Historia ya Kiswahili imeanza takriban miaka 1000 iliyopita kwenye pwani ya Afrika ya Mashariki.
Neno Swahili lina asili ya Kiarabu: Sahil ina maana ya pwani; sawahil ’’as-sawāhilī’’ ni wingi wake kwa kumaanisha yote yanayohusiana na pwani, watu au utamaduni wa eneo la pwani.
Mwanzo katika miji ya pwani
Kiswahili kilianza kama lugha ya miji na mabandari ya biashara ya kimataifa kwenye pwani ya Afrika ya mashariki.
Tuna historia jinsi gani miji kama vile Kilwa, Lamu na mingine kadhaa ilianzishwa na wafanyabiashara Waarabu au Wajemi waliooa wenyeji. Idadi ya wahamiaji kutoka Uarabuni haikuwa kubwa sana, hivyo lugha ya wenyeji ilitumika kila mahali ila tu maneno mengi yameingia kutoka Kiarabu. Kwa ujumla Kiswahili kina maneno yenye asili ya Kiarabu kati ya 30-40%, hali inayokaribia kiasi cha maneno yenye asili ya Kilatini au Kifaransa katika lugha ya Kiingereza.
Utamaduni mpya ulijitokeza uliokuwa wa Kiafrika na wa Kiislamu ukajielewa kuwa sehemu ya dunia ya Uislamu. Hivyo Kiswahili kilizaliwa kuwa lugha ya Kibantukilichopokea maneno mengi ya asili ya nje.
Lugha iliandikwa kwa herufi za Kiarabu tangu karne ya 13 BK. Kwa bahati mbaya leo hatuna tena maandiko ya kale sana, kutokana na hali ya hewa kwenye pwani isiyosaidia kutunza karatasi na kurasa zenyewe zinaweza kuoza kutokana na unyevu hewani pamoja na wadudu wengi walioko katika mazingira ya pwani.
Lakini maandiko ya kale yanayopatikana kutoka karne ya 17 huonyesha ya kwamba tenzi na mashairi vinafuata muundo uliotangulia maandiko yenyewe kwa karne kadhaa. Sehemu kubwa ya maandiko ya kale ni tenzi yaani mashairi yenye aya maelfu. Tenzi ndefu kabisa inahusu kifo cha Mtume Muhamad ikiwa na aya 45,000.
Kiswahili kimepokelewa kirahisi na wenyeji kwa sababu walikosa lugha ya pamoja kati yao, lugha za Kibantu ziko karibu sana na athira ya Kiarabu ilikuwa kilekile kote pwani. Haya yote yalisaidia kujenga umoja wa Kiswahili katika eneo kubwa la pwani ya Afrika ya Mashariki.
Kufika kwa Wareno huko Afrika ya Mashariki kuanzia mwaka 1500 kulileta athira mpya ikiwa maneno kadhaa ya Kireno yameingia katika Kiswahili kama vile "bendera", "gereza" na "meza".
Kuwepo kwa wafanyabiashara Wahindi katika miji mikubwa ya pwani kuliingiza pia maneno ya asili ya Kihindikatika lugha kama vile "lakhi", "gunia" n.k. Athira ya lugha za Kihindi iliongezeka kiasi baada ya Waingereza kutumia Wahindi wengi kujenga reli ya Uganda.
Lugha ya biashara
Kiswahili kilitumika kama lugha ya biashara baina ya watu wa pwani na bara katika kanda ndefu sana kutoka Somalia hadi Msumbiji wa Kaskazini. Wafanyabiashara Waswahili waliendeleza biashara ya misafara hadi Kongo.
Kiswahili kiliendelea kuenea kwenye njia za misafara hii. Kila msafara ulihitaji watu mamia hadi maelfu wa kubeba mizigo ya biashara kutoka pwani hadi pale msafara ulipolenga hata Ziwa Tanganyika. Watu hawa wote walisambaza matumizi ya Kiswahili katika sehemu za ndani.
Lakini katika maeneo fulani biashara hii ilijenga pia kizuizi. Watu kama Waganda waliona Kiswahili ni lugha ya Waislamu tena lugha ya biashara ya watumwa; hivyo hadi leo ni wagumu kukubali Kiswahili.
Kiswahili wakati wa ukoloni
Karne ya 19 ilileta utawala wa kikoloni. Wakoloni walitangulia kufika katika mabandari ya pwani wakatumia mara nyingi makarani, askari na watumishi kutoka eneo la pwani wakijenga vituo vyao barani. Watu hao walipeleka Kiswahili pande za bara.
Wajerumani waliamua kutumia Kiswahili kama lugha ya utawala katika Afrika ya Mashariki ya Kijerumani. Hapo waliweza kutumia kazi ya wamisionari Wakristo wa awali, hasa Ludwig Krapf, waliowahi kufanya utafiti wa lugha na kutunga kamusi na sarufi za kwanza pamoja na kuunda mfumo wa kuandika Kiswahili kwa herufi za Kilatini.
Utawala wa kikoloni ulirahisisha mawasiliano kati ya wenyeji. Reli zilijengwa na wafanyakazi kutoka makabila mbalimbali walishirikiana. Waafrika walilazimishwa kulipa kodi kwa wakoloni, hivyo walitafuta kazi ya ajira. Hasa katika mashamba makubwa yaliyolima mazao ya biashara pia katika migodi ya Kongo watu wa makabila mengi walichanganyikana wakitumia hasa Kiswahili kati yao. Kwa namna hiyo lugha ilienea zaidi.
Waingereza baada ya kuchukua Tanganyika kutoka kwa Wajerumani waliendela kutumia Kiswahili kama lugha ya utawala. Kuanzia mwaka 1930 waliunda kamatiyenye shabaha ya kuunganisha lahaja mbalimbali na kuunda Kiswahili cha pamoja kwa ajili ya Afrika ya Mashariki (Inter-territorial Language (Swahili) committee for the East African Dependencies). Mwenyekiti alikuwa Frederick Johnson, makatibu R. K. Watts, P. Mzaba na Seyyid Majid Khalid Barghash. Kamati hiyo iliamua kutumia lahaja ya Kiunguja kuwa msingi wa Kiswahili cha pamoja kilichoendela kufundishwa shuleni. Leo hii ni Kiswahili rasmi kinachofunzwa na wanafunzi na kuandikwa magazetini na vitabuni.
Miaka ya ukoloni ilisababisha pia kupokelewa kwa maneno mapya katika Kiswahili. Kijerumani kiliacha maneno machache kama "shule" (Kijerumani Schule) na "hela" (Heller) lakini maneno mengi sana ya asili ya Kiingereza yalipokelewa.
Kiswahili kimeonyesha uwezo mkubwa wa kupokea maneno kutoka lugha tofauti sana, kikitumia maneno haya kufuatana na sarufi ya Kibantu ya Kiswahili.
Kiswahili leo
Katika Tanzania Kiswahili kimekuwa lugha rasmi ya serikali na taifa. Shule za msingi hutumia Kiswahili lakini shule za sekondari na vyuo bado zinaendelea kufundisha kwa Kiingereza. Tarehe 15 Februari 2015 rais Jakaya Kikwete alitangaza mpango wa kubadilisha lugha ya elimu nchini kwa kutumia Kiswahili kwenye ngazi zote hadi shule za sekondari na chuo kikuu. [1]
Kenya imetangaza Kiswahili kuwa lugha ya taifa lakini inaendelea kutumia Kiingereza katika shughuli za serikali. Watu wa matabaka ya juu mara nyingi hupendelea kutumia Kiingereza wakiona ni lugha bora. Lakini tangu 1986 wanafunzi wote wanatakiwa kujifunza Kiswahili katika shule za sekondari. Tatizo mojawapo ni kuwepo wa makabila makubwa kama Wakikuyu au Waluo wenye wasemaji wengi sana katika eneo moja, hali isiyosaidia kujifunza lugha tofauti. Pia kaskazini na magharibi mwa Kenya wenyeji wengi si wasemaji wa lugha za Kibantu nao hawaoni Kiswahili ni lugha rahisi.
Uganda inatumia Kiswahili kama lugha ya polisi na jeshi, hali ambayo haikuongeza upendo wa Waganda kwa lugha kutokana na historia ya Uganda ya kuwa na vita na serikali za kijeshi. Lakini kinasikika pia kama lugha ya biashara masokoni. Pamoja na kwamba Waganda walikichukulia Kiswahili kama lugha ya kitumwa lakini pia lugha hii ilionekana kuwa na ustaarabu wa Kiarabu zaidi, yaani Uislamu. Lugha ya Kiswahili ilitumika katika kueneza dini hiyo.
Mashariki mwa Kongo Kiswahili kimeenea sana: ni moja kati ya lugha nne za kitaifa katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo.
No comments:
Post a Comment