Friday, 21 July 2017

Wakimbizi rudini Burundi -JPM

Rais John Magufuli amempongeza Rais Pierre Nkurunziza wa Burundi kwa juhudi zake za kusimamia amani nchini mwake.


Ametoa ushauri kwa wakimbizi wa Burundi hapa nchini, kuitikia wito wa Rais wao, aliyewataka warudi nchini mwao kwenda kulijenga Taifa lao kwa kuwa hali ni shwari. Rais Magufuli aliyasema hayo jana kwenye mkutano wa hadhara, uliofanyika kwenye Uwanja wa Posta wilayani Ngara Mkoa wa Kagera, ambao pia ulihudhuriwa na Rais Nkurunziza.
Katika mkutano huo, Rais Magufuli alimuagiza Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mwigulu Nchemba, kusitisha utoaji wa uraia kwa wakimbizi hao ili utaratibu huo usitumiwe kama kigezo cha watu kuzikimbia nchi zao.
“Siwafukuzi wakimbizi, ila muanze kuchukua hatua kwa hiari ya kurudi kwenu. Kama Burundi kungekuwa hakuna amani, Rais wenu angekuwa hapa?” Alihoji Rais Magufuli na kuagiza, “Waziri wa Mambo ya Ndani acha kutoa uraia kwa wakimbizi.”
Mapema, akizungumza katika mkutano huo wa hadhara, Rais Nkurunziza aliwaomba wananchi wake walioko kwenye kambi za wakimbizi mkoani Kigoma kurudi Burundi, kwani kuna amani ili waijenge nchi yao. Rais Nkurunziza aliitumia fursa hiyo, kumshukuru Rais Magufuli kwa Tanzania kuwapokea wakimbizi kutoka Burundi.
“Nawashukuru Watanzania wote kwa kuwapokea wakimbizi kutoka Burundi. Burundi leo kuna amani hivyo nawaomba warudi waijenge nchi yao. Ningependa ushirikiano kati ya Watanzania na Warundi uzidi kuimarika kwa kufanya kazi na biashara kwa pamoja,” alieleza Rais Nkurunziza.
Awali, Nchemba alimweleza Rais Magufuli kuwa zaidi ya wakimbizi 160,000 wa Burundi, wamepewa uraia nchini, wengine 150,000 wamerudi Burundi kwa hiari na waliopo ni 247,000. Aliongeza kuwa mpaka sasa wakimbizi 5,000 wamejiandikisha wanataka kurudi Burundi kwa hiari.
Mbali na suala la wakimbizi, Rais Magufuli alisema Tanzania na Burundi zinataka kuimarisha uhusiano wa kiuchumi na ndiyo maana kwenye ziara hiyo mawaziri wa fedha wa nchi zote mbili walikuwepo. Rais Magufuli aliwataka wananchi wa Ngara na Watanzania kwa ujumla, kufanya biashara na Warundi kwa bidhaa mbalimbali kama vile mchele na ndizi.
Aidha, Rais Magufuli aliwaahidi wananchi wa Ngara kuwa maandalizi ya kujenga barabara ya Rulenge – Nyakahura na barabara ya Nyakanazi – Ngara – Rwanda kwa kiwango cha lami yanaendelea vizuri

No comments:

 

ADVERTISE WITH US

AFRICAN FASHION

PLACE YOUR ADS HERE!