Saturday, 15 July 2017
Watumishi 450 Washinda Rufaa ya vyeti feki, Hakuna Mishahara Mipya
SERIKALI imetangaza kuwa watumishi wa umma 450 wameshinda rufaa, kati ya waombaji 1,050 ambao waliwasilisha rufaa zao katika mamlaka husika baada ya kutajwa katika orodha ya watumishi wenye vyeti feki.
Akizungumza na waandishi wa habari jana jijini Dar es Salaam, Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma, Utawala Bora, Dk Laurian Ndumbaro alisema serikali iliendesha uhakiki wa vyeti vya kidato cha nne, sita na ualimu ambako watumishi wa umma 9,932 walibainika kukutwa na vyeti feki.
Dk Ndumbaro alisema baada ya kutangazwa kwa orodha hiyo ya watumishi wenye vyeti feki, watumishi 1,050 walikata rufaa na watumishi 450 pekee walishinda rufaa hizo huku watumishi 8,800 wakiridhika na matokeo hayo.
Aliongeza kuwa rufaa hizo zilizokubaliwa ni kwa watumishi wale waliokuwa wakitumia majina ya waume zao baada ya kuolewa, ambayo yalitofautiana na majina yaliyopo kwenye vyeti na baada ya uhakiki walionekana kama ni vyeti feki.
“Bahati mbaya Watanzania wanapoolewa wanatumia majina mawili ya waume zao badala ya jina moja, hivyo ilileta usumbufu wakati wa uhakiki baada ya vyeti vyao kuonesha majina tofauti,” alisema Dk Ndumbaro.
Aidha, alifafanua kuwa wengine walioshinda rufaa ni wale ambao majina yao ya kidato cha nne yalikuwa tofauti na majina ya kidato cha sita kwa kuwa kidato cha nne hakutumia jina la kati kama kidato cha sita, lakini baada ya kujieleza, wamekubaliwa rufaa na kurejeshwa katika utumishi wa umma.
Wengine waliokubaliwa ni wale walioonekana kuwa na makaratasi ya vyeti ambayo sio sahihi, lakini matokeo ni sahihi na wamesoma katika shule husika, lakini baada ya kuhojiwa na Baraza la Mitihani la Taifa (NECTA), walionekana kuwa walipata vyeti kwenye shule zao, lakini karatasi iliyotumika haikuwa sahihi kutokana na wao kuchelewa kuchukua vyeti vyao kwa miaka mingi.
“Hawa wa kundi hili hawakuwa na lengo la kubadilisha matokeo hivyo imeonekana wanastahili kurejeshwa kwenye utumishi wa umma kwa kuwa walipewa vyeti ambavyo havikubadilishwa matokeo,” aliongeza Katibu Mkuu Utumishi.
Dk Ndumbaro pia alizungumzia suala la ajira mpya, akieleza kuwa serikali imeanza kutoa vibali vya ajira mpya kuanzia mwezi ujao, watatangaza nafasi hizo na Watanzania wenye sifa watajaza nafasi hizo 10,184 na nyingi zikiwa kwenye sekta ya afya na elimu.
Juzi, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Angella Kairuki alitangaza kutoa vibali vya ajira 10,184 ili kuziba nafasi zilizoachwa wazi na watumishi wa umma waliobainika kughushi vyeti vya elimu.
Kwa mujibu wa Kairuki, agizo hilo linazihusu Mamlaka za Serikali za Mitaa, Sekretarieti za Mikoa, Wakala wa Serikali pamoja na Taasisi na Mashirika ya Umma. Alieleza kuwa taratibu za kukamilisha mgawo wa nafasi za ajira 4,816 zilizosalia, unaendelea ili kuwezesha wizara na taasisi nyingine zilizokamilisha uhakiki wa watumishi wa umma hivi karibuni kuajiri watumishi wapya kuziba nafasi wazi zilizojitokeza.
Alieleza kuwa serikali imetoa kibali kuajiri watumishi wapya 15,000 ili kuziba pengo lililosababishwa na kuondolewa kwenye orodha ya malipo ya mishahara kwa watumishi wa umma, waliobainika kughushi vyeti baada ya zoezi la uhakiki.
Aprili mwaka huu, Rais John Magufuli alipokea ripoti yenye orodha ya watumishi wa umma ambao kati yao wanadaiwa kuwa na vyeti pungufu, vyenye utata na vya kughushi kutokea kwa Waziri Kairuki. Waliokuwa na vyeti vya kughushi walikuwa 9,932, na Rais aliapa kwamba hawatarudi kazini.
Rais Magufuli aliagiza kufutwa kazi kwa wote waliotajwa kwenye ripoti hiyo na kuzuia mishahara yao ya mwezi huo, lakini hata hivyo bado mlango uliwekwa wazi kwa wenye pingamizi na wapo waliokataa rufaa huku wengine wakienda kwenye mamlaka husika kutafuta ufumbuzi wa suala hilo.
Wiki iliyopita akiwa Dodoma, Dk Ndumbaro alitangaza kuwa wiki hii serikali itatoa vibali 3,000 vya ajira katika sekta ya afya vikiwemo vya madaktari na wauguzi pamoja na maofisa hesabu 535 kwa ajili ya vituo vya afya vya kata ili washughulike na ukusanyaji wa mapato kwenye vituo vya afya na zahanati.
Aidha, Dk Ndumbaro alisema baada ya kumalizika uhakiki, imeonekana kuna watumishi wengine katika utumishi wa umma wanaotakiwa kuwa na sifa za kidato cha nne na wanatakiwa kuwasilisha vyeti vyao kwa uhakiki, lakini hawajafanya hivyo mpaka sasa na walikuwa wanaendelea kupata mshahara kama watumishi wa darasa la saba.
Dk Ndumbaro alisema walitoa waraka unaoelezea kwamba Sera ya Watumishi wa Umma ya mwaka 1998 ilitaka watumishi wote wa umma wawe kidato cha nne badala ya darasa la saba na utekelezaji wa sera ulianza Mei 20, 2004 kwamba kuanzia hapo waajiriwa wote watakaoanza kuajiriwa wawe na sifa ya kidato cha nne.
Alisema baada ya sera hiyo, mtumishi yeyote aliyeajiriwa katika utumishi wa umma kuanzia Mei 20, 2004 ni lazima awe na ufaulu wa kidato cha nne na uliwataka watumishi walioajiriwa kabla ya 2004 kwa sifa ya darasa la saba wachukuliwe kama wamehitimu kidato cha nne yaani wabaki katika utumishi wa umma mpaka watakapostaafu.
Alifafanua kuwa baada ya waraka huo kumekuwa na mkanganyiko mkubwa kwa maofisa utumishi na waajiri mbalimbali wameamua kuwasimamisha kazi watumishi wa elimu ya darasa la saba kitu ambacho sio sahihi.
“Usahihi ni kwamba kuanzia Mei 20, mwaka 2004 watumishi walioajiriwa kuanzia tarehe hiyo wanatakiwa kuwa na sifa ya kidato cha nne lakini walioajiriwa kabla ya tarehe hiyo wataendelea kuwa na sifa yao ya darasa la saba na wataendelea kubaki kwenye utumishi wa umma mpaka watakapofikia wakati wa kustaafu,” alisema Dk Ndumbaro.
Alisema watumishi wote walioajiriwa kuanzia Mei 20, 2004 ambao hawajawasilisha vyeti vyao kwa ajili ya kuhakikiwa na Baraza la Mitihani mishahara yao isimamishwe kuanzia mwezi huu hadi hapo watakapowasilisha vyeti hivyo kwa uhakiki.
Aidha, alisema watumishi wote ambao miundo ya maendeleo ya utumishi wao iliwataka kuwa na sifa ya kidato cha nne wakati wanaajiriwa na ambao hawajawasilisha vyeti vyao kwa ajili ya kuhakikiwa mishahara yao isimame kuanzia mwezi huu hadi hapo watakapowasilisha vyeti kwa ajili ya uhakiki.
Akizungumzia suala mishahara mipya, Dk Ndumbaro alisema serikali haikupanga kuongeza mishahara katika mwaka huu wa fedha, bali Rais John Magufuli alisema anafikiria kutoa nyongeza na sio mishahara mipya na hilo linafanyiwa kazi na litakapokamilika taarifa itatolewa. “Kuna tofauti kati ya mishahara mipya na nyongeza, Rais alisema atatoa nyongeza na sio mishahara mipya,” alisisitiza
Chanzo: Habarileo
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment