Mungu Mkubwa! Dawa mpya ya kupambana na Virusi vya Ukimwi (VVU) imegunduliwa na kuanza kutumika nchini Kenya ambapo ndani ya muda mfupi tangu ianze kutumika, imeonesha mafanikio makubwa na kuleta faraja kwa waathirika pamoja na ndugu zao kwenye ukanda mzima wa Afrika Mashariki, ikiwemo Tanzania.
Kenya imekuwa nchi ya kwanza barani Afrika kuanza kuitumia dawa hiyo ya vidonge ambayo imeonesha ufanisi mkubwa wa kuzuia virusi visiendelee kuzaliana huku ikiviua vile ambavyo tayari vipo mwilini na hivyo kuboresha na kurefusha maisha ya maelfu ya watu wanaosumbuliwa na magonjwa nyemelezi na ambayo hayakubali tiba nyingine.
DOLUTEGRAVIR NI NINI?
Kwa mujibu wa daktari mmoja aliyezungumza na gazeti hili kwa masharti ya kutoandikwa jina gazetini, Dolutegravir au Tivicay ambalo ni jina lake la kibiashara, ni dawa ya vidonge ambayo mpaka sasa ndiyo inayotajwa kuwa na uwezo mkubwa wa kupambana na VVU (HIV), baada ya kuanza kutumika nchini Marekani mwaka 2013 na kuonesha mafanikio makubwa.
“Ufanisi wake, unatajwa kitaalamu kwamba ni kwa sababu ipo kwenye kundi la ‘integrase inhibitors’ ambapo huingilia mfumo wa kuzaliana wa virusi na kuuvuruga kabisa,” alisema daktari huyo na kuendelea kufafanua.
Kwa kawaida, mtu anapopata Virusi vya Ukimwi, kila kirusi hupitia hatua saba kabla ya kuzalisha virusi vingine vingi. Hatua hizo huanza kwa kirusi kujishikiza kwenye moja ya seli zinazolinda mwili. Baada ya hapo, kirusi kinatengeneza utando na kufunika seli zinazolinda mwili, kisha kinajipenyeza mpaka ndani kabisa ya seli.
Hatua ya tatu, kirusi kikiwa ndani ya seli, kinaibadilisha seli iendane nacho kila kitu mpaka vinasaba (DNA), kitaalamu inaitwa ‘reverse transcription’. Baada ya hapo, kirusi huzalisha kichocheo cha integrase kinachokiwezesha kupenya mpaka kwenye kiini cha seli kisha kwa kwa kutumia vinasaba vya seli iliyopo kwenye kiini, kirusi huanza kuzalisha protini maalum (HIV-Protein) kwa wingi.
Protini hii, baadaye ikiungana na kichocheo kiitwacho protease kinachozalishwa na kirusi aliyepo mwilini, hubadilika na kuwa virusi vingi vipya ambavyo baadaye huchomoza nje ya seli vilikozalishwa, navyo huanza kushambulia seli nyingine kwa mfumo uleule na kusababisha kasi ya kuzaliana virusi ndani ya mwili kuwa kubwa sana.
“Dolutegravir inachokifanya mwilini, inazuia uzalishaji wa kichocheo cha integrase kutoka kwenye kirusi kilichopo ndani ya seli, na hivyo kuzuia kirusi kutumia vinasaba vya seli kuzalisha HIV-Protein, kwa hiyo moja kwa moja inakuwa imeharibu kabisa mfumo wa virusi kuzaliana, huku kwa wakati huohuo pia ikikidhoofisha kirusi kilichopo ndani ya seli,” alisema daktari huyo.
Mwaka 2015, Shirika la Afya Duniani (WHO) lilipendekeza DTG iwe chaguo la kwanza kwa watu wazima na vijana, lakini hadi siku za karibuni watu wanaoishi na VVU katika nchi kama Kenya, walikuwa hawawezi kupata dawa hizo kutokana na uhaba wake.
Zipo taarifa kuwa kuna baadhi ya Watanzania wanakwenda Kenya kuzifuata dawa hizo ili wazitumie kutokana na wanayoyasikia kutoka kwa waliozitumia, jambo linalowafanya wengi wakae mguu pande, mguu sawa kuzifuatilia.
Dk. Godfrey Chale ambaye aliwahi kufanya kazi Hospitali ya Taifa ya Muhimbili, alipozungumza na gazeti hili, alisema dawa hizo hazijafika hapa nchini lakini zimetokana na utafiti uliofanyika Kenya.
Alisema utafiti kama huo uliwahi kufanyika Muhimbili na kuhusisha baadhi ya askari polisi, lakini hajui uliishia wapi hivyo akashauri tuwaulize mawaziri wanaohusika na wizara ya afya.
Alipotafutwa Waziri wa Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Ustawi wa Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu hakuweza kupatikana jana kuzungumzia dawa hizo kutumika nchi jirani na kama Tanzania ina mpango wowote wa kuingiza dawa hiyo nchini.
Hata alipotafutwa naibu wake, Dk. Hamisi Kigwangallah kwa njia ya simu, simu yake iliita bila kupokelewa na hata alipotumiwa ujumbe wa maandishi kuulizwa, hakujibu.
Akizungumza kwenye mkutano wa waandishi habari mjini Nairobi, Jumatano iliyopita, Dk. Peter Kimuu, ambaye ni mkuu wa idara ya sera za afya na mipango katika Wizara ya Afya ya Kenya, alisema dawa hiyo mpya haina madhara mengi kwa wagonjwa wanaoishi na HIV na haina hatari ya dawa kuwa sugu.
Alisema DTG ni nzuri kwa vile ina madhara madogo sana kulinganisha na dawa nyinginezo.
Naye Naibu Mkurugenzi wa Huduma za Afya, Wizara ya Afya Kenya, Dk. Martin Sirengo, alikuwa na furaha alipokuwa anazungumza juu ya matibabu hayo mapya. Hata hivyo alisema bado changamoto kubwa iliyopo ni upatikanaji wake.
“Tuna changamoto kutokana na kwamba haipatikani kibiashara kuweza kuwapatia waathirika wote matibabu. Ni dawa mpya kwa hiyo uzalishaji wake utachukua muda na tunaanza polepole. Pili matibabu yanabadilika kutoka watu kupewa vidonge vitatu kila siku ambayo ni mchanganyiko usio rahisi hadi kidonge kimoja,” alisema Dr. Sirengo
“Nilikuwa na tatizo la mara kwa mara la kutokuwa na hamu ya kula, lakini sasa hamu yangu ya kula imerejea, mwili wangu unafanya kazi vizuri, nainuka kitandani, ama kweli Mungu mkubwa,” alisema mkazi wa Nairobi, Ogutu Dugu alipozungumza na Taasisi ya Reuters Foundation.
Ogutu alianza kutumia dawa hizo mwaka huu kwa sababu tiba nyingine hazikuwa zinamfaa. Ogutu, ambaye ameishi na VVU kwa miaka 15, alisema kiwango cha VVU mwilini mwake kimepungua kwa kiasi kikubwa kutoka virusi 450,000 hadi 40,000 tangu aanze kutumia dawa hiyo.
Nchi za kusini mwa Jangwa la Sahara zimekuwa zikiathiriwa sana na Virusi vya Ukimwi kwa miongo kadhaa na karibu robo tatu ya wakazi wake wana Virusi vya Ukimwi na Ukimwi.
“Shirika la Umoja wa Mataifa la Ukimwi (UNAIDS) linalenga kuwa asilimia 90 ya watu watakaogundulika kuwa na VVU wawe wamepata dawa hiyo ifikapo mwaka 2020. Karibu asilimia 15 ya wagonjwa wa VVU hawawezi kutibiwa kwa kuwa dawa hazifanyi kazi mwilini mwao,” alisema Sylvia Ojoo, Mkurugenzi wa Shule ya Afya ya Chuo Kikuu cha Maryland nchini Kenya, ambaye anasimamia dawa hizo.
No comments:
Post a Comment