojiwe na TRA, yamewasilishwa mbele ya Hakimu Mfawidhi, Cyprian Mkeha na Wakili wa Serikali Mwandamizi, Kishenyi Mutalemwa ambaye amedai wanaiomba Mahakamani itoe kibali ili Manji ahojiwe kisha atarudisha ndani ya muda wa kazi kabla haujaisha.
Hata hivyo, Wakili anayemtetea Manji, Alex Mgongolwa amedai ombi hilo sio sahihi kwa kuwa walikwishafanya mawasiliano ya maandishi na TRA na kusema kuwa wapo Mawakili wa Manji wanaoshughulika na masuala ya kodi na siyo wao hivyo anahitaji kuwasiliana nao ili mahojiano hayo yawe na manufaa.
Kutokana na hatua hiyo, Kishenyi amedai anayehitajiwa ni Manji siyo Makampuni yake na kwamba akifika huko na kuona ipo haja ya kuwa na wataalam wake atasema.
Hakimu Mkeha amesema hawezi kuruhusu ombi hilo kwa sababu kesi iliyopo mbele yake ni ya uhujumu uchumi ambayo haihusiani na masuala ya kodi hivyo ameahirisha kesi hadi August 18, 2017 kwa ajili ya kutajwa.
No comments:
Post a Comment