Saturday, 8 July 2017

Nyama kuwa na bei elekezi

BODI ya Nyama nchini imesema inafi kiria namna ya kuanza kupanga bei elekezi ya nyama kuanzia mwakani, ambapo kwa sasa wanakamilisha uwepo wa miundombinu sahihi ya kupimia mifugo katika kila halmashauri.


Ofisa Mifugo wa Bodi ya Nyama, Ezekiel Maro alisema hayo katika Maonesho ya 41 ya Biashara ya Kimataifa ya Dar es Salaam (DITF) yanayoendelea katika Barabara ya Kilwa jijini Dar es Salaam.
Alisema katika kupanga bei hiyo ni lazima kuwe na utaratibu, ambao hautamuonea yeyote na utakuwa wa haki. Hata hivyo, alisema bei hiyo haiwezi kufanana maeneo yote nchini.
Alisema Bodi hiyo haiwezi kuanza kupanga bei hiyo mpaka kuwe na miundombinu sahihi ya kupima mifugo, ambapo kwa sasa wanaelekeza halmashauri kufunga mizani ambayo ni ya kidigitali katika minada.
Aliongeza kuwa katika maeneo hayo ni lazima kuwe na kilinge na pindi wakimaliza, wataweza kuanza kupanga bei. Alisema katika kuhakikisha hatua hiyo inafikiwa, Bodi itaimarisha vyama vya wadau wa nyama kama vyama vya wafugaji, wafanyabiashara wa nyama na mifugo, wasindikaji na hata vyama vya mifugo ya nguruwe.
Alisema tayari Bodi imewajengea uwezo wanachama hao ili kuwa imara na kuweza kusimamia sekta ya nyama kwa umakini. Alisema bei elekezi ya nyama, itapangwa kwa kuangalia uzito halisi alionao mfugo kabla ya kuchinjwa. Endapo atakuwepo mdau yeyote atakayeuza kwa bei nyingine, wahusika katika vyama hivyo wataingilia kati.
Alisema kwa Bodi kupanga bei ya nyama, walaji wategemee kupata thamani ya fedha yao kwa ubora wa nyama, na biashara ya nyama inatakiwa ifanywe katika nyumba maalumu iliyoidhinishwa.

No comments:

 

ADVERTISE WITH US

AFRICAN FASHION

PLACE YOUR ADS HERE!